Thursday, March 01, 2012

MUONGOZO KWA WAHITIMU KIDATO CHA NNE.

Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini quran(3:139).

Huzuni ikipitiliza humpelekea mtu kukata tamaa na kutoona thamani ya maisha na hata kufikia hatua ya kunywa sumu au kujiua wakati furaha ikizidi humfanya mtu akasahau majukumu mengine mazito yaliyo mbele yake.

Matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni yamewaacha wanafunzi na wazazi wengi kwenye majonzi huku wachache wakiwa na furaha. Hii ni kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliomaliza kutofanya vizuri katika mitihani yao.

Katika matokeo hayo, kati ya watahiniwa 426,314 waliofanya mtihani huo Oktoba mwaka jana, ni wahitimu 33,577 sawa na asilimia 9.98 waliopata daraja la kwanza hadi la tatu. Wahitimu 146,639 sawa na asilimia 43.60 walipata daraja la nne na 156,089 sawa na asilimia 46.41 walifeli kabisa kwa kuambulia daraja la sifuri.

Vyovyote iwavyo, matokeo haya si ya kujivunia kwani yanatoa fursa finyu kwa vijana wetu kuweza kujiendeleza.

Pamoja na hilo, kubwa ni kuangalia namna bora ya kusonga mbele kwa wale ambao hawakufanya vema wakijipanga upya kuangalia ni yepi ya kufanya ili kuweza kusonga mbele baada ya jitihada zao zilizotangulia kutofanikiwa wakati wale waliofaulu vizuri wakiweka mipango na mikakati madhubuti itakayowawezesha kuendelea zaidi.

Jambo la kwanza analopaswa kulitambua mwanafunzi ni kukubali matokeo aliyoyapata. Kuukana ukweli huu hakutakuwa na msaada kwake. Ni wazi zinaweza kuwapo kasoro za hapa na pale katika masuala ya usahihishaji lakini mchango wake katika matokeo ya jumla unaweza usiwe mkubwa sana. Hata hivyo, endapo itathibitika kuwa kuna hujuma za makusudi dhidi ya wanafunzi au shule fulani zilizopelekea wanafunzi kufeli au kufutiwa matokeo, ni vema suala hilo likafuatiliwa kwa kina na taasisi husika ili haki itendeke.

Kwa muhtasari, matokeo ya kidato cha nne unaweza kuyagawa katika makundi ya daraja la kwanza, daraja la pili, daraja la tatu, daraja la nne na daraja sifuri. Aidha unaweza kuyagawa katika makundi manne - walio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi; walio na sifa za kujiunga na vyuo vya ualimu lakini hawana sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi; walio na sifa za kujiunga na vyuo vingine; na waliofeli kabisa ambao wanakosa sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano na vyuo kwa vigezo vya ufaulu wa kidato cha nne.


KUJIUNGA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA UFUNDI

Awali ya yote ifahamike kuwa wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya serikali ni wale wanaotoka shuleni (school candidates).

Kadhalika wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja katika vyuo vya ufundi mfano Dar es Salaam Institute of Technology (DIT), Mbeya Institute of Science and Technology (MIST), Arusha Technical College na kama hivyo, huwa na sifa sawa na wale wanaochaguliwa kuijunga na kidato cha tano katika michepuo ya sayansi. Idadi ya wanafunzi hawa huwa si kubwa sana.

Mwanafunzi aliyefaulu kwa daraja la kwanza au la pili ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano au chuo cha ufundi katika shule na vyuo vya serikali. Aidha hata baadhi ya wahitimu waliopata daraja la tatu wana nafasi nzuri ya kuchaguliwa. Si tukio la kawaida mwanafunzi aliyepata daraja la nne kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano au chuo cha ufundi.

Mara nyingi changamoto wanayokuwa nayo wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu ni aina ya michepuo na shule za kuendelea nazo. Ni jambo la kawaida kukuta kijana akifaulu masomo mengi na kisha kusoma mchepuo ambao hana mapenzi nao sana. Hili husababishwa na mazingira ya ujazaji fomu za michepuo ya kuendelea nayo baada ya kuhitimu masomo. Hutokea kuwa mchepuo anaoupenda sana ana shaka ya kufanya vizuri na hivyo kuchaguwa michepuo mingine. Ama kwa upande wa shule, hutegemeana na nafasi, ufaulu wa wanafunzi na idadi ya wanafunzi walioomba katika Shule husika.

