Thursday, February 28, 2013

NJAMA ZA MAREKANI KUVIBAKIZA VIKOSI VYA UFARANSA NCHINI MALI

Uingiliaji kijeshi wa Ufaransa nchini Mali umepelekea serikali ya Paris kukabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile ya kifedha, kilojistiki na pia kudhamini askari jeshi kwa ajili ya kikosi maalumu cha kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali. Viongozi wa Ufaransa wanasema kuwa, uingiliaji huo umewagharimu mamilioni ya yuro. Licha ya yote hayo kupelekea viongozi wa Paris waanze kuratibu mipango ya kuondoa askari wao nchini Mali lakini Marekani inapinga suala hilo. Kwa kuzingatia kwamba imepangwa kuwa askari wa Ufaransa waanze kuondoka nchini Mali mwezi Machi, maseneta kadhaa wa Marekani waliotembelea Mali hivi karibuni, kwa kutoa kisingizo kuwa bado hali ya uthabiti ya nchi hiyo haijaimarika wamesisitiza kuendelea kuwepo askari wa Ufaransa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, kurejea nyuma wapinzani wa serikali ya mpito ya Mali na kutimuliwa katika miji ya kaskazini mwa nchi hiyo kumeandaa mazingira ya kuondoka taratibu wanajeshi wa Ufaransa nchini humo kuanzia mwezi Machi mwaka huu.  
Kwa msingi huo, kwa kutumia kisingizio kwamba bado askari wa Afrika wanaopelekwa nchini Mali katika fremu ya Umoja wa Mataifa hawana utayarifu wa kutosha wa kuchukua nafasi ya vikosi vya Ufaransa, maseneta wa Marekani wameitaka Paris kuendelea kuwepo kijeshi nchini humo hata baada ya mwezi Machi. Seneta Christopher Coons wa chama cha Democrats cha Marekani amedai kwamba, kuimarishwa uthabiti nchini Mali kunahitajia kuwepo kwa muda mrefu askari wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika. Inasemekana kuwa Maseneta hao katika safari yao hiyo walikutana na kuzungumza na makamanda wa kijeshi wa Mali mjini Bamako. Tarahe 11 Januari Ufaransa ilianza operesheni zake za kijeshi dhidi ya waasi wa kaskazini mwa Mali, na imekuwa ikiungwa mkono kilojistiki na Marekani. Mwezi Januari Marekani ilisisitiza kuwa, msaada wa Washington kwa Ufaransa ungekuwa wa kiushauri na kilojistiki tu na kwamba Marekani haina nia ya kupeleka askari wake nchini Mali. Hivi sasa kuna askari 4,000 wa Ufaransa huko Mali na imepangwa kuwa askari kadhaa kutoka nchi nyingine za Ulaya pia watapelekewa nchini humo kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali, ambapo kundi la kwanza la askari hao tayari limewasili mjini Bamako. Umoja wa Ulaya unakusudia kuisaidia Mali yuro milioni 270 ili kufanikisha mipango yake hiyo. Hata hivyo imepangwa kuwa, baada ya kupelekewa nchini Mali askari wote wa kikosi cha nchi wanachama wa Jumuiya ya ECOWAS, askari wa Ufaransa wataanza kuandoka nchini humo. Mashambulizi ya kijeshi ya Paris nchini Mali mbali na kukosolewa na shakshia wa kisiasa wa mirengo ya kulia na kushoto ya Ufaransa pia yamekosolewa na nchi nyingi duniani. Hata hivyo Wafaransa wanadai kwamba, lengo lao la kuingilia kijeshi nchini Mali ni kuimarisha amani na usalama wa nchi hiyo na kuangamiza makundi yenye silaha ya wapinzani. Lakini wataalamu wa mambo wanasema kuwa, umuhimu wa nchi hiyo ya Kiafrika kwa Ufaransa unatokana na maliasili iliyo nayo kama utajiri wa urani, ambayo ina nafasi muhimu katika kudhamini nishati inayohitajika kwenye taasisi za nyuklia za Ufaransa. Vilevile Umoja wa Ulaya umepasisha msaada wa fedha na kupelekwa askari nchini Mali ukiwa na malengo ya kiuchumi na kiusalama kama ya Ufaransa lakini yanayotekelezwa kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi.  

POLISI WAZIDI KUWAKAMATA VIONGOZI WA KIISLAM TANZANIA

POLISI mkoani Mwanza wanamshikilia Imamu wa Msikiti wa Ijumaa, huku likitangaza kuwasaka masheikh wawili wengine pamoja na Askofu (majina yote yanahifadhiwa) kwa kuhusika na uchochezi wa kidini. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alisema Imamu huyo wa msikiti alitiwa mbaroni kwa madai ya kubainika kwamba wanahusika na usambazaji wa CD za uchochezi ambazo zimekuwa zikihamasisha vurugu pamoja na mauaji ya kidini ikiwa ni pamoja na suala la kuchinja.
Kwa upande wake Askofu Mpemba wa Kanisa la Tanzania Field Evangelist yeye anasakwa kutokana na kutoa mkanda wa video (DVD) yenye jina la ‘Inuka Chinja Ule’ wakati mashehe wawili wanasakwa kwa kuhusika na uandaaji wa mikanda ya video mitatu (DVD) zenye majina ya ‘Unafiki katika Sensa, Kadhia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Uadui wa Makafiri’.
Wakati huohuo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Morogoro, limesema huenda likajitenga na Bakwata Taifa kufuatia hatua ya Sheikh Mkuu, Mufti Issa Shaaban bin Simba kumvua madaraka Sheikh wa Mkoa wa Morogoro, Yahya Semwali bila kufuata utaratibu.

ZIARA YA RAIS WA PAKISTAN IRAN YAKAMILIKA

Kongozi wa kiroho wa wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amemtaka rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, kuendelea na mradi uliocheleweshwa wa mabomba ya gesi wa dola bilioni 7.5 licha ya upinzani kutoka kwa Marekani. 
Khamenei amesema mradi huo wa mabomba ya gesi kati ya Iran na Pakistan ni mfano mzuri wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, licha ya hofu zilizopo. Zardari pia alikutana na rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ambaye alinukuliwa akisema kwamba wataendelea kuimarisha uhusiano baina yao. Mradi huo wa gesi, umekumbwa na changamoto za mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ufadhili kwa upande wa Pakistan, na upinzani mkali kutoka kwa Marekani, ambayo imeiwekea Iran vikwazo kutokana na shughuli zake za urutubishaji wa madini ya Uranium.

UN KUIONDOLEA VIKWAZO VYA SILAHA SOMALI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajitayarisha kuiondolea Somalia vikwazo vya silaha ambavyo vimekuwa vikitekelezwa kwa miongo miwili sasa. Duru za kidiplomasia zinasema uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa unalenga kuisaidia serikali ya Somalia iweze kukabiliana na waasi hasa wanamgambo wa Al Shabaab ambao bado wanaendelea kutekeleza mashambulizi nchini humo.
Imearifiwa kuwa katika kikao chake cha wiki ijayo, Baraza la Usalama litaidhinisha kuongezea muda wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika Somalia AMISOM pamoja na kuiondolea Somalia vikwazo vya silaha. Baraza la Usalama liliiwekea Somalia vikwazo vya silaha mwaka 1992 wakati wababe wa kivita walipoanza kuwania madaraka baada ya kuangushwa utawala wa Mohammad Siad Barre. Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia aliyechaguliwa mwaka jana amekuwa akitembelea nchi za Magharibi akitaka vikwazo vya silaha dhidi ya nchi yake viondolewe.

WAMAGHARIBI WAPANDIKIZA CHUKI ZA KIDINI SUDAN

Chama tawala nchini Sudan kimeonya kuhusu njama za nchi za Magharibi za kutaka kuzusha vita vya kidini na kikabila nchini humo. Qutbi al Mahdi mmoja wa viongozi wa chama tawala cha Kongresi ya Kitaifa ya Sudan amesema nchi za Magharibi zinataka kuwalazimisha watu wa Sudan wawe Wakristo sambamba na kuibua hitilafu za kikabila nchini humo lengo likuwa ni kuipokonya nchi hiyo utambulisho wake asili.
Al Mahdi amenukuliwa na tovuti ya Muhit akisema kuwa, utawala wa Kizayuni ukishirikiana na wakuu wa nchi za Magharibi wana lengo la kuhakikisha kuwa Sudan inageuka na kuwa nchi kibaraka. Amesema kutokana na kupenya majasusi wengi wa kigeni nchini humo sasa kuna haja ya Sudan kubadilisha mikakati yake ili iweze kukabiliana na tishio lililojitokeza. Al Mahdi ameongeza kuwa nchi za Magharibi zinataka kuidhoofisha Sudan ili kuzuia Uislamu kuenea zaidi barani Afrika. Ikumbukwe kuwa eneo la Sudan Kusini lilijitenga na Sudan mwaka 2011 kufuatia uchochezi wa nchi za Magharibi hasa Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Sudan vile vile inaituhumu Israel kuwa inahusika na kuchochea mapigano ya kikabila katika jimbo la Darfur Magharibi mwa nchi hiyo.

