Sunday, August 25, 2013

PENTAGON YASEMA IKO TAYARI KWA LOLOTE JUU YA SYRIA

Chuck Hagel Waziri wa Ulinzi wa Marekani amekariri kwamba Pentagon imejitayarisha kuchukua chaguo lolote la dharura dhidi ya Syria na ipo tayari kutumia nguvu iwapo Rais Barack Obama ataidhinisha suala hilo.Hagel amesema kwamba, Rais Obama ameitaka Wizara ya Ulinzi ya Marekani kujitayarisha kwa chaguo lolote lile litakalowezekana kuchukuliwa dhidi ya Syria.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameongeza kuwa, maafisa wa Marekani wanachunguza suala la kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Assad kutokana na ripoti ya kufanyika mashambulizi ya silaha za kemikali katika vitongoji vya Damascus wiki iliyopita.Hata hivyo ripoti zinasema kwamba, mashambulizi hayo ya silaha za kemikali yamefanywa na waasi wa Syria wanaoungwa mkono na nchi za Ulaya,  Marekani  na baadhi ya nchi za Kiarabu.

RAIS WA YEMEN AUNGA MKONO DRONE KUTUMIKA NCHINI HUMO

Rais Abd Rabbuh Mansur Hadi wa Yemen ameunga mkono mashambulizi ya mauaji ya ndege za Marekani zisizo na rubani yaani "drone" nchini humo. Mansur Hadi ameeleza kuwa mashambulizi ya drone za Marekani yanatekelezwa  kulingana na makubaliano yaliyosainiwa kati ya Washington na Ali Abdullah Saleh dikteta wa zamani wa Yemen baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.
Rais wa Yemen amesema hatua ya nchi yake ya kushirikiana na Marekani katika mapambano ya kile alichokitaja kuwa  dhidi ya ugaidi siyo siri. Ameongeza kuwa Yemen ina maafisa wake wa kijeshi katika vituo vya kuendeshea mashambulizi hayo ya drone nchini Djibouti na Bahrain. Marekani imekuwa ikikosolewa vikali kutokana na hatua yake ya kuzidisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Yemen, ambako raia wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana mara kwa mara wakilaani hatua ya Washington ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya Yemen.

MAREKANI YALAANI SHAMBULIZI LA LEBANON

Serikali ya Marekani imelaani shambulizi lililotokea huko Lebanon na kusababisha vifo vya watu 42 mpaka sasa huku mamia wakijeruhiwa baada ya magari yalokuwa yameegeshwa nje ya msikiti kulipuliwa mjini Tripoli. Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Susan Rice ameandika kupitia mtandao wa Twita kuwa Marekani imelaani vikali shambulizi hilo na kutoa pole kwa majeruhi na ndugu za watu wasiokuwa na hatia ambao walipoteza maisha yao. Mashambulizi hayo mawili yamejiri wakati wa ibada za waislamu mjini Tripoli ambapo wafuasi wa Suni ambao wanaunga mkono waasi wa Syria wamekuwa wakihusishwa na ghasia za mara kwa mara dhidi ya wale wanaomuunga mkono raisi wa Syria Bashar al Assad.
Serikali ya Washington mara kadhaa imevunja ukimya juu ya machafuko ya Syria na kuenea katika maeneo kadhaa na hususan kuvuruga amani ya lebanon. Naibu Msemaji wa serikali Marie Harf ametoa wito kwa pande zote mbili nchini Lebanon kuwa watulivu.

KIONGOZI WA WAASI SUDAN ATEULIWA KUWA MAKAMU WA RAIS

Raisi wa Sudani Kusini Salva kiir amemteua kiongozi wa zamani wa waasi James Wani Iga kuwa makamu wake,vyombo vya habari vya serikali nchini humo vimearifu. Igga, ambaye amekuwa spika wa bunge la Sudan kusini tangu 2005 ameonekana kuwa chaguo linalosawazisha tofauti ya kikabila kati ya viongozi wa taifa na itasaidia sana hali ya mambo kuelekea uchaguzi mwaka 2015.
Igga ambaye ni Naibu mwenyekiti wa chama cha SPLM anatokea katika kabila la Bari ambao ni wenyeji wa eneo la Juba. Mwezi uliopita raisi Kiir alichukua hatua ya kushangaza baada ya kuvunja Baraza la Mawaziri na kisha kumfuta kazi Makamu wa Rais Riek Machar kitu kilichotajwa kuchangiwa na tofauti za kisiasa baina yao. Makamu mpya wa Rais Kiir anatarajiwa kushauriana naye kuunda Baraza jipya la Mawaziri.

RAFAH YAFUNGULIWA TENA

Serikali ya mpito ya Misri leo imekifungua tena kivuko cha Rafah kilichoko kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na eneo la Ukanda wa Gaza la ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wagonjwa wanaohitaji kupatiwa matibabu nje ya Ukanda wa Gaza walikuwa wameshindwa kuelekea huko Misri huku mamia ya Wapalestina waliokuweko nchini humo wakishindwa kurejea makwao kutokana na kufungwa njia hiyo pekee ya mpakani kwa wakaazi wa Gaza. Uhusiano kati ya serikali halali ya Palestina inayoongozwa na HAMAS yenye makao yake Ukanda wa Gaza na serikali ya mpito ya Misri umekuwa wa kusuasua tangu jeshi lilipomuondoa madarakani rais Muhammad Morsi aliyekuwa muitifaki mkubwa wa HAMAS. Maher Abu Sabha, afisa anayesimamia kivuko cha Rafah kwa upande wa Palestina amesema mamlaka za Misri zinakifungua kivuko hicho kwa muda wa saa chache tu kwa siku. Maafisa wa HAMAS wameilalamikia hatua ya serikali ya Misri ya kupunguza kiwango cha watu wanaoruhusiwa kupita kwenye kivuko cha Rafah kutoka watu 1,200 hadi 300 kwa siku tangu Julai 3 wakati jeshi lilipomuondoa madarakani Morsi. Tangu mwaka 2007, utawala wa Kizayuni umeshadidisha mzingiro dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na kusababisha maafa na matatizo makubwa kwa wananchi hao.

WAISLAM NIGERIA WAANDAMANA KUTAKA MORSI KUREJESHWA

Maelfu ya Waislamu wameandamana kwa amani kaskazini mwa Nigeria leo kutaka kurejeshwa madarakani kwa Rais wa Misri Mohammed Mursi aliyepinduliwa na jeshi mwezi uliopita.Kiasi ya waandamanaji 4,000 waliokuwa wamebeba mabango waliimba nyimbo za kumsifu Mursi nje ya msikiti katika mji wa Kano.Waandalizi wa maandamano hayo wanasema takriban waandamanaji 5,000 walishiriki.Kiongozi wa maandamano hayo sheikh Abubakar Mujahid amewaambia wanahabari kuwa wanataka kuachiliwa huru kwa Mursi na wafungwa wengine wa kisiasa wanaozuiliwa na serikali ya muda ya Misri.Nigeria taifa lililo na idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika ya kiasi ya watu milioni 160 limegawanyika nusu kwa nusu ambapo Waislamu wanaishi hasa kaskazini  na Wakristo wanaokaa zaidi kusini mwa nchi hiyo.

