Friday, November 30, 2012

KATIKA MAWAIDHA YA IMANI PETRO JUU YA MBINU ZA MAKAFIRI.


IRAN YATISHIA KUJITOA NPT

Iran imetishia kujiondoa katika mkataba wa kimataifa unaopinga uendelezaji wa nyuklia, NPT, kama vinu vyake vya nishati hiyo vitashambuliwa. Mwakilishi wa Iran katika Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, Ali Asghar Soltanieh ametoa msimamo wa nchi yake mjini Vienna, Austria akirejerea kitisho cha Israel kuvishambulia vinu vya nyuklia vya nchi hiyo ambacho sasa kimezidi kuongezeka. Ali amesema kuwa uwezekano wa bunge la Iran kuilazimisha serikali kuuzuia ukaguzi wa IAEA kwenye vinu vya nyuklia vya nchi hiyo na hata kujitoa kwenye NPT. Mkataba wa NPT unazuia nchi ambazo hazina silaha za nyuklia kuzitengeneza. Mataifa ya magharibi yana wasiwasi kuwa kujitoa kwa nchi hiyo kwenye NPT ni mwanzo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo taarifa za IAEA zinasema kuwa huenda Iran imefanya utafiti kuhusu utengenezaji wa silaha lakini si kwamba  tayari wanazitengeneza. 

TAIFA HARAMU LA ISRAEL KUJENGA NYUMBA 3,000 ZA WALOWEZI

Siku moja baada ya Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa kuikubalia Palestina kuwa mwanachama asiyekuwa dola kwenye Umoja huo, taifa haramu la Israel imetangaza mpango wake wa kujenga nyumba 3,000 za walowezi katika maeneo inayoyakalia ya Jerusalem Mashariki na kwenye Ukingo wa Magharibi. Licha ya uamuzi huo kuchukuliwa tangu zamani, lakini kutangazwa kwake leo kumetajwa kama ujumbe kwa Wapalestina, kwamba kupatiwa kwao uwanachama huo kwenye Umoja wa Mataifa, hakujabadilisha chochote kwenye sera za makaazi ya walowezi za Israel. Hapo jana, mabalozi wa Israel na Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, waliwaambia wajumbe wa Hadhara Kuu ya Umoja huo, kwamba uamuzi wa kuipa uwanachama Palestina, ulikuwa bahati mbaya na kikwazo kwa juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

MELI YA KIVITA YA IRAN YATIA NANGA SUDAN


Meli ya kivita ya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetia nanga katika bandari ya Sudan katika Bahari Nyekundu.
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran Admeli Habibollah Sayyari amesema manowari hiyo ijulikanayo kama  'Jamaran' na ambayo imetengenezwa kikamilifu nchini Iran imewasili Sudan ikiwa na ujumbe wa amani na kirafiki kwa nchi za eneo na rafiki.
Manowari hiyo ni sehemu ya msafara wa 23 wa Jeshi la Wanamaji la Iran uliotumwa katika Bahari Nyekundu. Msafara wa 22 wa manowari za kivita za Iran ulirejea nchini mapema mwezi huu baada ya kumaliza kazi ya siku 75 katika maji ya kimataifa.
Jeshi la wanamaji la Iran limeimarisha harakati zake katika maji ya kimatiafa kwa lengo la kulinda doria na kusindikiza meli za Iran na za kigeni katika maji hayo. Katika fremu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na maharamia, Jeshi la Wanamaji la Iran limekuwa likilinda doria katika Bahari Hindi na Ghuba ya Aden tokea Novemba mwaka 2008.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya bahari IMO limepongeza juhudi na mafanikio ya Iran katika kupambana na maharamia.

PALESTINA YAWA NCHI MTAZAMAJI WA UN



Palestina imekubaliwa kuwa nchi mtazamaji asiyekuwa mwanachama katika Umoja wa Mataifa.
Katika kura iliyofanyika jana kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Palestina ilifanikiwa kupata kura 138 za ndio mkabala wa kura 9 zilizopinga Palestina kuwa nchi mtazamaji katika Umoja wa Mataifa.
Matokeo hayo yamepandisha juu nafasi na hadhi ya Palestina ambapo sasa inatambuliwa kuwa ni nchi mtazamaji katika Umoja wa Mataifa badala ya jumuiya mtazamaji katika jumuiya hiyo ya kimataifa.
Habari hiyo ya kutambuliwa Palestina kuwa ni nchi mtazamaji badala ya jumuiya katika Umoja wa Mataifa imezusha furaha, vifijo na nderemo huko Palestina. Hatua hiyo inaipa Palestina fursa ya kushiriki katika vikao vya Umoja wa Mataifa na kuboresha uanachama wake katika taasisi za umoja huo.
Mwaka 2011 Wapalestina waliomba kutambuliwa rasmi kama nchi mwanachama katika Umoja wa Mataifa lakini ombi hilo halikufanikiwa kutokana na upinzani wa Marekani na waitifaki wake.
Mara hii pia Marekani pekee kati ya nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imepinga suala la kupewa Palestina sifa ya nchi mtazamaji huku Uingereza ikikataa kupiga kura.