MAREKANI KUONGEZA MISAADA KWA WASYRIA

Msemaji wa White House Jay Carney amesema kuwa, Marekani itaongeza misaada kwa waasi wanaopigana na serikali ya Syria eti kwa lengo la kuharakisha mabadiliko ya kisiasa katika nchi hiyo.
Matamshi hayo yametolewa huku gazeti la Washington Post likiandika kuwa, White House inaazimia kuwatumia waasi wa Syria silaha, magari ya kijeshi na ikiwezekana pia kuwapatia mafunzo ya kijeshi. Marekani imekuwa ikiwafadhili waasi wa Syria kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo.
Katika upande mwingine mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amewataka wanaojiita 'Marafiki wa Syria' kuwashauri wapinzani kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa na serikali bila masharti. Bashar al Jaafar amesema, iwapo kweli watu hao ni marafiki wa kweli wa taifa la Syria na wanajali wananchi wa nchi hiyo wanapaswa kuwashauri wapinzani kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano na kutoharibu zaidi miundombinu ya nchi hiyo.

ALIYEMUUA KIONGOZI WA TUNISIA AJULIKANA

Waziri Mkuu mpya wa Tunisia, Ali Larayedh amesema kuwa, aliyemuua kiongozi wa upinzani Shokri Belaid majuma mawili yaliyopita amejulikana na kwamba vyombo vya usalama vinaendelea kumtafuta. Larayedh amesema uchunguzi umebaini kwamba Mawahabi wenye misimamo ya kufurutu ada ndio waliotekeleza mauaji hayo lakini akakanusha madai kwamba serikali ilihusika na mauaji hayo. Belaid ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akitoka nyumbani kwake. Kuhusu suala la kuunda serikali mpya, Waziri Mkuu huyo amesema anaendelea kujadiliana na vyama pamoja na makundi mbalimbali ili serikali itakayoundwa iwe na sura ya kitaifa. Kiongozi huyo ambaye hapo awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wiki iliyopita kufuatia kujiuzulu mtangulizi wake, Hamad Jebali.

WANAMGAMBO WAVAMIA OFISI YA WAZIRI MKUU WA LIBYA

Makumi ya wanamgambo wa Libya wanaohusika na kulinda amani katika baadhi ya mipaka ya nchi hiyo, wameshambulia ofisi ya Waziri Mkuu Ali Zeidan, wakilalamikia hali duni ya mishahara yao. Tukio hilo lilitokea jana Jumatatu wakati Waziri Mkuu akiwa hayupo ofisini. Habari zinasema kuwa, Waziri Mkuu wa Libya alikuwa amekwenda kushiriki kikao cha Baraza la Haki za Binaadamu cha Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, ambapo watu wanaokadiriwa 30 walishambilia ofisi yake mjini Tripoli. Awali wanamgambo hao walikuwa wamekwenda ofisini hapo  kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Ali Zeidan lakini walipopata habari kuwa hayupo walikasirika na kuanza kufanya fujo ofisini kwake. Wanamgambo hao wa vikosi vya ulinzi wa usalama katika mipaka ya Libya wako chini ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo.  Mipaka ya Libya inalindwa na wanamgambo, kutokana na nchi hiyo kudhoofika kijeshi na kipolisi.

JESHI LA WANAMAJI WA IRAN KUZIMA NJAMA ZA MAADUI


Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran kwa kutumia uwezo wa jeshi lake la wanamaji litazima njama zote za maadui katika eneo hili. Admeli Habibullah Sayyari ameyasema hayo Jumanne  mjini Tehran katika Kongamano la Tiba na Shughuli za Uokozi Baharini na kuongeza kuwa, Jeshi la Wanamaji la Iran lina uwezo wa kutekeleza oparesheni katika maji ya kieneo na kimataifa. Admeli Sayyari ameendelea kusema kuwa, leo Jeshi la Wanamaji la Iran linatumia teknolojia ya kisasa kabisa katika shuguhuli zake. Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran amesema, mbali na kuwa na suhula za kisasa pia kunahitajika wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu na kwa bahati nzuri Iran imefanikiwa sana katika uwanja huo. Admeli Sayyari amesema msafara wa manowari za Jeshi la Wanamaji la Iran kwa mara ya kwanza umepita katika Lango Bahari la Malacca ambalo ni moja kati ya maeneo muhimu ya zaidi ya baharini duniani. Ameongeza kuwa msafara huo wa meli za kivita za Iran leo umeingia katika Bahari ya Pasifiki na katika siku chache zijazo meli hizo zitatia nanga nchini Uchina kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya Beijing na Tehran.

ISRAEL YAZIDI KUSAKAMWA KUTOKANA NA MATESO YAKE KWA WAPALESTINA

Kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala huo usio na utu wala chembe ya ubinaadamu kumewafanya mateka madhulumu wa Kipalestina wakabiliwe na kifo cha polepole. Lakini walimwengu ni wanadamu, jinai hizo za Wazayuni zimewafanya walimwengu kutoka kila kona ya dunia kulaani vikali jinai hizo. Malalamiko ya walimwengu yamechukua wigo mpana zaidi baada ya kufa shahidi mateka wa Kipalestina Arafat Jaradat. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa tena huru kuhusiana na kifo cha mateka huyo wa Kipalestina. Kuhusiana na suala hilo, Robert Serry, Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Mashariki ya Kati ametaka kuundwe kamati huru ya kutafuta ukweli ambayo itakuwa na jukumu la kuchunguza namna Mpalestina huyo alivyofariki dunia. Amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 
Hii ni katika hali ambayo, Wasil Abu Yusuf, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO amesema kuwa, Wapalestina watawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ili kuzuia ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina unaofanyika kila uchao katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Kwa upande wake, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetoa taarifa na kulaani vikali kuuawa Arafat Jaradat, mateka wa Kipalestina. Profesa Ekmeleddin IhsanoÄŸlu, Katibu Mkuu wa OIC amelaani kitendo cha Wazayuni cha kumuua shahidi Jaradat na kusema kuwa, kitendo hicho ni jinai ya wazi na ukiukaji wa dhahiri kabisa wa haki za kimataifa. Amesema, kifo cha Jadarat kimefichua tena jinai na siasa za kibaguzi za Israel. Katibu Mkuu wa OIC amezitaka asasi za kimataifa kuwa amilifu zaidi katika hili na kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili uachane na siasa zake za muamala mbaya na mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina na uwaachilie huru mara moja mateka hao wa Kipalestina unaowashikilia katika magereza yake ya kutisha. Kadhalika wananchi wa Palestina walijitokeza kwa wingi katika shughuli ya maziko ya Arafat Jaradat na kusisitiza kwamba, damu ya shahidi hiyo haitapotea bure. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, kutokana na kutanda wingu zito la malamiko na upinzani wa Wapalestina dhidi ya Wazayuni, ni ishara ya kuingia Intifadha ya wananchi wa Palestina katika marhala mpya. Viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu na Kiislamu pia wametoa taarifa kwa nyakati tofauti wakilaani siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu imetoa taarifa maalumu ambapo sambamba na kulaani jinai hiyo ya Israel imesisitiza kwamba, kitendo hicho cha Israel ni ukiukaji wa wazi kabisa wa haki za binadamu. Iran imezitaka asasi za kimataifa hususan mashirika ya kutetea haki za binadamu ulimwenguni kuchukua hatua za maana na za kivitendo ili kuzuia kukaririwa maafa ya kibinadamu huko Palestina ambayo ni kinyume kabisa na mikataba ya kimataifa. Hapana shaka kwamba, kimya cha asasi za kieneo na kimataifa kwa jinai za Israel kwa upande mmoja, na uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa Tel Aviv kwa upande wa pili, ni mambo ambayo yamekuwa yakiupa kiburi utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuendeleza jinai zake hususan dhidi ya mateka wasio na ulinzi wa Kipalestina.

IRAN YAIKOSOA VIKALI FILAMU YA ARGO


Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran amekosoa vikali tuzo ya Oscar kutunukiwa filamu ya ARGO ambayo imetayarishwa huko Hollywood dhidi ya taifa la Iran. Dakta Muhammad Husseini amesema kuwa, Wamarekani wamefanya propaganda kubwa ndani ya filamu hiyo dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba watengeneza filamu wa Kiirani walioshiriki katika filamu hiyo pia wana kesi ya kujibu.
Dakta Husseini amesema kuwa, filamu ya Argo ambayo imetangazwa kuwa filamu bora kabisa duniani mwaka 2013 na kupewa tuzo ya Oscar, ni dhaifu mno katika upande wa kiusanii. Amesema hatua ya kupewa tuzo ya Oscar filamu ya Argo iliyo dhidi ya Iran inaonyesha kuwa, Hollywood imeshindwa kwenye siasa za tasnia ya filamu.