Saturday, August 24, 2013

WANANCHI WA CONGO WAANDAMANA

Mamia ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameandamana kupinga mashambulizi yanayowalenga wakati wa makabiliano kati ya wanajeshi wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa na wapiganaji wa kundi la waasi la M23 katika mji wa Goma ulioko mashariki mwa nchi hiyo.Mwanamke mmoja na watoto wawili waliuawa mapema leo asubuhi katika mji huo wa Goma ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini.Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakijibu mashambulizi ya waasi wa M23 tangu Jumatano.Msemaji wa kikosi hicho maalumu Luteni Colonel Felix Prosper Basse amesema hali katika eneo hilo ni tete mno na kwamba shambulio hilo la hivi karibuni kabisa halikubaliki kamwe kwani linawalenga raia. Mapigano hayo yamewalazimu kiasi ya watu laki nane kutoroka makwao.Umoja wa Mataifa umetuma kikosi maalum cha wanajeshi 3,000 mashariki mwa Congo hususan kukabiliana na makundi ya waasi.Basse amesema wanashirikiana na wanajeshi wa nchi hiyo kuhakikisha usalama wa raia unadumishwa na kuahidi shambulio kama hilo halitafanyika tena. 

MAREKANI KUICHUKULIA HATUA SYRIA

Rais wa Marekani Barrack Obama amekutana na washauri wake wakuu wa masuala ya kiusalama kujadili madai ya matumzi ya silaha za kemikali nchini Syria.Maafisa wa Ikulu ya rais wamesema wanaangalia hatua kadhaa ambazo wanaweza kuchukua kuambatana na maslahi ya kitaifa ya Marekani na kutathmini vipi malengo yanaweza kuendelezwa nchini Syria. Duru zimearifu kuwa jeshi la Marekani limeanza kujiandaa kwa uwezekano wa kuishambulia Syria iwapo rais wao atatoa agizo hilo.Huku hayo yakijiri maafisa wakuu wa kijeshi kutoka Marekani,Uingereza na nchi kadhaa za Kiarabu wanatarajiwa kukutana mjini Amman Jordan kuzungumzia hali hiyo ya Syria ambapo mamia ya watu waliuawa kwa kile kinachoshukiwa kuwa matumizi ya silaha za kemikali karibu na mji mkuu Damascus.Utawala wa Syria leo umewashutumu waasi kwa mauaji hayo madai ambayo pia waasi inainyooshea kidole cha lawama serikali.Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa Angela Kane amewasili leo nchini Syria ili kuzungumzia uchunguzi wa matumizi ya silaha hizo.Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema kuna ushahidi kuwa silaha hizo zilitumika na kulaani vifo vya raia.

Monday, August 19, 2013

MAAFISA WA POLISI 24 WAUAWA NCHINI MISRI

Takriban maafisa 24 wa polisi kutoka Misri wameuawa kwenye shambulizi la kuvizia katika eneo la Rasi la Sinai. Duru zinaarifu polisi hao walikuwa kwenye msafara wa mabasi mawili yaliyoshambuliwa na kundi la watu waliokua na silaha karibu na mji wa Rafa mpaka na Ukanda na Gaza. Polisi watatu walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Katika siku za karibuni jeshi la Misri limeimarisha operesheni dhidi ya wanamgambo eneo la Sinai hususan baada ya mashambulizi kuongezeka tangu kuanguka kwa uliokua utawala wa Hosni Mubarak mwaka 2011. Misri imekua ikishika doria eneo la Sinai chini ya mkataba wa mwaka 1979 kati ya Israel na Misri.Mashirika ya habari yanaripoti kwamba wanaume wanne waliojihami kwa silaha walisimamisha mabasi hayo na kuwaamrisha abiria wote kuondoka kisha wakaanza kuwapiga risasi.
Baadhi ya duru zinasema washambuliaji hao walitumia maroketi kulenga mabasi hayo. Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari kufuatia maandamano ya umma yaliofuatia kuondolewa mamlakani kwa Muhammed Morsi kama Rais wa nchi hiyo. Amri ya kutotoka nje usiku imewekwa mji mkuu Cairo.
Zaidi ya watu 800 wakiwemo polisi 70 wameuawa tangu Jumatano ya wiki jana wakati jeshi lilipovunja kambi za wafuasi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi. Na hapo Jumapili mahabusu 36 walikufa wakati wakisafirishwa katika jela moja nje ya mji wa Cairo.Serikali na jeshi wamesema mahabusu hao walikosa hewa kwenye gari walimokua. Hata hivyo Muslim Brotherhood wametaja kitendo hicho kama mauaji ya kinyama.
Huku haya yakiarifiwa Muungano wa Ulaya umeitisha kikao cha dharura kujadili uhusiano wake na Misri. Muungano huo umetoa taarifa ya pamoja na kusisitiza haja ya kumaliza ghasia mara moja.Wafuasi wa Morsi wametaja kuondolewa kwake kama mapinduzi, lakini jeshi na serikali zinasema vuguvugu la Muslim Brotherhood liliendesha kampeini ya ugaidi tangu kuondolewa kwa kiongozi wake kama Rais.

MAREKANI YAANZA MAZOEZI YA KIJESHI NA KOREA KUSINI

Korea ya Kusini na Marekani zimeanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayofanyika kila mwaka ambayo kwa kawaida Korea ya Kaskazini huyaona kama ni mazoezi ya kujiandaa kuivamia nchi hiyo. Mazoezi hayo ya kijeshi yanawahusisha wanajeshi 30,000 wa Marekani na 50,000 wa Korea ya Kusini na yamepangwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi wa Agosti. Safari hii shutuma za Korea ya Kaskazini dhidi ya mazoezi hayo hazijakuwa za juu sana kutokana na kwamba nchi zote mbili za Korea zimekuwa zikielekeza juhudi zao katika kulifunguwa tena eneo la pamoja la viwanda ambalo lilifungwa hapo mwezi wa Aprili wakati wa mvutano wa kijeshi wa hivi karibuni katika Ghuba ya Korea. Baada ya duru saba za mazungumzo, nchi hizo mbili hasimu wiki iliopita zilikubaliana juu ya mpango wa kuanza tena kazi katika eneo hilo viwanda la Kaesong ambalo ni muhimu katika kuipatia mapato Korea ya Kaskazini.

MERKEL APENDEKEZA MARUFUKU YA SILAHA MISRI

Ujerumani imependekeza kupiga marufuku upelekaji wa silaha nchini Misri kama hatua itakayoratibiwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya kupinga hatua ya serikali ya Misri ya kuvunja maandamano kwa kutumia nguvu na kusababisha umwagaji damu. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametowa wazo hilo katika mahojiano na televisheni la taifa hapo jana. Kansela Merkel amesema hatua zote zinaweza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kupeleka silaha nchini Misri zikiwemo zile ambazo tayari zimeidhinishwa kwa serikali ya Misri. Amesema suala hilo litajadiliwa kati ya Ujerumani na washirika wenzake wa Umoja wa Ulaya katika mkutano utakaofanyika siku chache zijazo. Umoja wa Ulaya utakuwa na kikao chake cha kwanza cha mazungumzo ya dharura kutokana na umwagaji damu nchini Misri uliozusha wasiwasi mkubwa huku ukionya kwamba utaangalia upya uhusiano wake na nchi hiyo iliokumbwa na ghasia.