KATIKA KUMBUKUMBU YA LEO IJUMAA


Leo ni Ijumaa tarehe 16 Muharram 1434 Hijria, sawa na tarehe 30 Novemba 2012 Miladia.



Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita aliaga dunia ustadh na karii mashuhuri wa Qur'ani Abdul Basit Muhammad Abdul Samad katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Alianza kujifunza Qur'ani Tukufu akiwa bado mtoto mdogo na alipewa tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani akiwa na umri wa miaka 12. Kipindi fulani Ustadh Abdul Basit alitumia muda wake mwingi kusafiri katika nchi za Kiislamu na kuwahamasisha watu kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ustadh Abdul Basit ameacha kanda nyingi za Sauti ya kiraa yake ya Qur'ani Tukufu ambazo bado zinawavutia wasomaji wengi wa Qur'ani.


BARAZA LA WAASISI MISRI LAPASISHA RASIMU YA KATIBA


Baraza la Waasisi la Misri limepasisha vipengee vya rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo katika kikao kilichofanyika jana.
Moja ya vipengee muhimu vya rasimu ya katiba mpya ya Misri ni kile kinachosisitiza kuwa sheria za Kiislamu ndio marejeo ya sheria zote za nchi hiyo. 


Rasimu ya katiba mpya ya Misri pia inasisitiza kuwa kipindi cha urais wa nchi sasa kitabanwa katika duru mbili, tofauti na ilivyokuwa katika utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo ambaye aliiongoza Misri kwa zaidi ya miaka 30. Rasimu hiyo itawasilishwa kwa Rais Muhammad Mursi ambaye baada ya kuipasisha ataitisha kura ya maoni ya wananchi na kuwa katiba mpya ya nchi hiyo.
Katiba ya zamani ya Misri ilibatilika baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka jana.

MUUNGANO WA TANZANIA UVUNJIKE USIVUNJIKE?



NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR' AN. Part. 1

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

 
كيف تحفظ القرآن في عشر خطوات – حسن أحمد بن أحمد همام

 
Haifichiki kwa kila Muislam ubora wa kuhifadhi Qur-aan Tukufu na fadhla za aliyeihifadhi.
 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
 
“Wale tuliowapa kitabu (Taurati, injili, Zaburi…) wakakisoma kama ipasavyo kukisoma (bila ya kupotoa tafsiri yake wala kutoa hili na kutia lile), hao huiamini hii (Qur-aan wakasilimu). Na wanaokikanusha (hicho kitabu chao wakapinduapindua tafsiri yake na wakaongeza na wakapunguza), basi hao ndio wenye hasara.” Al-Baqarah: 121.
 


“Kisha Tumewarithisha, (tumewapa) kitabu (hiki cha Qur-aan) wale Tuliowachagua miongoni mwao wanaodhulumu nafsi zao (kwa kuwa na maasia mengi kuliko mema). Na wako wa kati na kati, (wana mema kuliko mema). Na wako wanaokwenda mbele kabisa katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.” Faatwir: 32.

 
“Kwa yakini wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Swalah, na katika yale Tuliyowapa wakatoa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai (faida ya) biashara isiyododa (isiyobaga).” Faatwir: 29.

 
Katika hizi Aayah ni dalili ya ubora ya watu wa Qur-aan na kufaulu biashara yao na Allaah.
Ama Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) ni nyingi tunachukua zifuatazo:


 
kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):


 
“Hakuna hasadi ila katika vitu viwili; mtu ambaye Allaah Amempa hekima (elimu) anaisimamia usiku na mchana, na mtu ambaye Allaah Amempa mali naye anatoa sadaka usiku na mchana.” Muslim
 


Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Afaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema, anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
 
“Mbora wenu ni aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” Al-Bukhaariy
 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
 

“Ataambiwa Swaahib al-Qur-aan soma kama ulivyokuwa ukisoma duniani hakika daraja yako peponi ni mwisho wa Aayah utakayosoma.” At-Tirmidhiy
 

Kutoka kwa Sahl bin Mu’adh kutoka kwa baba yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
 

“Mwenye kusoma Qur-aan na akaifanyia kazi yaliyomo atavalishwa mzazi wake taji siku ya kiyama mng’aro wake ni bora kuliko mwangaza wa jua katika nyumba za dunia lau ingekuwa kwenu mnadhani vipi kwa aliyeifanyia kazi.” Abu Daawuud
 

Imepokewa katika Al-Bukhaariy kwamba walikuwa wanatangulizwa watu wa Qur-aan (Ahlul Qur-aan) kuliko wengine katika Swallah na katika kuwazika mashahidi. Pia kuna mtu alimuoa mwanamke kwa Qur-aan aliyokuwa nayo kama mahari.
 