KADINALI UINGEREZA AKUMBWA NA KASHFA YA KUNAJISI


Kiongozi wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki nchini Uingereza ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo. Taarifa kutoka Vatican zinasema kuwa, Papa Benedict wa 16 Kiongozi wa Wakatoliki Duniani amekubali takwa la kujiuzulu Kadinali Keith O'Brien, Kiongozi wa Kanisa Katoliki la Uingereza. Kadinali O'Brien anasakamwa  kwa kushindwa kuwachukulia hatua Mapadri waliokuwa chini yake ambao walikabiliwa na kashfa za kuwanajisi wafuasi wao. Kwa kujiuzulu Kadinali O'Brien Uingereza na Scotland hazitapata fursa ya kushiriki zoezi la kumchagua Papa mpya. Papa Benedict wa 16 atajiengua rasmi kutoka kwenye wadhifa huo tarehe 28 Februari mwaka huu.
Kadinali O'Brien alikuwa rafiki mkubwa wa mwandishi wa BBC aliyekuwa mashuhuri kwa kuwanajisi watoto wadogo kwa miaka mingi Jimmy Savile na inasemekana kuwa alimtukuza na mkumsifu mhalifu huyo baada ya kufariki dunia.

SAFARI YA UJUMBE WA IRAN HUKO KAZAKHSTAN


Duru mpya ya mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika leo Jumanne huko Almaty, Kazakhstan. Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Saeed Jalili amewasili Almaty mji mkuu wa Kazakhstan akiongoza ujumbe wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika duru hiyo ya mazungumzo. Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Marekani, Russia, Uchina, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani mwaka uliopita zilifanya duru tatu za mazungumzo. Duru ya mwisho ya mazungumzo hayo iliyohudhuriwa na Saeed Jalili, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na Bi Catherine Ashton Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ilifanyika mwezi Juni mwaka jana huko Moscow mji mkuu wa Russia.
Wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani bunge wametoa taarifa wakiitaka timu ya mazungumzo ya Iran kutetea kwa nguvu zote haki za taifa la Iran katika fremu ya makubaliano ya kuzuia kuzalisha, kutumia na kusambaza silaha za nyuklia  NPT. Taarifa ya wabunge wa Iran imeashiria pia kushiriki Russia na Uchina katika mazungumzo hayo kama nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza Iran inataraji kuwa nchi hizo hazitafuata sera za kupenda makuu na matakwa yasiyo na kimantiki ya Marekani bali zitalinda mkataba wa NPT khususan kipengee cha 4 kinachozipa nchi wanachama haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia.
Saeed Jalili Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kabla ya mazungumzo ya Kazakhstan kwamba, wananchi wa Iran wanataka kulindwa haki yao ikiwemo haki ya nyuklia na kwamba Iran kama nchi mwanachama hai na inayofuata sheria, inatekeleza kikamilifu sheria zote katika fremu ya mkataba wa NPT. Matamshi hayo yaliyotolewa kabla ya kuanza mazungumzo ya Almaty yanayonyesha kuwa Iran inaingia katika mazungumzo na kundi la 5+1 katika fremu ya mantiki, inayoeleweka na ya kujilinda huku ikitaraji kuwa muamala wa kundi la 5+1 pia utaegemea katika stratejia iliyo ya wazi.
Inaonekana kuwa duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 kama kawaida inaanza katika anga ngumu na iliyojaa mashinikizo ya kisiasa. Hii ni katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) pia umetoa ripoti yake kabla ya kuanza mazungumzo ya leo ukiashiria kufungwa mashinepewa za kisasa katika kiwanda cha Natanz hapa nchini ikiwa ni katika jitihada za wakala huo za kuzusha shaka na wasiwasi kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran. Hata hivyo aina hiyo ya vita vya kisaikolojia vinavyofanyika sasa  kabla ya kuanza mazungumzo ya leo huko Almaty havina jambo jipya. Moja ya mambo yaliyopelekea kusimamishwa mazungumzo kati ya Iran na kundi la 5+1 kwa karibu miezi tisa ulikuwa  ni muamala  kama huo wa wakala wa IAEA na misimamo yake isiyo ya kimantiki na sera za nchi za Magharibi  mbele ya haki ya kinyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baadhi ya duru za kisiasa na vyombo vya habari pia vimekuwa vikiukosoa muamala huo wa nchi za Magharibi kuhusiana na Iran.
Kuhusiana na jambo hilo, baadhi ya wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wanasema kwamba, Marekani itawasilisha pendekezo jipya katika mazungumzo ya Almaty ili kuhitimisha mkwamo uliosababishwa na  misimamo ya Magharibi katika kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa vyovyote vile, msimamo wa Iran kuhusu mtazamo huo uko wazi na chanya na Tehran inazitaka nchi za Magharibi kutambua rasmi haki yake ya nyuklia ikiwemo urutubishaji wa urani katika fremu ya mkataba wa NPT na si zaidi ya hapo. Iran kwa upande wake itaendelea kuheshimu kikamilifu sheria zote kwa mujibu wa mkataba wa NPT.

IRAN YAZINDUA MAKOMBORA YA KUTUNGULIA NDEGE


Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran SEPAH limefanyia majaribio bunduki mpya ya kutungulia ndege ya kubebwa begani na ambayo ina uwezo mkubwa wa kutungua vyombo vya angani hasa helikopta. Hilo limefanyika katika mazoezi ya kijeshi ya jeshi hilo yanayoendelea hivi sasa hapa nchini kwa mfululizo. Msemaji wa luteka hiyo yenye jina la Payambare A'zam 8, Brigedia Jenerali Hamid Sarkheili amesema kuwa, silaha hiyo mpya imebuniwa, kutengenezwa na kuendelezwa na jeshi lenyewe la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran. 
Ameongeza kuwa, silaha hiyo ina uwezo wa kutungua helikopta iliyoko umbali wa mita 1,400 angani. Jeshi la nchi kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH jana Jumamosi lilianza kufanya mazoezi hayo ya kijeshi katika mkoa wa Kerman wa kusini mashariki mwa Iran kwa lengo la kujiimarisha kijeshi na kufanyia majaribio silaha mpya. Jana pia na wakati mazoezi hayo yakiendelea, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran kwa mara nyingine lililazimisha kutua chini ndege isiyo na rubani (drone) ya nchi moja ya adui baada ya kuingia kwa siri katika anga ya Iran. Jenerali Sarkheili pia amesisitiza kuwa, kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa vita vya kielektroniki, Iran inaweza kuvuruga kwa urahisi mfumo wa makombora ya maadui.

Sunday, February 24, 2013

RAISI WA MISRI ABADILI TAREHE YA UCHAGUZI BAADA YA KULALAMIKIWA

Rais Mohammed Mursi  wa Misri amebadilisha ratiba ya uchaguzi wa bunge kufuatia malalamiko ya jamii ya wachache ya wakristo.Kwa mujibu wa televisheni ya taifa, uchaguzi huo uliopangwa kufanyika kwa awamu nne,utaanza hivi sasa April 22 na 23.Hapo awali uchaguzi huo ulipangwa kuanza April 27/28 na kwa namna hiyo ungefanyika wakati wa sherehe za pasaka za jamii ya wakristo wa madhehebu ya Koptik.Jamii hiyo inafikia asili mia 10 ya wananchi jumla wa Misri.Kwa jumla zoezi la uchaguzi litafanyika kwa awamu tofauti kote nchini humo na kuendelea hadi mwezi June mwaka huu.Kubadilishwa tarehe ya kupiga kura hakutaubadilisha wito wa upande wa upinzani kuususia uchaguzi huo.Upande wa upinzani unataka uchaguzi usiitishwe na badala yake iundwe serikali ya mpito itakayozijumuisha pande zote za kisiasa za nchi hiyo.Fikra hiyo inapingwa na chama cha Udugu wa kiislam cha rais Mohammed Mursi.Bunge la awali la Misri lilivunjwa mwezi June mwaka jana,miezi mitano tu baada ya kikao chake cha kwanza,baada ya korti ya katiba kusema uchaguzi haukuambatana na katiba.

WAFUNGWA WA KIPALESTINA WAGOMEA CHAKULA ISRAEL


Wapalastina kadiri 3000 wanaoshikiliwa katika jela za Israel wameanzisha mgomo wa siku moja kususia chakula hii leo waakilalamika dhidi ya kufariki dunia mwenzao aliyekuwa korokoroni-kisa hicho kimezusha mapigano kati ya vikosi vya usalama  vya Israel na waandamanaji katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.Msemaji wa shughuli za jela za Israel Sivan Weizman ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP  tunanukuu" ni chakula cha siku moja tu-"Arafat Jaradat,aliyekuwa na umri wa miaka 30 amekufa kwa ghafla jana akiwa jela,katika kile ambacho maafisa wa jela wanasema pengine kimesababishwa na kusita mipigo ya moyo.
Waandamanaji katika mji wa kusini mwa Ukingo wa magharibi-Hebron wanawavurumishia mawe wanajeshi wa Israel wanaoajibu kwa kufyetua gesi za kutoa machozi na kuvurumisha maguruneti.Hakuna  bado ripoti kuhusu majeruhi.