KIONGOZI MWANDAMIZI WA HAMAS ASEMA ABBAS SI KIONGOZI WA WAPALESTINA

Mahmoud al Zahar, kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema wananchi wa Palestina hawakumtuma Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani akafanye mazungumzo na utawala wa Kizayuni wa Israel. Akizungumza na kanali ya televisheni ya al Manar Al Zahar, mbali na kusisitiza kuwa mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni hayana maana yoyote amesema Mahmoud Abbas hawezi kuwa mwakilishi mzuri kwa ajili ya wananchi wa Palestina kwa sababu hawezi kutetea haki za Palestina. Akijibu suali la madai kwamba HAMAS imeacha mapambano na muqawama dhidi ya utawala ghasibu wa Israel Mahmoud al Zahar amesema HAMAS ingali imeshikamana na msimamo wake wa muqawama na ukombozi wa ardhi za Palestina na inawaheshimu wale wote walioikubali fikra ya muqawama. Afisa huyo mwandamizi wa HAMAS ametoa wito pia wa kutekelezwa makubaliano ya maridhiano ya kitaifa ya Palestina. Makubaliano ya maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina yalisainiwa rasmi miaka miwili nyuma mjini Cairo Misri kati ya HAMAS na harakati ya Fat-h inayoongozwa na Mahmoud Abbas lakini hadi sasa hayajatekelezwa kutokana na pingamizi na ukwamishaji unaofanywa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina

WAFUASI WA MORSI 38 WAUAWA GEREZANI

Kiongozi mmoja wa usalama nchini Misri ametangaza kuwa, wanachama 38 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin wameuawa, katika tukio la mapigano kati ya askari polisi na watu waliokuwa na silaha, waliotaka kuwatorosha watu hao kutoka gerezani. Habari zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea karibu na jela ya Abu Zaabal katika mkoa wa al-Qalyubiyah. Aidha wafungwa hao walikuwa wamemteka polisi mmoja katika mapambano hayo. Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetangaza kuwa, polisi walifanikiwa kumuokoa polisi huyo ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya. Jana wafuasi wa Ikhwanul Muslimin walisitisha maandamano mjini Cairo kwa kile walichosema kuwa ni kuepusha umwagikaji damu zaidi dhidi yao.  Ripoti iliyotolewa na harakati hiyo, ilisema kuwa, Ikhwan wameamua kusitisha maandamano yao, kutokana na kuwepo hali tete nchini humo. Kabla ya hapo, ilikuwa imepangwa kufanyika maandamano ya nchi nzima, kwa ajili ya kutaka kurejeshwa Muhammad Mursi, Rais halali wa Misri aliyepinduliwa na jeshi la nchi hiyo.

WAZIRI MKUU WA MISRI ATAKA KUTOINGILIWA MASUALA YA NDANI YA NCHI HIYO

Serikali ya mpito ya Misri imezitaka baadhi ya nchi kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Nabil Fahmy Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa Cairo inapinga uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala yake ya ndani. Fahmy amesema matukio ya sasa huko Misri ni masuala ya ndani na kwamba uingiliaji wa nchi za nje utazidisha tu ghasia na machafuko nchini humo.  
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameyasema hayo katika hali ambayo nchi nyingi duniani zimelaani jinai iliyofanywa na serikali ya mpito ya Misri kufuatia kuuliwa ovyo raia na jeshi la nchi hiyo wakiwemo wanawake. Nchi mbalimbali duniani zimetaka kusimamishwa mara moja mashambulizi ya jeshi la Misri dhidi ya raia. Mamia ya wafuasi wa Muhammad Mursi rais wa Misri aliyepinduliwa na jeshi la nchi hiyo wameuliwa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya jeshi dhidi ya wafuasi hao.  

MAANDAMANO YAFANYIKA YEMEN KULAANI MATUMIZI YA DRONE

Maelfu ya Wayemeni jana walimiminika kwenye mitaa ya Sana'a mji mkuu wa Yemen wakipinga kushtadi mashambulizi ya drone yaani ndege za Marekani zisizo na rubani nchini humo. Waandamanaji hao pia wamelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege za Marekani zisizo na rubani yaliyoua karibu watu 40 katika maeneo mbalimbali ya Yemen. Wananchi wa Yemen wanasema kuwa mashambulizi ya drone za Marekani yanawalenga wao katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kuitaka serikali ya Sana'a kutafuta suluhisho kwa mashambulizi hayo ya Marekani. Tarehe 16 mwezi huu pia raia wa Yemen walifanya maandamano huko Sana'a wakiilaumu serikali ya nchi hiyo wakisema kuwa inaunga mkono ajenda za kigeni na kupuuza matakwa ya wananchi. 

Sunday, August 18, 2013

WANAWAKE WA KIISLAM WAANDAMANA UFARANSA

Wanawake wa Kiislamu nchini Ufaransa wamefanya maandamano kutetea vazi la stara ya Kiislamu la Hijabu. Maandamano hayo yalifanyika jana katika eneo la Trappes huko kaskazini mwa nchi hiyo. Wanawake hao wa Kiislamu wameandamana kulalamikia ongezeko la mashambulio yanayotokana na chuki dhidi ya Uislamu wanayofanyiwa wanawake wanaovaa hijabu na kupinga ushadidishaji wa sheria zinazoweka mipaka ya uvaaji hijabu nchini Ufaransa. Maandamano hayo yalianzia mbele ya msikiti wa eneo la Trappes hadi kwenye jengo la Manispaa ya eneo hilo. Maandamano ya jana yamefanyika kufuatia mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya wanawake wa Kiislamu wanaovaa hijabu na kushindwa polisi kukabiliana na vitendo hivyo katika mji huo wa Trappes. Mbali na Polisi ya Trappes kushindwa kukabiliana na mashambulio yanayofanywa dhidi ya wanawake wa Kiislamu wanaovaa hijabu, inatuhumiwa pia kushirikiana na watu wenye chuki na Uislamu katika kufanya vitendo vya kibaguzi na miamala miovu dhidi ya Waislamu

ISRAEL YAOMBAMSAADA ZAIDI WA KIJESHI TOKA MAREKANI

Maafisa wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanajadili kuongeza kiwango cha fedha za msaada wa kijeshi wa Washington kwa Tel Aviv huku pande hizo mbili zikishauriana kuhusu msaada mpya wa kijeshi kwa kipindi cha miaka 10 ijayo. Jarida la Defense News limeripoti kuwa chini ya makubaliano ya sasa ya msaada huo uliosainiwa na pande mbili mwaka 2007, dola bilioni 30 za walipa kodi wa Marekani zinamiminwa kwenye mfuko wa hazina wa Israel. Hata hivyo Utawala wa Kizayuni umekuwa na wasiwasi kutokana na kuongezeka uuzaji silaha za Marekani kwa nchi za Mashariki ya Kati na hivyo unaitaka Washington kuuongezea kitita cha fedha katika msaada wa kuipatia silaha za kisasa zaidi. Msaada wa kila mwaka wa kijeshi unaotolewa na Marekani kwa Israel umeongezeka kutoka dola bilioni 2.4 hadi dola bilioni 3.1, ambapo kwa mujibu wa makubaliano ya sasa kiwango hicho kitaendelea hadi mwaka 2017. Wakati alipofanya safari huko Israel ambayo ni ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu mnamo mwezi Machi mwaka huu, Rais Barack Obama wa Marekani alisema ameafiki kuanza kufanya majadiliano na Israel juu ya kurefusha kipindi cha utoaji msaada wa kijeshi kwa utawala huo haramu

HOFU YA WAPALESTINA WALIOGOMA KULA

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya wafungwa saba wa Kipalestina ambao wamesusia chakula katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika taarifa siku ya Jumamosi, shirika hilo lilisema kunapaswa kutafutwa suluhisho kuhusu wafungwa hao. ICRC imesema ina wasiwasi mkubwa hasa kuhusu mfungwa aitwaye Imad Abdelaziz Abdallah al-Batran ambaye amesusia chakula kwa wiki kadhaa sasa. Wafungwa hao Wapalestina wamesusia chakula kulalamikia hali mbaya katika jela hizo za utawala wa Israel.
Mapema mwezi huu Wizara ya Masuala ya Wafungwa Palestina ilisema utawala haramu wa Israel unawashikilia Wapalestina 5,100 wakiwemo watoto 250 na wanawake 14 katika gereza 17. Wakuu wa jela za kuogofya za Israel wamekuwa wakikiuka haki za binadamu za wafungwa wa Palesitna kama vile kuwashikilia pasina kuwafunguliwa mashtaka na kuwatesa.