KUHIFADHI QUR-AAN NI KHASWA KWA UMMAH HUU

Allaah Amejaalia Ummah huu kuwa bora kuliko Ummah zingine na Akajaalia wepesi kuhifadhi  Kitabu hiki kimaandishi na kifuani.
 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
 
“Bali hizi ni Aayah waziwazi (zinazokubaliwa) katika vifua vya wale waliopewa ilimu, na hawazikatai Aayah Zetu isipokuwa madhalimu (wa nafsi zao).” Al-‘Ankabuut: 49
 
Na imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy;
 
“Na imeteremshwa kwako Kitabu kisichooshwa na maji unasoma ukiwa umelala na ukiwa macho.” Muslim
 
Itaendelea Ijumaa ijayo inshaa -Allah........................

Thursday, November 29, 2012

UN KUPIGA KURA YA PALESTINA

Rais wa Palestina Mahmud Abbas anapanga leo kushinikiza kupitishwa kura ya Umoja wa Mataifa ya kuitambua Palestina kama taifa. Ujerumani haitaunga mkono jitihada za Palestina za kutaka hadhi ya dola mwangalizi ndani ya Umoja wa Mataifa. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 193 linatarajiwa kupiga kura kwa wingi kuunga mkono ombi hilo, ambalo litaipa Mamlaka ya Palestina kibali cha kujiunga na mahakama za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita mjini The Hague, Uholanzi. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton anasema msimamo wao haubadiliki. Kuna wasiwasi miongoni mwa wanaounga mkono Israel kwamba Wapalestina watajaribu kuishitaki nchi hiyo ya Kiyahudi kwa uhalifu wa kivita katika mahakama ya ICC. Ombi la Palestina limeugawanya Umoja wa Ulaya, huku Ujerumani na Uingereza zikisema zitasusia kura hiyo nayo Ufaransa ikisema itaunga mkono jitihada hizo za kutaka hadi ya uangalizi.

MASHAMBULIO YA KIGAIDI DHIDI YA WAISLAM MAREKANI


Polisi ya jimbo la Texas nchini Marekani inamshikilia raia mmoja wa nchi hiyo kwa tuhuma za kutaka kuwashambulia waumini wa Kiislamu waliokuwa wakisali Msikitini. Polisi ya Texas imeeleza kuwa, Christopher Bane mwenye umri wa miaka 44 anashikiliwa na jeshi la polisi katika jimbo hilo kwa kosa la kutaka kuwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa ndani ya Msikiti mmoja katika mji wa San Antonio. Taarifa za polisi zinasema kuwa, Christopher Bane alikuwa na azma ya kuwashambulia Waislamu hao na kisha ajiuwe. Polisi ya Texas imeeleza kuwa, msamaria mwema mmoja alitoa taarifa hizo kituoni za kutaka kushambuliwa Waislamu. Kabla ya hapo, ofisi ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani katika jimbo la Chicago lilitangaza kushambuliwa Msikiti mmoja ulioko katika mji wa Morton Grove. Baraza hilo limeongeza kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Misikiti miwili iliteketezwa moto katika jimbo la Missouri nchini Marekani.

WAFUNGWA 3,800 WALIOHUKUMIWA KIFO WAPELEKWA SYRIA

Mkuu wa Shirika la Habari la Iraqi al Nakhil amesema kuwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zimewatuma nchini Syria wafungwa 3,800 waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa shabaha ya kupigana dhidi ya serikali ya Rais Bashar Assad wa nchi hiyo.