Baadhi ya wanafunzi wanapokosa michepuo au shule walizoomba huhangaika na kutumia muda mwingi wakitaka kubadilisha. Uzoefu unaonyesha kwamba ni sehemu ndogo za sana ya wanafunzi hao ambao hufanikiwa. Ushauri wetu ni kwamba endapo kijana atachaguliwa katika shule asiyoipenda na hakuna sababu za kiafya za kumfanya asiende katika shule hiyo pengine kutokana na hali ya hewa, au kachaguliwa mchepuo asioupenda na familiya yake haina uwezo wa kumsomesha shule binafsi, basi atulizane katika hicho alichopata na ajikite zaidi katika masomo kwani anaweza pia kufanikiwa katika fursa hiyo aliyoipata.

MASOMO KABLA YA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO (PRE FORM FIVE).
Changamoto nyingine ambayo huwakuta vijana wa kundi hili ni kuanza kusoma tuisheni za masomo ya kidato cha tano kabla ya uchaguzi kufanyika. Utata wa jambo hili ni kama tulioueleza hapo juu wa mwanafunzi kuchaguliwa mchepuo tofauti kabisa na masomo anayosoma. Kwa mfano kuna kijana tunayemfahamu akisoma masomo ya mchepuo wa Economics, Geography na Mathematics (EGM) lakini akachaguliwa mchepuo wa History, Kiswahili na Language (HKL). Tofauti iliyoje! Katika hilo inashauriwa kuwa kama mwanafunzi hana hakika ya kusoma katika shule binafsi, asianze masomo hayo mpaka baada ya uchaguzi wa kidato cha tano kufanyika. Na ikibidi kujisomea asome vitu vya jumla kama masomo ya lugha, kompyuta nk.
KUJIUNGA NA SHULE BINAFSI
Kwa wale waliokwisha amua au lazima wasome katika shule binafsi, ni muhimu kufanya utafiti juu ya ubora wa shule hizo kitaaluma, maadili na stadi nyingine za maisha. Aidha ni muhimu kufuatilia juu ya kiwango cha ada, muda wa kuchukuwa na kurejesha fomu za maombi, tarehe ya usaili na ya kufungua shule. Hutokea mwanafunzi akapoteza muda na hatimaye kuhangaika kutafuta shule wakati shule nyingi zimeshasimamisha kupokea wanafunzi.

Kuna wanafunzi waliopata daraja la tatu ambao hawatapata nafasi ya kujiunga na kidato cha tano. Hata hivyo vijana waliopata daraja la tatu na sehemu ndogo ya waliopata daraja la nne huwa wanapata sifa na wanaweza kujiunga na kidato cha tano katika shule binafsi endapo uwezo wa familiya unaruhusu. Hii ni kutokana na kanuni za Wizara ya Elimu ambazo zinamruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo ya kidato cha tano endapo amefaulu katika kiwango cha angalau alama C kwa masomo matatu au zaidi hata kama masomo aliyofaulu hayatengenezi mchepuo wowote mfano Civics, Biology na English huku akiwa amepata alama D au chini yake katika masomo mengine. Endapo familiya itamudu kumsomesha kidato cha tano kati shule binfasi, ni vema kijana akapata ushauri wa wazazi, walimu na wazoefu wengine juu ya mchepuo stahiki unaomfaa. Mara nyingi wanafunzi wa aina hii huwa wanashindwa kutofautisha baina ya matashi ya nafsi na uwezo binafsi wa kimasomo. Kwamba kijana tuliyemtaja hapo juu asome mchepuo wa CBG au HGL ni suala linalohitaji tafakuri pamoja na mhusika.

KUJIUNGA NA VYUO VYA UALIMU
Kuna wanafunzi waliopata daraja la tatu na hata daraja la nne ambao hawatachaguliwa kujiunga na kidato cha tano lakini watachaguliwa kujiunga na vyuo vyuo vya Ualimu. Kwa mujibu wa kanuni zilizopo sasa, kiwango cha ufaulu cha mwisho kuchukuliwa ni daraja la nne na pointi 28. Pamoja na kujaza nafasi za masomo ya Ualimu ngazi ya cheti, mwanafunzi atapaswa kuomba rasmi nafasi hizo kupitia Wizara ya Elimu baada ya matokeo kutoka na nafasi kutangazwa rasmi. Aidha kutokana na uchache wa nafasi katika vyuo huwa si wote walio na sifa wanaoweza kuchaguliwa. Wanafunzi wenye sifa lakini hawakuchaguliwa katika vyuo vya serikali, wanaweza kujiunga na vyuo binafsi vya ualimu endapo uwezo wa familiya kiuchumi unaruhusu.