RAJOELINA NA LALAO WAZUIWA UCHAGUZI

Korti inayosimamia masuala ya uchaguzi nchini Madagascar imeyakataa maombi ya kugombea kiti cha rais,rais wa sasa Andry Rajoelina na Lalao Ravalomanana, ambae ni mke wa rais wa zamani.Taasisi hiyo imeyakataa pia maombi ya rais wa zamani Didier Ratsiraka.Korti ya uchaguzi imehalalisha uamuzi huo kwa kile ilichokiita "kasoro zilizojitokeza katika kufuatwa sheria" na korti ya awali ya uchaguzi.Uamuzi huo umelenga kutuliza hofu za jumuia ya kimataifa kuhusu kuitishwa uchaguzi huo.Umoja wa Afrika ulioshikilia wagombea wote watatu wasiruhusiwe kupigania kiti cha rais,pamoja pia na Ufaransa na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC,umesema uamuzi huo wa korti ya uchaguzi ni hatua muhimu katika kupatikana masharti yanayohitajika kuitisha uchaguzi wa rais kwa njia za uwazi na kuaminika.
                    

WAANDAMANAJI WATOLEWA MSIKITINI

Majeshi ya usalama ya Misri yameondoa watu katika msikiti mmoja mjini Cairo, baada ya mvutano wa muda mrefu na wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood. Waandamanaji hao waliokuwa ndani wametolewa nje ya msikiti, na wengi wamekamatwa, kwa mujibu wa majeshi ya usalama.Makabiliano katika msikiti wa al-Fath yaliendelea kwa siku nzima, na hata majibizano ya risasi kutokea kati ya majeshi ya usalama wa waandamanaji.
Wakati huohuo Waziri Mkuu wa mpito amependekeza kuvunnja chama cha Brotherhood kwa njia halali. Chama hicho kinamuunga mkono Rais aliyetolewa madarakani Mohammed Morsi, na kinataka arejeshwe madarakani. Licha ya kuhusishwa kwa karibu na serikali ya Bw Morsi, chama cha Brotherhood ni taasisi ambayo imepigwa marufuku. Kilivunjwa rasmi na watawala wa jeshi la Misri mwaka 1954, lakini hivi karibuni kimejiandikisha kama chama kisicho cha kiserikali.

KESI YA HOSNI MUBARAK YAAHIRISHWA TENA

Kesi ya mauaji dhidi ya waandamanaji nchini Misri inayo mkabili rais wa zamani wa taifa hilo Hosni Mubarak imeahirishwa tena hapo jana Jumamosi hadi Agosti 25 baada ya kusikilizwa kwa muda mfupi jijini Cairo. Rais huyo wa zamani mwenuye umri wa miaka 85 ambaye utawala wake uliangushwa tangu mwaka 2011 baada ya kutokea maandano ya wananchi hakuwepo mahakamani wakati wa kuskilizwa kesi hiyo. Hayo yanjiri wakati Chama cha Muslim Bradherhood kimetowa wito kwa wafuasi wake kumiminika kwa wingi leo jumapili kuendeleza harakati za maandamano kuishinikiza serikali ya mapinduzi ilipo kuurejesha utawala wa rais Mohamed Morsi.
Hapo jana vikosi vya polisi vilifaulu kuwatia nguvuni watu 385 wafuasi wa kiongozi huyo alieondolewa madarakani waliokwua wamejificha katika muskiti wa Al Fath jijini Cairo kwa kuhofia kutokea mauaji baada ya vurugu za siku chache zilizo gharimu maisha wa watu 750. Wafuasi hao wa Mohamed Morsi aliepinduliwa na jeshi Julay 3 mwaka huu , wametowa wito kwa mara nyingine tena kuendelea kuandamana. Hata hivyo harakati za maandamao zimeonekana kupungua kasi baada ya hapo jana katika maeneo kadhaa kushuhudiwa utulivu licha ya mikusanyiko ilioonekana jana usiku.

Saturday, August 17, 2013

200 WAHOFIWA KUFA UFILIPINO

Waokoaji nchini Ufilipino wanaendelea kuwatafuta zaidi ya watu 200 wasiojulikana walipo, baada ya feri iliyokuwa imefurika abiria kugongana  na meli ya mizigo wakati wa usiku na kuzama papo kwa hapo. Miili 31 imeopolewa, lakini watu wengine 213 bado hawajulikani walipo, kwa mujibu wa idara ya ulinzi wa mwambao, ambayo imeonya kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa tatu za usiku, na mashuhuda walisema walisikia kishindo kikubwa, na kwamba ndani ya dakika kumi, feri hiyo ilikuwa itayari imezama. Watoto wachanga 58 walikuwa miongoni mwa abiria wa feri hiyo na haijajulikana ni wangapi kati yao wameokolewa. Usafiri wa feri ni maarufu sana katika taifa hilo lililo na visiwa zaidi ya 7,100, na unatumiwa hususani na watu wenye kipato cha chini wasio na uwezo wa kutumia usafiri wa ndege. Wakati ajali hiyo ilipotokea feri hiyo ilikuwa na abiria 870 wakiwemo wafanyakazi.

VIKOSI VYA USALAMA MISRI VYAUZINGIRA MSIKITI

Vikosi vya usalama nchini Misri, vimeuzingira msikiti uliojaa wafuasi wa rais aliepinduliwa Mohammad Mursi mjini Cairo, huku waandamanaji wakipanga maandamano mengine hii leo, baada ya mapigano ya mitaani hapo jana kusababisha vifo vya zaidi ya watu 80.
Kuzingirwa kwa msikiti wa Al-Fatih kumefuatia mapigano makali yaliyosababisha kuuawa kwa watu 83 nchini kote, na kukamatwa kwa wafuasi wengine zaidi ya 1000 wa Rais aliyepinduliwa Muhammad Mursi. Mwandamanaji moja alisema zaidi ya watu 1000 wamekwama katika msikiti huo. Ukandamizaji wa vyombo vya usalama umeigawa Misri zaidi, na kulaaniwa na jamii ya kimataifa.
Ujerumani ilitangaza kusitisha msaada wake kwa Misri, na Kansela Angela Merkel na rais Francois Hollande wa Ufaransa walipendekeza uitishwe mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, ili kuwe na msimamo wa pamoja kuhusiana na hali inayoendelea Misri.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton alisema jana kuwa idadi ya vifo katika siku chache zilizopita inashtua, na kwamba serikali ya muda na uongozi mzima wa kisiasa nchini Misri, wanawajibika kutokana na vifo hivyo.