JESHI LA IRAN LAISHUSHA DRONE NYINGINE ILIYOKATIHS ANGA YAKE

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kwa mara nyingine limefanikiwa kuilazimisha kutua chini ndege isiyo na rubani (drone) ya nchi adui baada ya kuingia kwa siri katika anga ya Iran. Ndege hiyo ya kijasusi imenaswa  katika Mazoezi ya Kijeshi ya Mtume Mtukufu SAW 8 yaliyoanza jana Jumamosi kusini mwa nchi. Msemaji wa maneva hiyo Jenerali Hamid Sarkheili amewaambia waandishi habari kuwa,  ‘wataalamu wa kitengo cha vita vya kielektroniki katika IRGC walitambua ndege isiyokuwa na rubani iliyokuwa na lengo la kukiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu na hapo waliweza kuidhibiti na kuilazimisha kutua chini pasina kuwepo uharibifu.’ Ikumbukwe kuwa  Desemba mwaka 2011 vikosi vya ulinzi vya Iran vilkifanikiwa kuinasa ndege ya kisasa ya kijasusi ya Marekani aina ya RQ-170 iliyokuwa imeingia nchini. Aidha Desemba 4 mwaka 2012 Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitangaza kuwa lilifanikiwa kunasa ndege ya kijasusi ya Marekani aina ya ScanEagle katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Jenerali Sarkheili amesisitiza kuwa kwa kutumia uwezo huo wa vita vya kielektroniki Iran inaweza kuvuruga kwa urahisi mfumo wa makombora ya maadui. Amesema  Mazoezi ya Kijeshi ya Mtume Mtukufu SAW 8 yanalenga kuimarisha uwezo wa mbinu mpya za kivita. Jenerali Sarkheili amesistiza kuwa uwezo wa kijeshi wa Iran ni wa kujihami na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuvamia nchi nyingine. Mazoezi hayo yataendelea hadi Februari 25.

WAPALESTINA WATAKA KUUNDWA TUME KUCHUNGUZA MAUAJI YA MWENZAO.


Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) imetaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na kifo cha mateka wa Palestina katika jela ya Israel. Afisa wa mamlaka hiyo Issa Qaraqea amesema kwamba taarifa walizopata zinaonyesha kwamba Mpalestina huyo alifariki dunia wakati alipokuwa akihojiwa na kwamba suala hilo linaonyesha kwamba huenda alifariki dunia kutokana na kuteswa wakati wa kuhojiwa.
Mpalestina huyo Arafat Jaradat aliyekuwa na miaka 30 alifariki dunia katika jela ya Israel ya Magiddo na askari usalama wa jela hiyo wanadai kwamba, kifo chake kimetokana na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo. Kuna zaidi ya Wapalestina 4,500 wanaoshikiliwa katika jela na korokoro za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel bila kuhukumiwa huku wakikabiliwa na mateso na hali mbaya ya kibinadamu.

RAIS WA IRAN ASEMA IRAN INAMIKAKATI YA KUPAMBANA NA MAADUI

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali inatathmini kwa kina njama za kiuchumi za maadui ili kuzisambaratisha. Akizungumza jana usiku na wananchi kwa njia ya moja kwa moja katika Kanali ya Kwanza ya Televhisheni ya Kitaifa ya Iran, Rais Ahmadinejad amesema baada ya kuchunguza kwa kina njama za maadui serikali imetayarisha bajeti yenye ubunifu mkubwa. Amesema kwa mujibu wa bajeti ya mwaka mpya wa Kiirani wa 1392, unaoanza Machi 21, uchumi wa Iran utarejea katika hali ya kawaida na hivyo kufelisha njama za maadui. Amesema bajeti mpya ya Iran imepunguza utegemezi kwa pato la mafuta. Akiashiria vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran, rais Ahmadinejad ametoa wito kwa watu wote Iran kushirikiana ili nchi iweze kupita vizuri katika kipindi hiki.  Amesema Iran ni nchi yenye uwezo mkubwa na kuongeza kuwa pamoja na kuwa maadui na hasa serikali ya Marekani inatumia uwezo wake wote kuishinikiza Iran lakini haitafanikiwa katika malengo yake hayo. Amesema Wamarekani walidhani kwa pigo la kiuchumi kwa Iran, nchi hii ingeyumba lakini, Alhamdulillah, Iran imesimama imara.

vituo vipya vya nyuklia kujengwa iran


Shirika la Atomiki la Iran limetangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imeainisha maeneo 16 ya kujengwa vituo vya nishati ya nyuklia. Katika taarifa, Shirika la Atomiki la Iran limesema vituo hivyo vitajengwa katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Kaspi, Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.
Taarifa hiyo imesema miradi hiyo ni katika mpango wa muda mrefu wa Iran wa kuimarisha uwezo wake wa kuzalisha umeme wa nyuklia kwa mujibu wa kanuni za kimataifa. Wakati huo huo Shirika la Atomiki la Iran limesema migodi mipya ya madini ya urani imegunduliwa nchini na hivyo kuimarisha uwezo wa Iran kujitegemea kikamilifu katika uzalishaji nishati ya nyuklia. Kwingineko Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Fereydoun Abbasi amesema kizazi kipya cha mashinepewa au centrifuge 180 zimeanza kutumika katika kituo cha nyuklia cha Natanz. Akizungumza Jumamosi amesema mashinepewa hizo aina ya IR2M  zitaendelea kuongezwa katika kituo hicho ili kuwezesha urutubishaji wa urani hadi kiwango cha asilimia tano. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza mara kwa mara kuwa shughuli zake za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani chini ya usimamizi wa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Saturday, February 23, 2013

GAZETI ANNUUR FEB 22 - 28

ANNUUR 1059 by annurtanzania

ANNAN ATUMA SALAM ZA UCHAGUZI WA AMANI KENYA


Kofi Annan aliongoza shughuli za kupatanisha baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi miaka mitano iliyopita ambapo watu zaidi ya elfu-moja walikufa. Katika barua iliyokusudiwa Wakenya wote, Kofi Annan alisema uchaguzi lazima uwe amani, huru na wa haki. Amesema matukio ya ghasia ya karibuni na mvutano unaozidi kabla ya uchaguzi yanatia wasi-wasi mkubwa. Siku kumi kabla ya uchaguzi Bwana Annan ametoa wito kwa viongozi wa siasa, dini na jamii walaani hatua au matamshi yanayokusudia kuwatenga watu na kuwachochea. Ametaka mizozo yoyote baada ya uchaguzi ipelekwa mahakamani. Juma hili hakimu mkuu wa Kenya, Willy Mutunga, alisema mahakimu wanakabili vitisho na bughudha. Bwana Mutunga alisema majaji watano wameshambuliwa hivi kabla ya uchaguzi. Hakimu Mutunga amesifiwa kwa jumla kwa kujaribu kusafisha mahakama ambayo yamehusishwa na rushwa. Aliwalaumu wanasiasa kwamba wanahusika na vitisho hivyo na alisema majaji hawatakubali kutishwa na kundi la wale wanaotaka kuirejesha nchi nyuma.