Muhammad Ali al Hakim amesema kwamba, hadi sasa wafungwa 3,800 waliohukumiwa adhabu ya kifo katika baadhi ya jela za nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Qatar, Saudi Arabia na Kuwait wameachiliwa huru na kupelekwa  nchini Syria ili kutekeleza operesheni za kigaidi.
Mkuu wa shirika la habari la Iraq al Nakhil amesema, Walid Twabatwabai mwakilishi wa Masalafi katika Bunge la Kuwait ndiye anayegharamia kupelekwa wafungwa hao wa Kiarabu nchini Syria kutekeleza operesheni za kigaidi. Walid Twabatwabai miezi mitatu iliyopita aliitembelea Syria na mbali na kushiriki katika maandamano dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo alitangaza kuwa yuko tayari kutoa fedha na kuunga mkono magaidi nchini humo.
Kwa miezi kadhaa sasa Syria inakabiliwa na machafuko ambapo makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za kigeni yanapigana dhidi ya serikali ya Damascus.

MWILI WA HAYATI YASSIR ARAFAT WAFUKULIWA KWA UCHUNGUZI


Mwili wa kiongozi wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat, umefukuliwa kutoka kaburi lake liloko ukingo wa Magharibi mjini Rammala ili kuwawezesha kuufanyia uchunguzi kubaini iwapo aliuwawa kwa sumu. Bwana Arafat alifariki dunia mwaka 2004 nchini Ufaransa baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.


 
Maradhi yaliyopelekea kifo chake hayakubainika. Uamuzi wa kuufukua mwili wa Yasser Arafat katika kaburi lake lililoko ukingo wa Magharibi unafuatia makala ya televisheni iliyodai kupata mabaki ya madini ya kitonoradi aina ya Polonium kwenye nguo zake.
 
Wapalestina wengi wanashuku kwamba huenda Israel ilihusika katika kifo cha kiongozi huyo. Israel imekuwa ikikanusha shutuma hizo.
Uchunguzi wa mauaji dhidi ya Bwana Arafat umeanzishwa nchini ufaransa kufuatia ombi lililowasilishwa na mjane wake.
 

Wednesday, November 28, 2012

HIZBULLAH YAFANYA MAZOEZI YA KIJESHI NA KUIONYA ISRAEL PIA

Gazeti la Al Jamhuriyyah la Lebanon limeandika kuwa, hivi karibuni Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ilifanya manuva kubwa ya kijeshi iliyowashirikisha wapiganaji shupavu wa harakati hiyo wapatao elfu 10.

Gazeti hilo limeendelea kuandika kuwa, manuva hiyo imefanyika kwa minajili ya kujiweka tayari kwa chokochoko zozote za utawala wa Kizayuni wa Israel na yalifanyika katika maeneo kadhaa ya kusini na mashariki mwa Lebanon. 

Aidha gazeti hilo limeandika kuwa, manuva hayo yalifanyika kwa muda wa siku tatu. Manuva hayo yaliyowashirikisha vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 20 yanahesabiwa kuwa ya kwanza na ya aina yake ambayo yamewahi kufanywa na Hizbullah katika maeneo yaliyochini ya udhibiti wake.


Pia katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba utakabiliwa na tsunami ya makombora yenye nguvu zaidi kuliko Fajr 5 katika miji yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ukiwemo Tel Aviv, iwapo utawala huo khabithi utaanzisha tena chokochoko dhidi ya ardhi ya Lebanon. Akizungumza na waumini waliokuwa wakiomboleza Ashura ya Imam Hussein AS kusini mwa Beirut, Sayyid Hassan Nasrullah amehoji kuwa, utawala wa Israel umetiwa kiwewe na makombora machache tu ya Fajr 5 yaliyorushwa na wapiganaji wa Hamas wa Kipalestina, vipi utaweza kustahamili kishindo cha maelfu ya makombora yenye nguvu zaidi ya Hizbullah yatakayokita kwenye miji yote ya utawala huo? Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa, utawala wa Israel unaelekea kusambaratika kwani kwa muda mrefu umekuwa ukiingiwa na kitete mbele ya wanamuqawama.

Viongozi wa Israel wahusishwa na kifo cha Arafat

Mkuu wa Kamati ya Palestina inayochunguza kifo cha Yassir Arafat amesema kuwa viongozi wa Israel walihusika kumuua kiongozi huyo wa zamani wa Palestina. Tawfiq al Tirawi amesema ushahidi uliopo ni wa matamshi yaliyotolewa na viongozi wa Israel waliosema kuwa Arafat lazima auawe ambapo Shaul Mofaz na Ariel Sharon walifanya mazungumzo na kutaka kuuliwa Arafat. Hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano wa utawala wa Kizayuni alieleza kuwa yoyote anayetaka kuchunguza kifo cha Yassir Arafat ajue kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutangaza vita na Israel. Mbali na waziri huyo, makumi ya maafisa wa kisiasa, usalama na kijeshi wa utawala haramu wa Kizayuni walisema kuwa Arafat ni lazima auliwe. Wapalestina wamekuwa wakisisitiza kwa miaka kadhaa sasa kuwa Yassir Arafat aliuliwa kwa sumu na Israel.