IRAN YALAANI SHAMBULIO LA BEITUR

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mlipuko wa kigaidi uliotokea jana mjini Beirut Lebanon na kusema Tehran inaungana na familia za wahanga wa tukio hilo katika maafa hayo. Sayyid Abbas Araqchi amesema wananchi wa Lebanon hususan harakati ya mapambano ya nchi hizo watashinda njama hiyo chafu ya Wazayuni na vibaraka wao ya kutaka kuzusha machafuko nchini humo. Umoja wa Mataifa na nchi mbalimbali duniani zimeendelea kulaani vikali mlipuko wa kutegwa ndani ya gari uliotokea jana jioni majira ya saa 12: 15 huko kusini mwa mji mkuu wa Bairut, Lebanon.
Katika mlipuko huo, watu 25 wameripotiwa kuuawa na wengine 200 kujeruhiwa sambamba na kuharibu nyumba magari yaliyokuwa karibu na eneo la tukio. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mlipuko huo na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga.
Nchi mbalimbali duniani ikiwemo Syria, Uturuki, nchi za Ulaya na kadhalika zimelaani vikali shambulizi hilo. Mlipuko huo wa kigaidi. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas mbali na kulaani mripuko huo  wa kusini mwa Bairut, imetaka kudumishwa umoja na mshikamano kati ya makundi yote ya Lebanon mbele ya njama za maadui.

JINA LINALOONGOZA UINGEREZA

Jina la Mtume wa Uislamu, Muhammad (saw) limeongoza kwa kupewa idadi kubwa zaidi ya watoto wa kiume waliozaliwa katika mji mkuu wa Uingereza, London katika mwaka 2012. Jina hilo tukufu limeshika nafasi ya pili kwa kupewa watoto wa kiume waliozaliwa nchini kote Uingereza baada ya jina la Harry.
Idara ya Takwimu ya Taifa yaUingereza imesema jina la Muhammad ndilo lililoongoza kwa kupewa watoto wengi zaidi wa kiume waliozaliwa mjini London katika mwaka uliopita wa 2012. Taarifa ya idara hiyo imesema jina tukufu la Muhammad limetolewa na wazazi kwa watoto elfu 7 na 139 wa kiume waliozaliwa mwaka jana. Jina la Muhammad pia lilisajiliwa kati ya majina mia moja yaliyoongoza mwaka jana katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris na lilipendelewa zaidi na watu katika mji wa Marselle, na Vilevile Oslo nchini Norway.

KATIBU WA UMOJA WA MATAIFA AKOSOA SIASA ZA ISRAEL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  amesema kwamba siasa za ujenzi wa vitongoji vya walowezi za  utawala wa Kizayuni wa Israel zinadhoofisha  jitihada za amani zinazofanywa na jamii ya kimataifa. Ban Ki Moon amesema hayo alipotembelea Ukingo wa Magharibi hapo jana katika mkutano na waandishi habari pamoja na Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa ameeleza kusikitishwa mno na hatua ya Israel ya kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Ukingo wa Magharibi likiwemo eneo la Baitul Muqaddas Mashariki.  Utawala wa Kizayuni wa Israel umejenga vitongoji vingi katika maeneo ya Palestina na kuyafanya makaazi ya walowezi wa Kizayuni suala ambalo ni kinyume cha maazimio ya kimataifa.

BARAZA LA USALAMA LATAKA KUJADILIWA MAUAJI YANAYOENDELEA MISRI

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limefanya mkutano wa dharura kuzungumzia namna vikosi vya usalama vya Misri vilivyowaua wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi na kusema kuna haja ya pande husika kuwa na "uvumilivu wa hali ya juu". Tamko hilo la baraza la usalma linakuja siku moja tu baada ya watu wapatao 638 kuuwawa wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji wafuasi wa Muslim Bortherhood. Waandamaji hao wamekuwa wakitaka Bwana Morsi aliyeondolewa uongozini arudishwe maradaraki. Wakati huo huo rais wa Marekani Barack Obama ameshutumu hatua ya serikali ya muda ya Misri akisema haukuwa na sababu za kutosha.
"tunasikitishwa sana na unyama uliofanyiwa raia wa kawaida " , amesema Obama huku akitangaza kuwa zoezi la kijeshi la pamoja kati ya Marekani na Misri ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika mwezi ujao umefutwa. Rais Obama amesema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili hauwezi kuendelea wakati raia wanauwawa. Licha ya mauaji hayo na umwakikaji mkubwa wa damu ,lakini kikao hicho cha dharura cha umoja wa mataifa kilichoandaliwa mahusus kujadili swala la Misri kilikumbwa na mgawanyiko mkubwa baina ya wanachama 15 wa baraza hilo la Usalama. Wanachama hao 15 walishindwa kuafikiani kuhusu jinsi ya kukabiliana na hali ya Misri, huko jeshi likizidi kukaza kamba.
Kwa kawaida Urusi na China huwa zinapinga hatua yeyote ya baraza la usalama kuingilia maswala ya ndani ya nchi yeyote ile. Hivyo katika kikao hicho cha dharura , Urusi na China hazikibadili msimamo wao wa jadi , bado walipinga kuwa Misri na jeshi lisiingiliwe bali njia ya maridhiano itafutwe. Pengine hii ni kutokana na swala la Chechnya ambalo bado linaisumbua Urusi huko China ikihangaishwa na tatizo la Tibet. Taarifa zinasema China ilikataa katakata kutia saini taarifa rasmi ya baraza la usalama la kulishutumu jeshi la Misri kwa kusababisha umwagikaji wa damu na mauaji.

LIBYA KUSHAMBULIA MELI ZA MAFUTA HARAMU

Waziri Mkuu wa Libya,Ali Zeidan ametishia kutumia nguvu kuwazuia walinzi katika bandari kuu nchini humo dhidi ya kuuza mafuta kwa mashirika ya kibinafsi.Afisa huyo amesema meli yeyote itakayotia nanga katika bandari za Libya bila idhini ya serikali itashambuliwa kwa bomu.Wafanyikazi wa badari wamekua kwenye mgomo wiki kadhaa sasa kulalamikia malipo. Maafisa wamesema mgomo huo umesababisha kupungua kwa mauzo ya mafuta nchini Libya na hivyo kuathiri vibaya uchumi wa nchi.
Waziri Mkuu amesema serikali itatumia nguvu zozote zile kuzuia kile amesema kuvuruga biashara ya mafuta. Banadari zilizoathirika na mgomo ni pamoja na Zeitunia, Brega, Ras Lanouf na Sedra. Uzalishaji wa mafuta Libya ulipungua hadi mapipa laki sita kutoka mapipa milioni moja baada ya kuzuka mapinduzi dhidi ya kiongozi wa zamani Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.