KUJIUNGA NA VYUO VINGINE.
Wapo vijana ambao licha ya kuwa na sifa za kuchaguliwa katika vyuo vya ualimu, huwa hawachagui au hawaendi hata baada ya kuchaguliwa kwasababu zao binafsi. Kama uwezo wa familiya unaruhusu na inaona kusoma ualimu si kipaumbele cheo, haina tatizo. Hata hivyo, ni vema kuangalia fursa zilizopo na uwezo wa familiya kiuchumi. Kijana anapaswa kufahamishwa na kufahamu kuwa si busara kwa familiya yenye uwezo duni wa kiuchumi, kama zilivyo familiya nyingi za kitanzania, kumsomesha kijana katika ngazi hii kwa gharama kubwa wakati kuna wengi wanahitaji kuendelezwa kitaaluma katika familiya.

Wale wote waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi au vyuo ualimu, fursa pekee waliyonayo ni kujiunga na vyuo vingine vinavyotoa kozi mbalimbali katika ngazi ya cheti katika Biashara, Utawala, Ufundi, Afya, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Maendeleo ya Jamii, nk. Vyuo kama Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Usimamizi wa Fedha (IFM), Uhasibu (TIA), Kodi, Utumishi wa Umma, Serikali za Mitaa (LGTI), Ardhi, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka, Mahakama, Ustawi wa Jamii, Elimu ya Watu Wazima, ni mifano michache katika ya vyuo vingi vilivyopo. Changamoto kubwa katika vyuo hivi ni uwezo wa kuzimudu gharama za mafunzo hayo. Hata hivyo, mara nyingi gharama za mafunzo katika vyuo vya Serikali kama Afya, Kilimo, Ufugaji, Ufundi, Uvuvi, nk huwa nafuu sana kuliko vyuo binafsi.

WANAFUNZI WALIOFELI KABISA
Mwanafunzi aliyefeli kabisa na kupata daraja la sifuri, hana fursa yoyote katika zote zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo anakuwa amepata cheti cha kuhudhuria masomo (leaving certificate) ambacho huwa na msaada fulani katika maisha kwani kuna wakati huhitajika vijana waliomaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wao.

Pia kuna fursa zinazohitaji vijana waliomaliza shule ya msingi ambazo bado zinaweza kutumiwa na vijana hawa. Kwa mfano kuna fani mbalimbali zinazotolewa na vyuo vilivyo chini ya VETA ( vya serikali na binafsi) kama ufundi, udereva, usafi, utunzaji bustani, ushonaji, upishi nk ambazo zinaweza kutumiwa vema na vijana ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne.

Ni muhimu kutaja hapa kwamba si wale tu waliofeli ndio wanaoweza kuzitumia fursa za mafunzo ya VETA bali hata wale waliopata daraja la nne na hata daraja la tatu ambao ama hawakupata fursa za kuchaguliwa kidato cha tano au familiya zao hazimudu kuwasomesha katika shule au vyuo vya kujilipia.
KURUDIA MITIHANI

Wanafunzi wengi wanaofanya vibaya katika mitihani yao, jambo la haraka linalowajia vichwani ni kurudia mitihani. Ndio maana siku hizi vituo vinavyotoa mafunzo kwa wanaorudia mitihani vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ni kwakuwa soko linakuwa na wateja wameongezeka.

Pamoja na kuunga mkono na kuheshimu juhudi za wanaotoa mafunzo hayo, tungependa tutanabahishe kwamba ili kuepusha upotevu mwingi wa muda na pesa, ni vema mwanafunzi akawa akijiandaa kurudia mitihani huku akijifunza ujuzi mwingine. Uzoefu unaonyesha kuna wanafunzi wanaorudia mitihani na matokeo yao kuwa mabaya kuliko ya mwaka uliotangulia. Aidha kuna wanafunzi waliorudia mitihani zaidi ya mara moja na bado hawakufanikiwa kupata alama C (credits) tatu au zaidi walizohitaji ili wajiunge na kidato cha tano.

Endapo mwanafunzi atajiandaa kurudia mitihani huku anapata ujuzi mwingine mfano udereva, ufundi,nk anakuwa katika nafasi nzuri ya ajira hata asipofaulu mitihani yake anayorudia. Ni uzuri ulioje endapo atapata vyote - credits na huku ana cheti cha ujuzi wake.

Jambo hili linawezekana endapo kijana ataugawa vizuri muda wake chini ya muongozo wa familiya. Kwa mfano asubuhi anakwenda chuoni kupata ujuzi na jioni anakwenda tuisheni kwa ajili ya kurudia mitihani. Aidha endapo mwanafunzi hatofanikiwa kupata credits, anaweza kuanza kazi huku ajiandaa taratibu kurudia mitihani yake. Wengi wamefanikiwa kwa utaratibu huu.