SUSAN RICE AKIRI ALIONGOPA KUHUSU KUUAWA BALOZI WA MAREKANI LIBYA

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice amekiri kwamba alitoa taarifa ya uongo kuhusu matukio yaliyopelekea kuuawa balozi wa nchi yake huko Libya miezi kadhaa iliyopita. Awali Rice alikuwa amesema shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, Libya lilikuwa la kigaidi lakini mwishoni mwa wiki alikiri kwamba, waandamanaji wa Kiislamu waliokuwa na hasira baada ya kuonyeshwa filamu inayomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW ndio waliovamia ubalozi huo na kuuchoma moto. Amesema Waislamu walikuwa na haki ya kuonyesha hasira zao lakini akadai kwamba walichupa mipaka katika kuelezea ghadhabu zao.

Matamshi ya Rice yamemuweka katika hali ngumu na Wabunge wa upinzani wameapa kukabiliana na juhudi zozote za Rais Barack Obama za kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje baadaye mwaka ujao. Rice alikuwa amepigiwa upatu kuchukua nafasi ya Hillary Clinton anayemaliza muda wake mapema mwaka ujao.

Tuesday, November 27, 2012

NYEPESI KUTOKA TUME YA KATIBA LEO ASUBUHI


Pamoja na maoni hayo, kuna matukio mawili yaliyojitokeza leo yanafaa ku-share na wengine.


LA KWANZA: Hili limetokea asubuhi Welezo ambapo Mzee Warioba alikuja kujumuika na wana-Tume iliyopo Zanzibar. Mwana-Mkataba mmoja alihoji vipi Wazanzibari waendelee na mfumo uliopo wakati nafasi zote kubwa kubwa katika mihimili mbali mbali ya Dola zinashikwa na watu wa Tanganyika tu.

 Mzee Warioba kama kawaida yake huwa hawezi kustahamili mawazo yasiyokubaliana na yake, akamwambia hivi hajui Tume ya Katiba Makamu Mwenyekiti wake ni Mzanzibari? Mwana-Mkataba akamjibu hivi huyo Jaji Agostino Ramadhani hana sifa za kuwa Mwenyekiti na wewe ukawa chini yake? Mzee Warioba akagwaya. Kimya!


LA PILI: Hili limetokea jioni Welezo. Mwana-Mkataba mmoja alipozungumzia Zanzibar kuwa na mamlaka kamili na Rais wa Zanzibar awe na hadhi kamili kama Mkuu wa Nchi ndani na nje. Mwenyekiti wa Timu iliyopo Zanzibar, Prof. Mwesiga Baregu akamwambia hivi sasa Rais Shein yupo Vietnam, kenda kama Rais.

 Mwana-Mkataba akamjibu kenda kama Rais lakini baada ya kupata kibali cha Waziri Benard Membe na kumuuliza na Rais wa nchi gani anayehitaji kibali cha Waziri ili apokelewe kama Rais? Prof. Baregu akabaki kimya!

KWA KIDATO CHA SITA NA WENGINE WA FORM FOUR

 Assalam Alaykum Warahmatul lahi wabarakatu.

Baraza la mitihani NECTA limetoa taarifa na vigezo kwa wanafunzi wenye sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha sita 2013. Taarifa hizo rasmi wameshapelekewa wanafunzi na wazazi kwa upande wa Zanzibar. Miongoni mwa vigezo muhimu ili kuweza kuufanya mtihani huo ni kuwa na PASS TANO na pia kuwa na CREDIT TATU.


Hivyo jumuiya ya msamu kama mhusika katika kushauri masuala ya kielimu inapendekeza yafuatayo.

1. kwa wanafunzi wa shule za privates zikiwemo za KIDINI, kama Ubungo   Islamic High School, Ridhwaa Seminary na nyingine. Kama mwanafunzi aliingia kutokana na kuwa na D mbili au moja basi fanya haraka kuweza kujua kama atafanya mtihani huo au hatofanya.

2. Changamoto kwa wanafunzi ambao wapo KIDATO CHA NNE huu ni wakati wa kujipanga vizuri kwani wengi wanaoumia ni sisi waislam. Hii ni kutokana na kuwa katika baraza ni rahisi kuzikandamiza zaidi shule za kiislam kuliko za makafiri kutokana na kuwa wao wamejazana ndani ya baraza.