OIC KUANZISHA TELEVISION YAKE


Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ina azma ya kutekeleza baadhi ya malengo likiwemo suala la kupambana na chuki na uadui dhidi ya Uislamu, kwa kuanzisha kanali yake ya televisheni. Taarifa zinasema kuwa, leo Jumamosi kinafanyika kikao cha wataalamu wa nchi wanachama wa OIC ambacho kitajadili kwa kina mikakati ya kuanzisha kanali ya televisheni itakayorusha matangazo yake kwa lugha za Kiarabu, Kiingereza na Kifaransa. Esam al Shanti Mkurugenzi wa Idara ya Habari wa OIC amesema kuwa, lengo kuu la kuanzishwa kwa kanali hiyo ya televisheni ni kuonyesha sura halisi ya Kiislamu, kukabiliana na vitendo vya kuufanya Uislamu uogopwe na hasa katika nchi za Magharibi na hali kadhalika kukurubisha staarabu za Mashariki na Magharibi na Kaskazini na Kusini. Hakuna shaka kuwa, vyombo vya kupasha habari vina nafasi kubwa ya kuathiri matukio ya kimataifa na fikra za walio wengi duniani na hasa katika zama hizi za utandawazi. Hali kadhalika, vyombo vya kupasha habari licha ya kuwa na athari kubwa katika kusambaza tamaduni mbalimbali, vinahesabiwa pia kuwa wenzo wa kutoa huduma kwa madola ya Kimaghairbi. Aidha kuna baadhi ya vyombo vya habari katika ulimwengu wa Kiislamu ambavyo havijishughulishi na kukabiliana na vitendo vya kiadui dhidi ya Uislamu, bali vimekuwa bega kwa bega na vyombo vya Magharibi katika kuleta mifarakano ya kimadhehebu na kuzipaka matope baadhi ya nchi za Kiislamu. Nafasi hizo za uharibifu na utibuaji wa vyombo vya habari vya Kimagharibi na vya Kiarabu zimefichuka zaidi katika kipindi cha miaka miwili  iliyopita, ambapo ulimwengu umeshuhudia mwamko na Kiislamu na wimbi kubwa la wananchi wa nchi za Kiarabu lililokuwa dhidi ya watawala vibaraka. Kuhusu suala hilo, OIC ikiwa ni miongoni mwa jumuiya kubwa ulimwenguni, haikuwa na athari yoyote muhimu katika matukio yaliyojiri miaka miwili iliyopita na wala kuweza kutoa ushawishi wake katika kukabiliana na vyombo vya habari vya Magharibi na vile vya nchi za Kiarabu vinavyochochea  mifarakano ya Kimadhehebu. Hakuna shaka kuwa, kwa kuzingatia mazingira ya kiadui yaliyoko dhidi ya Uislamu ulimwenguni na hali kadhalika fitina za kimadhehebu zilizoko katika eneo, huu ni wakati mwafaka kwa jumuiya ya OIC kuchukua maamuzi hayo mazito na muhimu ya kuanzisha kanali ya televisheni ambayo itaweza kubadilisha anga ya kiadui iliyotanda dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Alaa kulli haal, baada ya kuanzishwa kanali hiyo ya televisheni ya OIC, suala muhimu ni kuwa,  chombo hicho hakipasi kuathiriwa  kiutendaji na watawala wa baadhi ya nchi za Kiarabu, kwani utendaji wake unapasa kuwa na maslahi kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu kwa kuondoa hitilafu zilizopo. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC iliundwa tarehe 25 Disemba mwaka 1969 na hivi sasa ina jumla ya wanachama 57.

USA YAFUNGUA KITUO CHA DRONE ZAKE NIGER


Marekani imeasisi kituo kipya cha ndege zake zisizo na rubani huko Niger kwa shabaha ya kupambana na wanagambo wa al Qaida na makundi yote yanayoliuga mkono kundi hilo barani Afrika na pia kwa lengo la kuviunga mkono vikosi vya Ufaransa katika vita vyao huko Mali. Gazeti za new York Times limeripoti kuwa Marekani imetuma huko Niger ndege zake zisizo na rubani aina ya Predator ili kuisaidia nchi hiyo katika kile ilichokitaja kuwa mapambano dhidi ya ugaidi. Ijumaa ya jana Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kuwa wanajeshi 100 wa nchi hiyo wametumwa nchini Niger ili kusaidia kukusanya taarifa za kiitelijenisia na kuwezesha usambazaji wa taarifa hizo kwa washirika wengine wa Marekani katika eneo na kwa vikosi vya Ufaransa vinavyoendesha oparesheni huko Mali. Afisa wa ulinzi wa Marekani ambaye hakutaja jina lake amesema kuwa ndege hizo za ujasusi hazijabeba silaha zozote na kwamba kazi yake ni kufanya ujasusi tu. Ndege hizo huenda zikatumika kuendeshea mashambulizi hapo baadaye iwapo itahitajika.  

Viongozi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wametangaza kuwa nchi hiyo imetuma ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kuvisaidia vikosi vya Ufaransa vilivyoko huko Mali. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imedai kuwa imeazimia kutumia vituo vya ndege zisizo na rubani katika maeneo ya pwani na jangwani huko magharibi mwa bara la Afrika kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa harakati za wapinzani wa kisiasa katika nchi za eneo hilo.
Hadi sasa Washington imetumia ndege zake hizo zisizo na rubani katika baadhi ya nchi hususan huko Pakistan Afghanistan, Yemen na Somalia. Tangu baada ya tukio la Septemba 11 huko Marekani Pentagon imekuwa ikitumia ndege hizo kama silaha ya kufunika mashambulizi ya anga yanayofanywa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) katika pembe mbalimbali za dunia katika kile kinachotajwa kuwa ni mapambano dhidi ya ugaidi. Hata hivyo, viongozi wa Pentagon wanasisitiza kuwa ndege zisizo na rubani zilizotumwa huko Niger hazijabeba silaha wala makombora na kwamba zitatumika tu kwa ajili ya masuala ya ujasusi na kukusanya taarifa kuhusu wapinzani wa serikali ya Mali.

MUGABE KUSHIRKI TENA UCHAGUZI UJAO


Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe ametangaza kushiriki kwa mara ya sita kwenye uchaguzi wa rais utakaofanyika miezi michache ijayo nchini humo. Rais Mugabe ameyasema hayo jana wakati wa kuadhimisha kutimia miaka 89 ya kuzaliwa kwake, kwenye sherehe ndogo iliyofanyika nchini humo. Mugabe ambaye anaiongoza nchi  hiyo kwa zaidi ya miaka 33 sasa amepanga kufanya sherehe kubwa zaidi ya kuzaliwa kwake  mwezi ujao itakayogharimu kiasi cha dola laki sita. Wakati Rais Mugabe akijiandaa kufanya  sherehe mwezi ujao, hivi karibuni Tendai Biti Waziri wa Fedha wa nchi hiyo alitangaza kuwa, kuna kiasi cha chini ya dola 300 kwenye hazina ya serikali ya nchi hiyo. Zimbabwe licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi,  inatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Rais Mugabe amesema kwenye hafla hiyo kuwa, mashinikizo ya Marekani na Uingereza yanafanyika kwa minajili ya kumuondoa yeye madarakani pamoja na chama chake cha Zanu PF.  Duru ya tano ya uchaguzi wa rais nchini humo iligubikwa na ghasia na rangaito iliyopelekea chama cha Zanu PF na kile cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.

MISRI YAKANUSHA JUU YA USHIRIKIANO WAKE NA ISRAEL

Msemaji wa Jeshi la Misri amekadhibisha habari za kuwepo mashirikiano ya kijeshi kati ya jeshi la nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kuharibu njia za chini kwa chini zilizoko katika mpaka kati ya Misri na Ukanda wa Ghaza. Ahmad Muhammad Ali amesisitiza kuwa, Misri haijafanya mazungumzo yoyote na utawala wa Israel kuhusiana na suala hilo. Amesema kuwa, jeshi la Misri lilianza kuharibu njia hizo za chini kwa chini baada ya watu wanaobeba silaha katika eneo la Rafah kuwauwa wanajeshi 16 wa Misri mwezi Agosti mwaka 2012. Msemaji wa Jeshi la Misri ameongeza kuwa, operesheni hiyo  bado inaendelea. Baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuweka mzingiro dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza tokea mwaka 2006, wananchi wa Gaza walitengeneza  mamia ya njia za chini kwa chini kwa lengo la kupitisha mahitajio yao muhimu kama vile madawa, chakula na vifaa vya ujenzi.

ARAB LEAGUE YALAANI UKANDAMIZAJI UNAOFANYWA NA ISRAEL

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League imelaani vikali siasa zisizo za kibinaadamu zinazofanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina. Akiashiria kuendelea kugoma kula mateka wa Kipalestina Samir al-Issawi anayeshikiliwa katika jela za kutisha za utawala huo, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) Muhammad Sabih amesema kuwa, viongozi wa Israel hawaitilii umuhimu wowote hali ya mateka huyo. Ameelezea hukumu ya hivi karibuni ya utawala katili wa Kizayuni, iliyosisitiza juu ya kucheleweshwa ufatiliaji wa kesi ya al-Isawi na kuitaja hukumu hiyo kuwa ya kifo dhidi ya mateka huyo wa Kipalestina ambaye alianza kugoma kula chakula tangu siku 215 zilizopita.
Al-Issawi alichukua uamuzi huo ili kulalamikia siasa za ukandamizaji zinazofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni. Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia amesisitizia udharura wa kufanyika juhudi za dhati zitakazosaidia kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina hususan al-Isawi na kuongeza kuwa jumuiya hiyo itawasilisha kadhia hiyo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu Human Right Watch na taasisi nyingine za kimataifa ili kuushinikiza utawala wa Kizayuni uheshimu haki za mateka hao.