WAFUASI WA MORSI WAZIDI KUUAWA MISRI

Takriban Wafuasi watano wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi na Askari mmoja wa kikosi wa usalam wameuawa hii leo baada ya kutokea mapigano katika miji kadhaa kati ya Waandamanaji na Vikosi vya usalama. Watano waliuawa katika mji wa Ismailiya, huku askari mmoja akiuawa baada ya kituo cha ukaguzi alichokuwamo kuvamiwa na Watu wenye silaha jijini Cairo. Ghasia hizo zilijitokeza wakati Waandamanaji walipoanza maandamano katika miji kadhaa maandamano waliyoyaita Ijumaa ya Ghadhabu. 
 Wafuasi wa Chama cha kiislamu cha Muslim Brotherhood waliitisha maandamano siku ya leo kudhihirisha ghadhabu zao baada ya kuuawa kwa Watu takriban 600 wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vikisambaratisha makambi yaliyowekwa na Wafuasi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Morsi. Wito huu uliongeza hofu ya kuzuka kwa machafuko baada ya yale ya siku ya jumatano hali iliyosababisha Umoja wa Mataifa kukemea Machafuko hayo na kutaka kusitishwa mara moja na pande zote mbili. Hali ya hatari ilitangazwa katika majimbo mengi ya nchini Misri huku kukiripotiwa kuuawa kwa Wanajeshi saba na Askari mmoja kuuawa katika mji wa Assiut. Wizara ya mambo ya ndani ilitoa amri kwa Askari kutumia risasi iwapo majengo ya Serikali yatashambuliwa. Baraza la usalama la umoja wa Mataifa limekemea yanayojiri nchini Misri na kuitisha mkutano wa dharura juu ya Misri, hatua iliyoombwa na Ufaransa, Uingereza na Australia.
 Msemaji wa makundi ya kiislamu yanayomuunga mkono Morsi, Laila Moussa amesema kuwa yamepangwa maandamano nchi nzima hii leo na kuongeza kuwa wafuasi wa Morsi wakiwemo Wabunge wa zamani wamekamatwa wakati wa maandamano . Jijini NewYork Balozi wa Agentina ndanu ya Umoja wa Mataifa, Maria Cristina Perceval, amesema kuwa Wanachama wa Baraza la usalama la umoja wa Mataifa wanasikitishwa na namna ambavyo Wamisri wamekuwa wakipoteza maisha jijini Cairo na kutoa wito wa kufanyika maridhiano ya kitaifa. Jijini Washington, Rais wa Marekani, Barack Obama amesitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Misri kutokana na yanayojiri hivi sasa nchini Misri. Halikadhalika Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa wito kwa Raia wake kutosafiri kwenda Misri na kuwataka Wamarekani walio nchini Misri, kuondoka.

Thursday, August 15, 2013

KAMANDA WA NATO NCHINI AFGHANISTAN ATAKA KUJUA IDADI YA WANAJESHI WATAOBAKI AFGHANISTAN BADA YA 2014

Marekani na Washirika wake wametolewa wito kuwa watangaze ni Wanajeshi wangapi wataendelea kubaki nchini Afghanistani baada ya Mwaka 2014, kamanda wa zamani wa majeshi ya NATO James Stavrisis ameeleza. Stavridis ambaye amemaliza muda wake wa miaka minne akiwa kiongozi wa Majeshi ya NATO amesema ni muhimu kuweka wazi idadi ya Wanajeshi watakaobaki ili kufuta propaganda za kundi la Wanamgambo wa Taliban kuwa majeshi ya nchi za kigeni yanaitelekeza Afghanistani. Kiongozi huyo wa Majeshi ya zamani amesema kuwa anaunga mkono hatua ya Marekani na washirika wake kubakisha wanajeshi 15,000 nchini Afghanistani baada ya Wanajeshi wengine kuondoka nchini humo kabisa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.
 Hivi sasa kuna wanajeshi takriban 100,000 nchini Afghanistani chini ya Mwamvuli wa Majeshi ya kujihami ya nchi za magharibi, NATO, huku Marekani ikiwa na takriban asilimia 60 ya Wanajeshi. Maafisa wa Marekani walipendekeza kubakisha sehemu ndogo ya Jeshi lake nchini humo la Takriban vikosi 8,000 mpaka 12,000 baada ya Mwaka 2014. lakini kutokana na kuwepo kwa hali ya kutoelewana kati ya Kabul na Marekani, Maafisa wa Ikulu ya Marekani walionelea kuwa wawaondoe wanajeshi wote wa Marekani baada ya mwaka 2014.

W/MKUU WA MISRI ARIDHIA MAUAJI YA WANANCHI

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Misri inayoungwa mkono na jeshi ametetea uamuzi wa serikali kushambulia mikusanyiko ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Muhammad Mursi uliosababisha mauaji makubwa ya raia na kusema kwamba serikali haikuwa na chaguo lingine zaidi ya hilo.
Hazem al Beblawi amesema, uamuzi wa kuvunja kambi za waandamanaji haukuwa rahisi lakini jambo hilo limetekelezwa baada ya serikali kujitahidi kusuluhisha na kushindwa. Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya mpito ya Misri Mohammed Ibrahim amesema kuwa, wafuasi wa Muhammad Mursi rais aliyepinduliwa hawataruhusiwa tena kufanya mkusanyiko wowote katika eneo lolote la nchi hiyo. Ibrahim ametoa matamshi hayo baada ya jeshi la Misri jana kutumia nguvu kuvunja mkusanyiko ya wafuasi hao mjini Cairo ambapo mamia ya watu waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
Wakati hayo yakiripotiwa viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin wametiwa mbaroni na askari usalama wa Misri waliposhambulia mikusanyiko ya maelfu ya wafuasi wa Mursi mjini Cairo. Miongoni mwa viongozi hao waliokamatwa ni Muhamed al Beltagy, Essam al Arian, msemaji wa harakati hiyo Ahmed Aref na kiongozi wa kiitikadi wa Ikhwanul Muslimin Abdul Rahim al Bar.

MACHAFUKO YA MISRI NI FAIDA KWA MAREKANI NA ISRAEL

Mbunge mmoja wa ngazi za juu wa Iran amesema hali ya hivi sasa ya ghasia Misri ni kwa maslahi ya Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel. Bw. Allaudin Burujerdi mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali pia mauaji ya raia nchini Misri. Ameongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona nchi muhimu ya Kiislamu kama Misri ikitumbukia katika hali kama hii baada ya harakati ya kimapinduzi ya wananchi ambao waliuondoa utawala wa kidikteta. Burujerdi amesema, baada ya Wamisiri kuutimua madarakani utawala kibaraka wa Hosni Mubarak, hivi sasa Marekani na Utawala wa Kizayuni zinachochea machafuko Misri na jambo hilo linatia wasi wasi kwani yamkini nchi hiyo ikatumbukia katika vita vya ndani baina ya serikali ya mpito na harakati ya Ikhwanul Muslimin. Mbunge huyo mwandamizi wa Iran ametoa wito kwa wanasiasa, wasomi na wanazuoni Misri kutumia busara ili kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa sasa.

HIZBULLAH YATHIBITISHA KUWASHAMBULIA WANAJESHI WA ISRAEL

Harakati ya Hizbullah imesema ndiyo iliyohusika na milipuko iliyowajeruhi wanajeshi wanne wa utawala haramu wa Israel ambao walikuwa wamepenya na kuingia kusini mwa Lebanon.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen yenye makao yake Beirut, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrullah amesema Hizbullah haitauruhusu utawala haramu wa Israel ukiuke ardhi ya Lebanon.
Ikumbukwe kuwa mnamo Agosti 7 milipuko miwili iliwajeruhi wanajeshi vamizi wa Israel ambao walikuwa wameingia mita 400 ndani ya ardhi ya Lebanon katika eneo la kusini. Sayyed Nasrallah amesema, ‘Hizbullah ilikuwa na taarifa za mapema kuwa wanajeshi wa Israel walikuwa wamepanga kuingia kusini mwa Lebanon na hivyo harakati hiyo ilitega mabomu ambayo yalilipuliwa kutokea mbali wakati wanajeshi hao wa Israel walipofika hapo.’ Kufuatia milipuko hiyo jeshi la Lebanon lilitoa taarifa na kusema uingiaji huo wa askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni ‘ukiukaji wa mamlaka ya Lebanon’.