3. Mwisho tuondoe imani kuwa haiwezekani kupata katika mitihani, kwa mujibu wa wataalam wa masuala ya saikolojia 


inaonyesha kuwa imanu ya mtu katika suala huchochea zaidi utendaji wake. Hii ikimaanisha kuwa kwa wenye imani kuwa hawawezi daimahuwa hawawezi na huvunjika moyo na hata kujaribu huwa hawataki.

Insha Allah juhudi zinafanyika kwa baadhi ya wazazi wa kizanzibari wakishirkiana na waalimu wa wanafunzi wao ili kulipinga hili suala lakini ichukuliwe kama changamoto kwa wanafunzi na wazazi katika kuwaandalia mazinginra mazuri watoto wao waweze kusoma na hatimaye kufikia malengo yao.

Monday, November 26, 2012

ISRAEL YAJARIBU MTAMBO MWINGINE WA ULINZI


Israel imesema kuwa imefanikiwa kufanyia majaribio zana zake za ulinzi zinazokusudiwa kuzuia makobora yalio umbali wa kilomita 300.
Maafisa wa dola wamesema mtambo huo, kwa jina David's Sling au Manati ya Daudi, ulifanikiwa kuangusha kombora la kwanza katika jaribio lililofanyika wiki iliyopita.
Wakati utakapokamilika, mtambo huo utakuwa sehemu moja ya mfumo mkubwa wa ulinzi dhidi ya makombora ambao unashirikisha mtambo mwingine wa Iron Dome, ambao Wizara ya Ulinzi ya Israel inasema ulidungua mamia ya makombora ya kurushwa kwa roketi kutoka Gazi wakati wa mzozo wa majuma kadhaa yaliyopita.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas yalianza kutekelezwa Jumatano iliyopita baada ya siku nane za mapigano.

WAZIRI WA VITA WA ISRAEL AJIUZULU


Kushindwa jeshi la utawala wa Kizayuni katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza, kumemlazimisha Waziri wa Vita wa utawala huo atangaza kujiuzulu siasa.
Kwa mujibu wa duru za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel, Ehud Barak leo ametangaza kwamba anajiuzulu siasa na hatogombea tena uchaguzi wa Bunge wa tarehe 22 Januari.
Kujiuluzu huko kwa Waziri wa Vita wa Israel kumetangazwa katika hali ambayo katika siku kadhaa zilizopita Barack alitishia kwamba mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Gaza yatafanywa kwa muda mrefu.
Kufuatia hatua hiyo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema kwamba kujiuzulu Waziri wa Vita wa Israel kumetokana na ushindi wa muqawamah wa Palestina. Fauz Barhum msemaji wa Hamas amesema kwamba, kujiuzulu Ehud Barack Waziri wa Vita wa Israel kunaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni haukufanikisha hata lengo moja kati ya malengo yake ya kisiasa na kijeshi katika mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya Ukanda wa Gaza. Ameongeza kuwa, hatua hiyo inaonyesha kushindwa Israel na kushinda mapambano ya Palestina.

Tuesday, November 20, 2012

FADHILA ZA MWEZI WA MUHARRAM

Siku Ya 'Aashuraa Na Bid'ah Zake 

 Nasiha Za Minasaba Mbalimbali 

 AlhamduliLLaah, Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha tena katika mwaka mwengine mpya wa Kiislamu. Katika mwezi wa Muharram, kuna fadhila zake maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi mja anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho ili aweze kujichumia thawabu nyingi. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana kama Taasu'aa na 'Aashuraa. Hivyo ndugu Waislamu tusiache kufunga siku hizi mbili kwani thawabu zake ni kama ilivyotajwa katika mapokezi yafuatayo:

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم 

 Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka uliotangulia)) [Muslim] (soma maelezo chini kujua kwanini tufunge pia na tarehe 9 Muharram) Jumla ya miezi mitukufu ni minne na mwezi huu wa Muharram ndio mwezi wa kwanza unaoanza kuhesabika kama ni mwaka mpya.

 ((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَق السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ)) 
 ((Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Allaah ni miezi kumi na mbili katika ilimu ya Allaah (Mwenyewe tangu) siku Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajab, Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram) (kufanya) hivi ndiyo dini iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu (kwa kufanya maasi) katika (miezi) hiyo)) [At-Tawbah 9:36] Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyotoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu):

 (السنة اثنا عشر شهرا، منها أربعة حرم: ثلاث متواليات، ذو القعدة، وذو الحجة، والمحرم، ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان)) رواه البخاري، ومسلم

 ((Mwaka una miezi kumi na mbili, minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab ambao uko baina ya (mwezi wa) Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Ni neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutujuaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au masiku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Kuhesabika Kwa Mwaka Mpya Wa Hijriyah Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya kuhama (Hijrah) kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba kutoka Makkah kuhamia Madiynah. 

Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji ambao wataanza kutumia Sharia'h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana kama Muharram. Na pia inasemekana kuwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipata barua kutoka kwa mabalozi wake wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislam, na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe.

 Akawashauri Maswahaba wenzake kuwa kuwe na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohamia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah. Na mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama A.H au H kwa kirefu yenye maana 'After Hijrah' au Hijriyah, tarehe 1 Muharram A.H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622M. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka mwezi wa Dhul-Hijjah unapomalizika na mwezi wa Muharram utakapoingia hivi karibuni Fadhila Za Mwezi Huu Khaswa Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika Aayah ya juu ni mitukufu lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine kama ilivyo katika Hadiyth zifuatazo:

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم

 Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]

 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان " رواه البخاري 

 Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisubiri kufunga siku yoyote kama siku hii ya siku ya 'Aashuraa na mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhaan" [Al-Bukhaariy] Swawm ya 'Ashuraa imependezeshwa hata kwa watoto kuifunga kama walivyokuwa wakifanya Maswahaba katika siku hiyo.

 عن الرُّبيّع بنت معوذ رضي الله عنها قالت: "أرسل رسول الله صلى الله عليه وسلم غداة عاشوراء إلى قرى الأنصار "من أصبح مفطرا فليتم بقية يومه ومن أصبح صائما فليصم" ، قالت : فكنا نصومه بعد ونصوّمه صبياننا ... رواه البخاري ومسلم 

 Kutoka kwa Ar-Rubay'i bint Mu'awwadh (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituma ujumbe Alfajiri ya siku ya 'Ashuraa katika vijiji vya Answaar "Aliyeamka akiwa amefuturu amalize siku yake (kwa kutokula) na aliyeamka amefunga afunge" Akasema (Ar-Rubay'i: 'Tulikuwa tukifunga baada yake na tukiwafungisha watoto wetu...' [Al-Bukhaariy na Muslim] Sababu Ya Kufunga Siku Ya 'Aashuraa

 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ" رواه البخاري 

 Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Aashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa Wana wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy] Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa kuongeza siku moja kabla.

 روى عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قال : "حِينَ صَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ يَوْمٌ تُعَظِّمُهُ الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((فَإِذَا كَانَ الْعَامُ الْمُقْبِلُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ صُمْنَا الْيَوْمَ التَّاسِعَ)) قَالَ فَلَمْ يَأْتِ الْعَامُ الْمُقْبِلُ حَتَّى تُوُفِّيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ". رواه مسلم

 Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alipofunga Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya 'Aashuraa na akaamrisha ifungwe wakasema: Ewe Mtume wa Allaah, hii ni siku wanayoitukuza Mayahudi na Manaswara. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ikifika mwakani In shaa Allaah tutafunga siku ya tisa pia)). Akasema (Ibn 'Abbaas) haukufika mwaka uliofuata ila alifariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Muslim] Kwa hiyo ni bora kufunga siku ya tisa na kumi Muharram, na kama mtu hakujaaliwa kufunga siku ya tisa na kumi, basi afunge siku ya kumi na kumi na moja. Na kama mtu hakujaaliwa kufunga hivyo basi afunge siku ya kumi peke yake ili asikose kupata fadhila ya siku hiyo. 

 Kwa vile siku hii ni siku Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyomnusuru Muusa ('Alayhis-Salaam) na Wana wa Israaiyli, na sisi pia tutakaofunga tuwe na tegemeo kuwa nasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatunusuru pia kutokana maadui wetu na mabaya kama Alivyotuahidi In shaa Allaah 

 ((إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ))

 ((Bila ya shaka Sisi Tunawanasuru Mitume Yetu na wale walioamini katika maisha ya dunia ya siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe)) [Ghaafir 40: 51] Juu ya kwamba fadhila ya kufunga Swawm ni ibada Aipendayo kabisa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama ilivyo katika Hadiyth mbali mbali, vilevile funga hii itatusafisha na madhambi ya mwaka mzima,

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم 

 Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka wa nyuma)) [Muslim] Ndugu Waislam, hii ni fursa kubwa ya kujisafisha na dhambi na kuzidisha taqwa (ucha Mungu) ili kujibebea zawadi nyingi twende nazo Akhera kwa vile hatujui amali njema zipi zitakazokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na hatujijui kama tutakuwa na umri wa kuchuma zaidi. Bid'ah Katika Siku Ya 'Aashuraa Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa, tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu, kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu).