MAREKANI NA NJAMA ZA KUIMALIZA HIZBULLAH

Mtandao wa habari wa al-Manar umeandika kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, zinafanya njama za kuimaliza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah. Al-Manar imeongeza kuwa, Marekani kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu, zimeshadidisha njama zao za kuizingira harakati hiyo. Mtandao huo umeongeza kuwa, Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati zinafanya mawasiliano ya siri baina yao kwa ajili ya kuzuia uwezo wa Hizbullah kupitia mgogoro wa Syria. Pia umeandika, mawasiliano  hayo yanafanyika kwa kiwango cha hali ya juu na kwa siri, na  yanasimamiwa na Washington. Tangu utawala wa Kizayuni ulipopata kipigo kikali katika vita vya siku 33 kutoka kwa harakati hiyo ya Hizbulla, umekuwa ukifanya kila liwezekanalo kujaribu kuinyanganya Hizbullah silaha zake, suala ambalo limeshindikana kabisa.

SPIKA WA BUNGE LA LEBANOPN AIONYA VIKALI ISRAEL

Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri, ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kupora utajiri wa mali ya Lebanon. Nabih Berri amesema kuwa, utawala ghasibu wa Kizayuni unafanya njama za kupora utajiri wa nchi hiyo kwa kutumia vibaya tofauti zilizopo kati ya ulimwengu wa Kiarabuhivi sasa. Ameukumbusha utawala huo kuwa, haupaswi kusahau kwamba, ipo Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya nchi hiyo, ambayo itasimama kidete kutetea haki na mali za Lebanon. Onyo hilo linatolewa wakati ambapo kwa mara kadhaa viongozi wa serikali ya Beirut walikwishaionya vikali Israel kuhusiana na kuendelea kupora utajiri wa mafuta na gesi vya nchi hiyo. Mbali na hayo, viongozi wa Beirut wametaka Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala huo wa Kizayuni ili ukomeshe mara moja kupora utajiri wa Lebanon.

IRAN YALAANI MRIPUKO WA DAMASCUS


Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulio la kigaidi lililolenga makaazi ya raia na kusababisha watu 53 kuuawa na wengine 250 kujeruhiwa katika mji mkuu wa Syria, Damascus. Taarifa ya wizara hiyo imesema kuwa, wanaolitakia mema taifa la Syria wanatiwa wasiwasi na kuendelea kukosekana amani na usalama nchini humo na kutoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa badala ya kutumiwa mtutu wa bunduki. Taarifa hiyo pia imesisitiza kwamba vitendo kama hivyo vinaendelea kutekelezwa na magaidi wanaofadhiliwa na madola ya kigeni kwa lengo la kukwamisha jitihada za kutekeleza mageuzi ya kisiasa na kurejesha amani na usalama nchini Syria.
Wakati huo huo Russia imekosoa msimamo wa kindumilakuwili wa Marekani kuhusiana na Syria na kuilaumu Washington kwa kuzuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani mlipuko huo wa bomu uliotokea mjini Damascus.

ASKARI WA ISRAEL WAWAJERUHI WAPALESTINA


Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewalenga risasi na kuwajeruhi Wapalestina 35 waliokuwa wakiandamana katika mji wa al Khalil kwenye Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan. Wapalestina hao walikuwa wakiandamana baada ya Sala ya Ijumaa ya leo ili kuonyesha mshikamano wao kwa mateka wa Palestina wanaogoma kula katika jela za Israel. Askari wa Israel katika kuzuia maandamano hayo ya amani ya Wapalestina waliwashambulia na kuwajeruhi 35 miongoni mwao.
Katika upande mwingine wanajeshi wa Israel tangu leo asubuhi walimiminika katika mji wa Quds na kuwashambulia Wapalestina waliokwenda kuswali kwenye msikiti wa al Aqswa kwa gesi za kutoa machozi.  Hayo yamejiri sambamba na kushuhudiwa maandamano katika maeneo tofauti ya Palestina ya kuunga mkono mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa  bila kujulikana makosa yao katika jela za kuogofya za Israel.

TUNISIA YAPATA WAZIRI MKUU MPYA


Rais Moncif Marzouki wa Tunisia amekubali uteuzi wa Ali Larayedh aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo kama Waziri Mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Hamadi Jebali aliyejiuzulu. Larayedh ni miongoni mwa waasisi wa chama cha an Nahdha na amependekezwa na chama hicho kushika wadhifa huo.  Hivi sasa Larayedh atakuwa na siku 15 za kuunda serikali mpya na kuwasilisha mpango wake wa kuongoza serikali. Pia Rais Marzouki amemtaka Waziri Mkuu huyo mpya wa Tunisia kuunda serikali haraka iwezekanavyo akisisitiza kwamba nchi hiyo haiwezi kusubiri tena suala hilo.
Hamadi Jebali alitangaza kujiuzulu Jumanne baada ya mpango wake wa kuunda serikali inayowajumusiha wataalamu mbalimbali kufeli, mpango ambao ulianza kupingwa ndani ya chama chake cha an Nahdha. 

URUSI YAISHUTUMU MAREKANI JUU YA SYRIA

Urusi imeituhumu Marekani kuwa ni ndumilakuwili juu ya mzozo wa Syria ikisema kuwa nchi hiyo imezuia kutolewa kwa tamko la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kulaani mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotokea jana mjini Damascus. Akiukosoa msimamo wa Marekani waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amewaambia waandishi wa habari kuwa wanaamini kwamba kitendo hicho cha Marekani ni aina ya undumilakuwili. Jana kulifanyika mashambulizi katika eneo la katikati la Damascus ambayo yaliuwa watu 53 karibu na ubalozi wa Urusi nchini Syria eneo ambalo pia ni makao makuu ya chama tawala cha Baath. Makundi ya wanaharakati yanaarifu kuwa watu waliokufa ni 83. Mashambulizi hayo yanaaminika kufanywa na waasi ambapo nao wameitupia lawama serikali.

MAREKANI YAIONYA IRAN JUU YA NYUKLIA

Marekani imeionya Iran kuacha vitendo vya uchukozi kufuatia ripoti kuwa inauendeleza mpango wake wa nyuklia. Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, limesema kuwa Iran imeanza kuweka vifaa vya kuchuja mionzi ya nyuklia katika moja ya vinu vyake. Vifaa hivyo vinaaminika kuwa bado havijaanza kufanyakazi. Mara vitakapoanza kufanya kazi, vifaa hivyo vitaiwezesha Iran kufanya kazi zake za nyuklia kwa kasi kiasi cha kupata malighafi ambazo mataifa ya magharibi yanahofia zinaweza kutumikia kutengeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake huo wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Ripoti ya IAEA imetolewa ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza mazungumzo baina ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani ikiwemo Ujerumani. Mkutano huo utakuwa wa kwanza tangu kufanyika mazungumzo ya awamu tatu yaliyofanyika Juni mwaka jana.

Thursday, February 21, 2013

MARZOUKI ATAFUTA SULUHU TUNISIA

Rais Moncef Marzouki wa Tunisia amekutana na viongozi wa chama tawala cha Ennahda kuzungumzia uteuzi wa waziri mkuu mpya wa taifa hilo baada ya kujiuzulu kwa kiongozi aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Hamadi Jebali. Ofisi ya rais nchini humo imethibitisha kuwa Marzouki amekutana na mwenyekiti wa Ennahda Rachid Ghannouchi pamoja na viongozi wa vyama vingine viwili vinavyounda serikali yake kujaribu kutafuta suluhu.
Kumekuwepo na wito kutoka mataifa mbalimbali yakiitaka Tunisia kuchukua hatua sahihi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema ni muhimu viongozi wa taifa hilo wakazingatia kuutatua mzozo huo badala ya kuzozana. Tunisia imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu alipouawa kiongozi wa upinzani Chokri Belaid kilichofuatiwa na pigo la kujiuzulu kwa waziri mkuu.

WAASI WA SYRIA WATISHIA KUISHAMBULIA HIZBOLLAH

Kamanda wa jeshi huru la waasi wa Syria, FSA, Jenerali Selim Idriss, ametoa muda wa masaa 48 kwa kundi la Hezbollah la Lebanon kuacha kuzishambulia ngome zinazoshikiliwa na waasi la sivyo watalishambulia kundi hilo. Kitisho hicho kimetolewa jana baada ya waasi kuishambulia ndege ya kivita ya serikali kufuatia shambulizi kubwa lililouwa watu 20 mjini Damasucus. Jenerali Idriss ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kundi la Hezbollah limekuwa likijihusisha kwa muda mrefu na mapigano yanayoendelea nchini Syria, lakini sasa limevuka mipaka kwa kuvishambulia vijiji vilivyo karibu na eneo la Qusayr kwenye mji wa Homs. Kundi la Hezbollah limekanusha kuhusika na mashambulizi hayo ingawa mwezi Oktoba mwaka uliopita kiongozi wake Hassan Nasrallah alikiri kuwa baadhi ya wanamgambo wake waliwashambulia waasi wa syria.