KEITA ASHINDA DURU YA PILI YA UCHAGUZI MALI

Serikali ya Mali imetangaza kuwa, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa rais kwa kujipatia asilimia 78 ya kura. Serikali pia imesema idadi jumla ya waliopiga kura ilipungua kutoka asilimia 49 kwenye duru ya kwanza hadi asilimia 46 kwenye duru ya pili. Keita alipata uungaji mkono kutoka kwa wagombea 22 kati ya 25 aliowashinda kwenye duru ya kwanza. Weledi wa mambo wanasema ushindi huo mnono aliopata Keita ni kibali rasmi kutoka kwa wananchi cha kufanya mazungumzo na waasi wa kaskazini ili kutatua mgogoro ulioko kwa njia ya amani. Keita anakabiliwa na changamoto chungu nzima lakini kubwa zaidi ni jinsi ya kulikarabati jeshi la nchi hiyo ambalo mwaka uliopita lilimpindua rais Amadou Toumane Toure. Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema ataunda serikali yenye sura ya kitaifa itakayowaleta pamoja wananchi wote wa Mali.

CAIRO KIMYA BAADA YA VIFO

Mji mkuu wa Misri Cairo umeripotiwa kuwa kimya, baada ya operesheni ya kinyama dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi kupelekea vifo vya mamia ya raia. Mauaji hayo yamezua shutuma kutoka jamii ya kimataifa. Zaidi ya watu 278 waliuwawa wakati maafisa wa usalama waliposhambulia kambi mbili za wafuasi wa Bwana Morsi. Kambi hizo zilianzishwa mwezi uliopita kupinga hatua ya jeshi kumng'oa rais huyo anayezingatia itikadi za kiislamu. Hali ya hatari imetangazwa na amri ya kutotoka nje nyakati za usiku kutolewa katika miji mikuu ya Misri. Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani John Kerry amesema matukio ''mabaya'' yaliyotokea ni ''pigo kubwa kwa juhudi za maridhiano''.
Afisa wa mashauri ya kigeni katika Muungano wa Ulaya, EU, Catherine Ashton na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kadhalika wamekosoa hatua ya maafisa wa usalama kutumia nguvu dhidi ya raia.
Raia wa Misri wanaamkia siku nyingine yenye shaka juu ya mustakabal wao, anasema mwandishi wa BBC Bethany Bell aliyepo mjini Cairo. Hata baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa Alhamisi asubuhi, kumekuwa na magari machache katika barabara za katikati mwa Cairo na madaraja yanayovuka mto Nile, anasema mwandishi wetu.

MAKAO MAKUU YA GAVANA NCHINI MISRI YACHOMWA MOTO

Rais Barack Obama  wa  Marekani  ametoa  taarifa kuhusiana  na  hali  nchini  Misri  baada  ya jeshi  nchini humo  kuwaondoa  kwa  nguvu  waandamanaji  mjini  Cairo jana. Obama  amesema  kuwa  anasitisha  ushirikiano  wa kijeshi ambapo  majeshi  ya  nchi  hizo  yalitarajiwa kufanya  mazoezi  ya  pamoja  mwezi  huu. Pia Obama amesema Wamisri  hawapaswi  kuilaumu Marekani kwa kile  kinachotokea  nchini  humo.
Wakati huo  huo waandamanaji  kutoka makundi  ya Kiislamu  nchini  Misri wamevamia  makao  makuu  ya gavana  mjini  Cairo  leo na kuchoma  moto jengo hilo. Kituo cha binafsi cha televisheni cha CBC kimeonesha picha za makao makuu hayo yakiwaka moto wakati  wazima moto wakijaribu kuuzima moto huo.
Nao maafisa  nchini  Misri  wamesema kuwa  idadi  ya  watu waliouawa  katika mapambano  kati  ya  polisi  na waandamanaji wanaomuunga  mkono  rais aliyeondolewa madarakani  Mohammed Mursi  imefikia  zaidi ya watu 525.

Monday, August 12, 2013

BAKWATA NAO WATAKA UCHUNGUZI DHIDI YA KUSHAMBULIA SHEIKH PONDA

Baraza la waislamu Tanzania limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kiislamu za kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililopelekea kupigwa risasasi kwa mhubiri Sheikh Issa Ponda. Taarifa imetolewa na kaimu mufti wa Tanzania Al Had Musa Salum. Pamoja ya kwamba (BAKWATA) limekuwa likipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es Salaam, Baruan Muhuza, sheikh Ponda ambaye amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali alipigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa hadhara wa baraza la sikukuu ya Idd el Fitr. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania. Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Msemaji wa Jeshi la polisi Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini. Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200. Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.

ISRAEL YAZIDI KUJENGA MAENEO YA WAPALESTINA

Serikali ya Israel imeidhinisha ujenzi wa nyumba mpya zaidi ya 1,000 katika makaazi ya Wayahudi kwenye maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa na Israel.Waziri wa Makaazi wa Israel, Uri Ariel, alisema nyumba hizo zitajengwa Ufukwe wa Magharibi na masahriki mwa Jerusalem ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Israel. Tangazo hilo limetolewa siku tatu kabla ya mazungumzo ya amani baina ya Israel na Wapalestina kuanza tena mjini Jerusalem. Waziri wa Makaazi wa Israel ametoa idhini ya mwisho kujenga karibu fleti 1,200 katika maeneo yenye makaazi ya Wayahudi, siku tatu tu kabla ya mazungumzo ya amani kati ya Israeli na Palestinian kuanza tena.
Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, alishikilia kwa muda mrefu kwamba hatarejea kwenye mazungumzo bila ya Israel kusitisha kujenga makaazi mepya kwenye maeneo inayoyakalia. Lakini hatimaye alikubali kushiriki katika mzungumzo baada ya Israel kusema kuwa itawaachilia huru wafungwa wengi wa Kipalestina.
Makaazi ya Wayahudi katika Ufukwe wa Magharibi ndio swala kubwa linalokwamisha mazungumzo. Makaazi hayo yanaonekana kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa, ingawa Israel inapinga hilo.

WAFUASI WA MURSI BADI WAENDELEZA MAANDAMANO

Wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi wameweka kambi jijini Cairo na pia wamekuwa wakifanya maandamano kila siku nchini Misri kukemea mapinduzi yaliyofanywa dhidi ya morsi tarehe 3 mwezi Julai. Viongozi wa Serikali ya mpito iliyowekwa madarakani na Jeshi la nchi hiyo wamekuwa wakiwaonya Waandamanaji kuondosha kambi zao, lakini pia kukiahidi Chama cha Muslim Brotherhood kutafuta suluhu ya mgogoro wao iwapo watasitisha maandamano. Takriban watu 250 wameuawa tangu kuangushwa kwa Morsi na kushikiliwa, Mamlaka zikisema kuwa wana nia ya kuepuka vitendo vya umwagaji damu. Lakini wafuasi wa Morsi wameitisha Maandamano makubwa siku ya jumanne kushinikiza kurejeshwa madarakani kwa Morsi na kulikemea Jeshi la nchi hiyo.
 Kiongozi ndani ya Chama cha Muslim Brotherhood amesisitiza kuwa wanataka kutuma ujumbe kwa Viongozi wa mapinduzi nchini humo kuwa Watu wa Misri watajitokeza katika maeneo mbalimbali nchini humo. Hivi sasa nchini humo kunafanyika jitihada za kufanya mazungumzo ili kupatikana suluhu ya kisiasa, mazungumzo ambayo yanaelezwa kuwa huenda yasipokelewe na Chama cha Muslim Brotherhood. Utawala wa mpito nchini Misri umeweka mpango wa kuelekea mabadiliko uya nchini humo ambao umetangaza kufanyika kwa uchaguzi mpya mwaka 2014, na kutoa mwanya kwa Muslim Brotherhood kushiriki katika mabadiliko hayo.Jitihada mbalimbali zimefanyika ikiwemo kufika jijini Cairo kwa Wajumbe toka nchini Marekani,Umoja wa Ulaya, na nchi za kiarabu kwa lengo la kumaliza mzozo wa kisiaasa lakini jitihada zao hazikuzaa matunda.