KUKATA RUFAA JUU YA MATOKEO
Wapo wanafunzi ambao wanakuwa hawakuridhika na matokeo waliyopata wakiamini hawakutendewa haki katika usahihishaji pengine kwa kuzingatia rekodi za matokeo yao katika mitihani ya shuleni au kwa jinsi walivyofanya mitihani.

Kwamba hatupingi jambo hili ndivyo pia tungependa kusisitiza kuwa wakati kijana akikusudia hilo ni vema akaendelea na mipango mingine ya kujiendeleza kama tulivyoitaja hapo juu. Hii ni kwasababu ni wanafunzi wachache sana ambao matokeo yao hubadilika baada ya mitihani yao kusahihishwa upya. Aidha anaweza kupoteza muda mwingi akisubiri hatma ya rufaa yako na kisha majibu kuja asivyotarajia.
UFADHILI WA MASOMO
Hutokea wanafunzi waliopata nafasi za masomo katika shule binafsi au vyuo vinavyohitaji kujilipia wakawa hawana uwezo wa kujisomesha na hivyo kuhangaika huku na kule kutafuta ufadhili. Ukweli ni kuwa ni wachache sana ambao hufanikiwa. Hii ni kutokana na kutokuwa na taasisi rasmi zinazotoa ufadhili katika viwango hivi ya elimu nchini.

Pamoja na kutokatishana na tamaa, ni vema kijana anapokuwa katika hali hiyo kutafuta shughuli itakayokuwezesha kujenga nguvu za kiuchumi na kisha kuweka akiba kwa ajili ya kujisomesha. Unaweza kuweka malengo ya kusoma huku ukifanya kazi. Endapo shughuli zako hazikupi fursa ya kusoma huku ukifanya kazi, unaweza kuahirisha kusoma hadi kipindi fulani baada ya kujiimarisha kiuchumi. Endapo hilo litakuwa gumu kulitekeleza, familiya iangalie uwezekano wa kuuza sehemu ya rasilimali ilizo nazo ambazo hazitaithiri familiya nzima endapo zitauzwa.

Tuhitimishe kwa kusema, matokeo vyovyote yawavyo hayawezi kuwa ndio mwisho wa maisha. Siku zote wanaofanikiwa ni wale wanaotazama mbele huku wakijifunza kwa yaliyowatokea. Walofaulu washukuru huku wakijipanga; waliofanya vibaya wasubiri huku wakijifuza. Tumia vizuri kila fursa unayoipata bila kujali udogo wake. Jifunze kwa wengine, uliza, pata miongozo kwa waliokutangulia, na amini kuwa ipo siku utafanikiwa. Washindi huwa hawaachi, na wenye kuacha huwa hawashindi.

Imetolewa na:

Kitengo cha Elimu - Jumuiya ya Wataalam wa Kiislam Tanzania (TAMPRO)

TAMPRO imeandaa kitabu kinachoonyesha orodha ya vyuo ambavyo mhitimu wa kidato cha nne na kidato cha sita anaweza kujiunga, muda wa kujiunga, sifa za kujiunga na gharama za masomo. Kitabu hicho kitatoka hivi karibuni inshaAllah.

6 comments:

  1. Allah awawezeshe zaidi na zaidi katika utendaji wenu....illa nlikuwa naomba vitabu viwe vinazalishwa kwa wingi kwani mwaka uliopita hitajio lilikuwa kubwa pale MUSLIM UNIVERSITY OF MOROGORO lakini vitabu vilifika vichache..wabillah tawfiq

    ReplyDelete
  2. NASHUKURU KWA MUONGOZO

    ReplyDelete
  3. ni zipi sifa za kujiunga na chuo cha maendeleo ya jamii

    ReplyDelete
  4. Mimi ni kijana niliemaliza kidato cha NNE mwaka 2005 na nilipata point 33.lizti slip Yang inasema ni divishen four.samba ni D mbili tu,he ninaweza kupata cheti?

    ReplyDelete
  5. Ni ajabu xana kuona mambo kam haya yakitokea nyakati ngumu kama hizi hasa kwa familia zenye uchumi duni pamoja na kuwa wanajitahid kuweka mikakati mbalimbali juu ya watoto wao ili kuwafikixha japo hata SEDUSI YA MAFANIKIO YAO; Lakin bado wanajikuta wakiingia kwenye dmbwi LA majanga kama haya kwa kweli imeumiza xana kidzygn: For this case government is supporsed to be very careful & accurate to minimize if not totally Remedy of such problem!



    By Juss Onair'etta.

    ReplyDelete
  6. Vip kwa mwanafunzi mwenye 4 ya 32 o level

    ReplyDelete

TUPE MAWAZO YAKO