HAGUE UKO ZIAANI LEBAON

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague yuko Lebanon kujadili juu ya mzozo unaoendelea nchini Syria pamoja na suala la kuimarisha mahusiano baina ya Uingereza na Lebanon. Hague alikutana na rais wa Lebanon Michel Suleiman na atakutana pia na Mkuu wa majeshi wa nchi hiyo Jenerali Jean Kahwagi. Hague aliyewasili Lebanon Jumatano jioni akitokea Qatar, aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa atajadili katika mazungumzo yake na maafisa wa Lebanon kuhusu hali ya kisiasa nchini humo pamoja na mzozo wa syria. Ziara ya kiongozi huyo inafanyika wakati huu kukiwa na hali ya wasiwasi katika mpaka wa Lebanon na Syria unayowahusisha waasi wa Syria pamoja na kundi la Hezbollah la Lebanon ambalo ni mshirika mkubwa wa utawala wa rais Bashar al-Assad.

UJERUMANI YAWASHITAKI WALIOIPA IRAN NDEGE ZAKE


Raia wawili wa Iran wamefunguliwa mashitaka kwa tuhuma za kusafirisha kwa njia haramu ndege za kivita zilizotengenezwa Ujerumani kwa ajili ya kutumiwa katika uchunguzi wa ndege ya kivita ijulikanayo kama Ababil 3 pamoja na ndege zisizokuwa na rubani. Ujerumani inakataza usafirishaji wa zana zake za kijeshi nchini Iran ambazo zinaweza kutumiwa kijeshi kinyume na hivyo kwenda kinyume na vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa dhidi ya taifa hilo. Watu hao ambao mmoja ana uraia wa Iran na Ujerumani na mwingine mwenye uraia wa Iran wamefunguliwa mashitaka ya kukiuka sheria za usafirishaji za Ujerumani. Ababil 3 inaaminika kuwa na ukubwa wa kilometa 145 na inaweza kuruka angani katika umbali unaofikia mita 4,300. Ndege hiyo imetengenezwa kwa ajili ya uchunguzi na masuala ya ukusanyaji taarifa za kijasusi, ingawa waendesha mashitaka nchini Ujerumani wanasema kuwa inawezekana pia zikatumika kama ndege za mashambulizi zisizokuwa na rubani.

UFARANSA YATUMIA SILAHA ZA ISRAEL HUKO MALI


Ufaransa inatumia ndege zisizo na rubani (drone) zilizotengenezwa Israel katika vita vyake dhidi ya watu wa Mali.
Kwa mujibu wa jarida la World Tribune, Jeshi la Ufaransa linatimua drone aina ya “Harfang” iliyotengenezwa Israel. Drone hiyo inatumiwa kuvurumisha makombora katika maeneo ya kaskazini mwa Mali.
Ufaransa ilianzisha vita dhidi ya Mali Januari 11 mwaka huu kwa kisingizio cha kupambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo.  
Wakati huo huo Rais Francois Hollande wa Ufaransa ametangaza kuwa, komandoo mmoja wa jeshi la nchi yake ameuawa kwenye mapigano ya kaskazini mwa Mali. Komandoo huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na waasi wa Ansaru Din katika milima ya Iforhas. 
Ufaransa inadai kuwa imeingia Mali kupambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo weledi wa mambo wanasema lengo kuu la hujuma ya Ufaransa huko Mali ni kupora utajiri wa nchi hiyo hasa mafuta ya petroli, dhahabu na madini ya urani.

IRAN YATENGENEZA RADA YENYE UWEZO WA KILOMITA 3000


Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu sasa inatengeneza mifumo ya rada za masafa marefu zenye uwezo kulinda usalama wa masafa ya kilomita 3000.
Vahidi amesema hayo leo Jumanne na kuongeza kwamba, Iran imekuwa ikitengeneza kwa wingi rada za kijeshi zenye uwezo wa wigo wa kilomita 500-700 na sasa inatengeneza rada mpya zenye wigo wa kilomita 1000 hadi 3000.
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema, baadhi ya rada hizo zilizotengenezwa hapa nchini zitatumika pia kutafuta satalaiti zilizoko kwenye anga za mbali.
Vahidi ameongeza kuwa hivi karibuni Iran itazindua rada za kisasa, manowari mpya za kivita, boti zenye uwezo wa kupaa na nyambizi za kisasa kabisa. Mapema jana Jumatatu Vahidi alitangaza kuwa hivi karibuni Iran itaonyesha ndege mpya zisizo na rubani au drone zenye uwezo mkubwa wa kivita na kiupelelezi.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya kujihami na imeweza kujitosheleza katika uzalishaji wa zana muhimu za kivita. Iran imesisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi umejengeka katika msingi wa kujihami na si tishio kwa nchi nyingine.

WAZIRI MKUU WA TUNISIA AJIUZULU

Hamad Jebali Waziri Mkuu wa Tunisia jana alitangaza kujiuzulu kufuatia mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Jebali alitangaza kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa katika jitihada zake za kuunda serikali mpya ya kiteknokrasia yaani inayowajumuisha wataalamu wa taaluma mbalimbali badala ya wanasiasa. Jebali alisema baada ya kukutana na Rais Munsif Marzouq kama ninavyomnukuu:"niliahidi na kutoa hakikisho kuwa nitajiuzulu wadhifa huu nilionao wa mkuu wa serikali iwapo juhudi zangu zitashindwa, na ndivyo nilivyofanya",mwisho wa kunukuu. Jebali  hata hivyo amesema kuwa kushindwa kwa juhudi zake hakumaanishi kushindwa Tunisia au kushindwa mapinduzi ya Januari mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta wa nchi hiyo Zainul Abidin bin Ali. 

HAMAS YAITAKA ISRAEL IFUATE UTARATATIBU WA KUBADILISHANA MATEKA

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na kukiuka mkataba wa ubadilishanaji mateka. Sami Abu Zuhri, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameitahadharisha Israel na kusisitiza kwamba, utawala huo ghasibu unapaswa kutazama upya, tena haraka iwezekanavyo uamuzi wake wa kutaka kuwatia mbaroni tena mateka wa Kipalestina walioachiliwa huru. Sami Abu Zuhri amesema, Hamas inautaka utawala huo ufikirie upya uamuzi wake huo kabla haujajuta. Wakati huo huo, Sami Abu Zuhri, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amezikosoa vikali siasa za kindumakuwili za Marekani kuhusiana na kadhia ya Palestina na kusisitiza kwamba, Washington inakwamisha mwenendo wa utekelezwaji makubaliano ya maridhiano ya kitaifa huko Palestina.

WAMAGHARIBI HAWALIONI SUALA LA MYANMAR


Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje wa Bunge la Iran ameashiria ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya kukiukwa haki za Waislamu wa Myanmar na kusema kuwa, siasa za kindumilakuwili za Wamagharibi kuhusu haki za binadamu na kulinda utu wa mwanadamu zimechangia katika mauaji ya Waislamu wa Myanmar.
Hussein Subhani-niya ameongeza kuwa wakati magaidi wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi wanapotenda jinai huko Syria, Iraq, Pakistan na Afghanistan nchi hizo pia hunyamaza kimya, suala linaloonesha kwamba Wamagharibi ndio waungaji mkono wakuu wa magaidi duniani. Amesema, kuuawa bila hatia Waislamu wa Myanmar ni mfano wa wazi wa kukiukwa haki za walio wachache katika nchi hiyo.
Wakati huo huo Tomas Ojea Quintana, mwakilishi maalum wa UN katika masuala ya haki za binadamu pia mwishoni mwa safari yake ya siku 5 huko Myanmar amesema kwamba, licha ya madai ya serikali ya kufanya mabadiliko nchini humo lakini bado Waislamu wanadhulumiwa.

LARIJANI ASEMA IRAN HAITAACHA KUIUNGA MKONO IRAN

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amesema kuwa, kuuliwa kamanda wa ngazi ya juu wa vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) hakutaathiri uungaji mkono wa Iran kwa Lebanon. Larijani amesema hayo leo na kuongeza kuwa, maadui wanapasa kufahamu kwamba Iran haitaacha kuliunga mkono taifa la Lebanon kutokana na kuuawa Jenerali Hassan Shateri. Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo kwamba Iran itaendelea kuiunga mkono Lebanon kwa ushupavu kabisa. Itakumbukwa kuwa kamanda mmoja wa vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Jenerali Hassan Shateri alitoa huduma na kufanya juhudi kubwa katika kufanikisha ujenzi wa maeneo mbalimbali yaliyoharibiwa huko kusini mwa Lebanon kutokana na uvamizi na vita vya utawala haramu wa Kizayuni. Mwaka 2006 Israel ilianzisha vita dhidi ya Lebanon, vita ambavyo vilidumu kwa siku 33 na kuharibu miundo mbinu na majengo mengi ya kusini mwa nchi hiyo. Tangu wakati huo Iran imekuwa ikitoa msaada mkubwa katika juhudi za kuyajenga upya maeneo hayo yaliyoathiriwa na vita vya utawala ghasibu wa Kizayuni.