 Matendo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu): "Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliharamisha kama ilivyo katika Hadiyth hii sahihi:

 عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية)) البخاري .

 Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy] Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo." Ibn Rajab amesema: "Wanayoyafanya Ma-Rafidhah (Mashia) katika siku hii kuwa ni siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema, wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya huzuni kwa wasio Mitume?"

 Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.

Source: http://www.alhidaaya.com/sw/node/2475

Friday, November 16, 2012

SHULE YA SEKONDARI KIBITI YAFUNGWA KWA MGOGORO WA KIDINI

SHULE ya Sekondari Kibiti imeifungwa shule kwa madai ya mgogoro wa kidini hivyo wanafunzi kupewa saa mbili kutoonekana shuleni hapo vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kufungwa kwa shule hiyo kumefikiwa na Bodi iliyokutana na kuamua kuifunga shule hiyo kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na hisia za kidini zinazozidi kukua kwa kasi shuleni hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, amethibitisha kufungwa kwa shule hiyo.

“Sipo Rufiji lakini nimejulishwa kuhusiana na kufungwa kwa shule hiyo,”alisema kwa ufupi.

Chanzo cha kufungwa kwa shule hiyo inadaiwa kuwa ni malalamiko ya pande zote mbili baina ya wanafunzi Waislam na Wakikristo ambao wamekuwa wakilaumiana kila upande kudhalilisha dini ya mwenzake hapo shuleni.

Mmoja wa wanafunzi hao wa dini ya kiislam ambaye aliomba asitajwe jina na kudai kuwa waislam wanalalamika kuwa wakiwa wanafanya ibada katika eneo hilo wenzao wa dini ya kikristo huwafanyia fujo.

Alisema kuwa sababu nyingine ni kwamba wanafunzi wenzao siku moja walikwenda kutafuta nyama ya nguruwe na kuja kuitumia katika vyombo vinavyotumika shuleni hapo.

Kwa upande wa wanafunzi wa kikristo wao wanasema kuwa wanafunzi wenzao walichana chana Biblia na kuchoma ofisi yao ya kidini iliyopo hapo shuleni .

Alisema kuwa bodi ya shule imelazimika kuifunga shule hiyo kwa muda usiojulikana ili kuepuka vurugu kutokea shuleni hapo ili wapate muda wa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.

Mmoja wa wanafunzi hao alisema kuwa wanafunzi hao walilalamikia suala hilo kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na ndipo kukawa na mgomo wa hapa na pale wakiutuhumu uongozi wa shule hiyo kwa kushindwa kuthibiti malalamiko hayo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Mkuu wa shule hiyo, Leslaus Kihongosi alithibitisha kufungwa kwa shule hiyo lakini akasema kuwa hawezi kuwa msemaji wa suala hilo kwa kuwa sio mmiliki wa shule hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji anayedaiwa kuwa mmiliki wa shule hiyo Nasoro Mwingira alipoulizwa kuhusiana na kufungwa kwa shule hiyo alisema kuwa amepata taarifa za tukio hilo.

“Nasema kwa sasa siwezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa naelekea kwenye tukio nipo njiani,”alisema.

Diwani wa kata ya Mtawanya iliyopo shule hiyo ya kitaifa, Rashidi Mkinga alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa analisikia mitaani na hakushirikishwa katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo na yeye hawezi kusema lolote.

Haijafahamika mgogoro wa kidini baina ya wanafunzi wa dini mbili hizo umeanza lini kutokana na wahusika kukwepa kulizungumzia suala hilo huku wakitupiana mpira.

Source: Mwananchi

Tuesday, November 13, 2012

KONGAMANO LA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA KIISLAM 1434

Msamu kwa ushirikiano mkubwa na Shura ya Maimam Tanzania tunapenda kutoa taarifa juu ya KONGAMANO la kuukaribisha mwaka mpya wa kiislam 1434 tarehe 16/11/2012.

Kongamano linategemewa kuanza mara tu baada ya Swala ya Ijumaa katika msikiti wa MTAMBANI. 


Miongoni mwa agenda:
     1.kufanya Tathmini na mwaa 1433
     2.Kutolewa kwa Taarifa za kesi za waislam na sheikh Ponda.

-Masheikh mbalimbali watatoa Mada kuhusu  Dhulma wanazofanyiwa waislam nchini Tanzania kwa ujumla.

-Wanafikiwa watatajwa hadharani

-Kila mwenye kupata taarifa hii basi na amfikishie mwenziwe

-Insha allah kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko na mola atusaidie katika hili AAAMIN.


                             KAMATI YA MAANDALIZI - SHURA YA MAIMAM