Sunday, February 17, 2013

KATIBU MKUU WA HIZBUL LAH ATANGAZA MSIMAMO WAO DHIDI YA ISRAEL


Kufuatia vitisho vinavyooengezeka kila uchao vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon na kukiuka mara kwa mara utawala huo ardhi ya Lebanon, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah ameitahadharisha Tel Aviv juu ya madhara ya hatua zozote za hujuma dhidi ya ardhi ya nchi hiyo. Katika hotuba yake kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi viongozi wa muqawama wa Lebabon dhidi ya Israel, Sayyid Hassan Nasrullah jana alisema kuwa, viwanja vya ndege, bandari na vituo vya umeme vya utawala wa Kizayuni vinaweza kulengwa na makombora na roketi za Hizbullah, na kwamba mahesabu yoyote ya kimakosa ya viongozi wa Israel yanaweza kupelekea kuangamizwa kwao. Kuhusiana na kuunga mkono muqawama wa Palestina Sayyid Nasrullah amesema, muqawama nchini Lebabon unaunga mkono nguvu za wananchi wa Palestina na kwamba Wazayuni waliozikalia ardhi za Palestina kwa makumi ya miaka, katika siku za hivi karibini wataangamia. Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, muqawama umeleta mafanikio makubwa nchini humo na kwamba katika mwaka uliopita umefanikiwa kubadilisha uwiano ambapo kwa miaka kadhaa iliyopita madola ya kibeberu yalikuwa yakiathiri mazingira ya eneo hilo.
Bila shaka kusimama kidete wananchi wa Lebanon dhidi ya Wazayuni kwa uongozi wa Harakati ya Hizbullah kumejenga ngome imara dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni. Suala linalopaswa kukumbushwa hapa ni kuwa, kila siku maqawama unazidi kupendwa na wananchi wa Lebanon na fikra za waliowengi katika eneo huku suala hilo likipewa kipaumbele na viongozi wa nchi hiyo. Harakati ya muqawama nchini Lebanon iliyopelekea kushindwa mara kadhaa utawala wa Kizayuni katika miaka kadha iliyopita, inabainisha mabadiliko ya uwiano yaliyoshuhudiwa kutoka upande wa viongozi wa Tel Aviv na washirika wao katika eneo. Israel na washirika wake kwa kuendeleza siasa za kuzusha wasiwasi na woga katika eneo na kuongopa kwamba utawala huo hauwezi kushindwa, wamekuwa wakikusudia kuangamiza muqawama mkabala na kujipanua utawala huo na madola ya kibeberu katika Mashariki ya Kati. Lakini kushindwa utawala huo kutokana na kusimama kidete wananchi wa Lebanon, ambako kulishuhudiwa wazi mwaka 2000 Miladia, kumekwamisha mipango na njama za Israel na Marekani dhidi ya Lebanon na eneo zima kwa ujumla. Kushindwa huko kulipelea Israel irudi nyuma kutoka katika maeneo ya Lebanon iliyokuwa ikiyakalia kwa mabavu mwaka 2000. Kushindwa Tel Aviv na muqawama kuliendelea kushuhudiwa katika vita vya siku 33 mwaka 2006 na hivyo kuvunja kabisa madai ya uongo ya kutoshindwa utawala huo katika medani ya vita. Hii ni katika hali ambayo, kushindwa Israel katika vita hivyo, kulikwamisha kabisa mpango wa kibeberu wa Marekani kwa ajili ya Masahariki ya Kati uliojulikama kama 'Mashariki ya Kati Mpya' uliokuwa ukifuatiliwa kwenye vita hivyo. Muqawama wa Lebanon umebadilika na kuwa kigezo cha mapambano ya mataifa ya eneo dhidi ya utawala wa Kizayuni, na ushindi wake umeongeza nguvu na matumaini kwa Wapalesina katika mapambanao yao dhidi ya adui Mzayuni. Uzoefu unaonesha kuwa, kusimama kidete na kuendeleza muqawama ndiyo njia pekee ya kukabiliana na siasa za kupenda kujitanua za Israel, kwani njia za suluhu hazijakuwa na faida yoyote zaidi ya kushadidisha siasa za kupenda kujitanua na jinai za utawala huo. Hii ndio sababu Sayyid Hassan Nasrullah sambamba na kubainisha wazi kuwa aduia mkuu wa wananchi wa eneo la Mashariki ya Kati ni Israel na washirika wake, akasisitiza udharura wa kudumishwa muqawama na kusimama kidete dhidi ya Wazayuni.    
Na Fatma Muhammad Mbepey

RUSSIA YASEMA MRIPUKO ULIODHANIWA NI KIMONDO NI MAJARIBIO YA SILAHA ZA MAREKANI


Mjumbe mmoja katika bunge la Russia amesema mlipuko wa kimondo (meteor strike) uliojiri hivi karibuni katika eneo la milima ya Ural nchini humo ulikuwa jaribio la silaha mpya za Marekani.
Mbunge mashuhuri Vladimir Zhirinovsky amesema kinyume na inavyodhaniwa kilichoshuhudiwa  eneo la Ural si jiwe la nyota bali ni Wamarekani waliokuwa wakifanyia majaribio silaha zao mpya. Amedai kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amekuwa akitaka kuzungumza na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov bila mafanikio lengo likuwa ni kumuonya kuhusu kadhia hiyo. Siku ya Ijumaa kimondo kuliripuka angani na baadhi ya vipande kuporomoka katika eneo la Ural ambapo watu zaidi ya 1,200 walijeruhiwa. Aghalabu walipata majeraha kutokana na gilasi za madirisha  yaliyovunjika kutokana na nguvu ya mripuko mkubwa uliojiri katika tukio hilo.
Maafisa wa Wizara ya Maafa Russia wamesema wangali wanalitafuta jabali ambalo lililoporomoka kutoka angani na kuanguka katika Ziwa Chbarkul  lililoganda barafu.

KARZAI APIGAA MARUFUKU MASHAMBUIZI YA ANGA YANAYOFANYWA NA NATO


Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema atatoa dikrii ya kupiga marufuku vikosi vya usalama vya nchi hiyo vinavyofanya operesheni katika maeneo ya raia kuomba msaada kwa vikosi vya NATO ili kutekeleza mashambulio ya anga katika maeneo hayo. Karzai ametoa tamko hilo leo zikiwa zimepita siku tatu tu tangu raia kumi walipouawa katika shambulio la anga lililofanywa na NATO mashariki mwa nchi hiyo. Mashambulio ya anga ya Shirika la Kijeshi la NATO na vifo vya raia vinavyosababishwa na mashambulio hayo yamepelekea kuzuka mkwaruzano kati ya Rais wa Afghanistan na vikosi vya kigeni vinavyomsaidia katika vita dhidi ya wanamgambo wa Taliban. Akihutubia hadhara ya maafisa, makomando na wanafunzi wa Akademia ya Taifa ya Kijeshi mjini Kabul Karzai amesema atatoa dikrii hiyo hapo kesho na kwamba kuanzia hapo vikosi vya usalama vya Afghanistan havitoweza katika hali yoyote ile kuviomba vikosi vya kigeni vifanye shambulio la anga kwenye maeneo ya nyumba na vijiji wakati wa operesheni za vikosi hivyo. Watu kumi wakiwemo watoto watano na wanawake wanne waliuawa siku ya Jumatano wakati makombora ya ndege za vikosi vya NATO yalipolenga nyumba mbili kwenye eneo la Shultan huko katika mkoa wa Kounar mashariki mwa Afghanistan.

PAKISTAN YAOMBOLEZA MAUAJI YA WATU 81

Idadi ya vifo kufuatia shambulizi kubwa la bomu lililofanywa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kusini magharibi ya Pakistan imepanda leo na kufikia watu 81. Wakaazi wa eneo hilo wametishia kufanya maandamano ikiwa hakuna hatua madhubuti itakayochukuliwa dhidi ya waliofanya shambulio hilo. Bomu hilo lililokuwa na takribani tani moja ya miripuko, na kufichwa ndani ya tangi la maji, liliripuka jana jioni, katika soko moja lillokuwa limejaa watu katika mji wa Hazara, ambao unakaliwa na waislamu wengi wa Kishia. Eneo hilo liko karibu na Quetta; mji mkuu wa mkoa wa Baluchistan. Afisa mkuu wa polisi eneo hilo amesema idadi ya waliojeruhiwa imefika watu 178. Mkoa wa Baluchistan umeendelea kukumbwa na mashambulizi za kimadhehebu baina ya waislamu wa madhehebu ya Sunni walio wengi nchini humo, na washiya ambao wanajumlisha moja juu ya tano ya jumla ya watu milioni 180 nchini Pakistan. Shambulizi hilo la Jumamosi limefanya idadi ya mauwaji ya mashambulizi la kimadhehebu mwaka huu nchini Pakistan kufikia 200, ikilinganishwa na zaidi ya 400 waliouawawa mwaka wa 2012, mwaka ambao Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliztaja kuwa mbaya zaidi dhidi ya Washiya nchini humo.