ZAIDI YA WATU 60 WAUAWA KATIKA MRIPUKO BAGHDAD

Watu zaidi ya sitini wameuawa na wengine zaidi ya mia mbili kujeruhiwa katika mfululizo wa milipuko ya mabomu ya kutegwa kwenye magari katika mji mkuu wa Iraq Baghdad, mashambulizi hayo yametekelezwa wakati waumini wa dini ya kiislamu wakiendelea kusherehekea sikukuu ya Eid el-Fitr. Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya mashambulizi nchini humo ambapo watu zaidi ya mia nane wameripotiwa kuuawa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani pekee.
 Takwimu zaidi juu ya mauaji ya nchini humo zinasema kuwa watu zaidi ya elfu tatu wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Vikosi vya usalama vimekuwa katika jitihada za kupambana na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al Qaeda linalotajwa kuratibu mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya serikali, vikosi vya kigeni na raia. Hivi karibuni Marekani ilitangaza donge nono la dola milioni kumi kwa yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa kiongozi wa kundi hilo Abu Bakr a-Baghdadi ambaye inaaminiwa yuko nchini Syria.

ISRAEL YASEMA HIZBULLAH WANAPATA UZOEFU TOKA SYRIA

Kamanda mmoja wa jeshi la utawala haramu wa Israel amesema kuwa, hatua ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuingia katika mapambano na makundi ya kigaidi nchini Syria inawafanya wapiganaji wa harakati hiyo wajinoe zaidi kwa ajili ya kukabiliana na Israel.
Yaron Formosa amedai kuwa, hatua ya Hizbullah kuingia katika vita dhidi ya magaidi nchini Syria si kwamba itadhoofisha uwezo wa harakati hiyo, bali kutazidisha maradufu uzoefu wake katika kupambana na Israel. Yaron ameongeza kuwa, Hizbullah inafuatilia kwa karibu sana harakati zote za jeshi la utawala wa Israel katika mipaka ya Lebanon. Amezidi kuongeza kuwa, wapiganaji wa harakati hiyo, wamejipatia uzoefu mkubwa wa kutumia silaha za aina mbalimbali huko nchini Syria, suala ambalo linaitia wasiwasi mkubwa Israel.

MZAZI WA SNOWDERN AMKOSOA OBAMA

Baba wa jasusi wa zamani wa Marekani, Edward Snowden amesema kuwa, Rais Barack Obama wa Marekani anaipotosha jamii ya nchi hiyo.
Lon Snowden ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la ABC na kusisitiza kuwa, matamshi ya Obama yaliyojengeka juu ya kuweka sheria za kuwalinda wafichua siri za nchi hiyo mfano wa Snowden, yako mbali na ukweli wa mambo, au yanapingana na washauri wake au yana lengo la kuipotosha jamii ya Wamarekani.
Siku ya Ijumaa iliyopita Rais Barack Obama wa Marekani aliwambia waandishi wa habari kuwa, kabla ya jasusi huyo kufichua siri, alikuwa amekwishatia saini muswada wa kuwalinda wafichuaji siri za nchi hiyo. Kwa upande mwingine Lon amevituhumu vyombo vya usalama na vya sheria vya Marekani akisema haviwezi kumhukumu kwa uadilifu mwanaye.

W/MKUU WA PALESTINA ASEMA HAKUNA FAIDA MAZUNGUMZO NA ISRAEL

Waziri Mkuu wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina amesema kuwa, kuanza tena mazungumzo ya mapatano baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel hakuna faida yoyote ile. Ismail Hania amesisitiza kuwa, mazungumzo hayo yatapelekea kuongezeka ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina. Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina inayoongozwa na HAMAS amesisitizia udharura wa kutekelezwa maridhiano ya kitaifa ya Palestina na kuongeza kwamba, serikali ya Hamas inapinga kuweko mazungumzo hayo kwani hayana faida yoyote ile kwa Wapalestina. Hayo yanajiri katika hali ambayo, makundi ya mapambano ya Palestina yameendelea kusisitiza kwamba, kuanza mazungumzo eti ya mapatano yameufanya mwenendo wa utekelezaji makubaliano ya maridhiano ya kitaifa kuwa mgumu zaidi.

KURA ZAANZA KUHESABIWA MALI

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa duru ya pili ya uchaguzi wa Rais uliofanya hapo jana nchini Mali limeanza huku wananchi wa nchi hiyo wakiwa na matumaini kwamba, Rais ajaye ataleta uthabiti katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika. Mamilioni ya wananchi wa Mali jana walishiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa Rais baada ya duru ya kwanza kukosa kutoa mshindi. Waangalizi wa uchaguzi wa Mali wamesema kuwa, uchaguzi wa jana ulikuwa huru na wa haki. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Mali yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha siku mbili au tatu tangu kufanyika uchaguzi huo na Mahakama ya Katiba ina muda wa hadi kufikia siku ya Ijumaa kuthibitisha matokeo hayo. Weledi wa mambo wanasema kuwa, Rais ajaye nchini Mali kati ya Ibrahim Keita au Soumaila Cisse, atakuwa na majukumu makubwa na mazito zaidi, hasa kwa kuzingatia mgogoro na matatizo chungu nzima yanayoikabili nchi hiyo.

Friday, August 09, 2013

MARUBANI WA UTURUKI WATEJWA NYARA

Watu waliokuwa na  silaha leo wamewateka nyara marubani wawili wa ndege kutoka Uturuki,  kwenye njia ya uwanja wa ndege wa Beirut. Waziri wa  ndani wa Lebanon Marwan Charbel aliliambia Shirika la habari la AFP kwamba tukio hilo lilitokea mapema alfajiri wakati wahudumu wa shirika la ndege la Uturuki walipokuwa wakielekea uwanja wa ndege kutoka hoteli. Duru zinasema watu wanne waliokuwa na silaha walihusika. Waziri Charbel alisema amezungumza na  balozi wa Uturuki nchini Lebanon na kwamba uchunguzi umeanza, ikiwa ni pamoja na kumhoji dereva wa basi. Utekaji nyara huo unaaminiwa kuwa tukio linalohusiana na kutekwa nyara nchini Syria  kwa  Walebanon 9 wa madhebu ya shia  mwezi Mei mwaka jana.

AMNESTY YAITAKA ETHIOPIA KUTOWAKANDAMIZA WAISLAM

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limeitaka serikali ya Ethiopia iache kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo. Taarifa ya Amnesty International iliyotolewa hapo jana imeitaka serikali ya Ethiopia iache vitendo vya kuwakandamiza Waislamu. Aidha taarifa hiyo imesema, serikali ya Ethiopia inapaswa kukomesha vitendo vya kukandamiza maandamano ya amani ya Waislamu wa nchi hiyo. Maandamano karibu yote yaliyofanywa na Waislamu wa Ethiopia katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu yalikuwa ya amani lakini vikosi vya usalama vya nchi hiyo vilitumia mkono wa chuma kuzima baadhi ya maandamano hayo, imebainisha taarifa ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International. Taarifa ya Amnesty International imekuja masaa machache tu baada ya Waislamu wa Ethiopia kuandamana jana baada ya Sala ya Eid ul Fitri wakipinga hatua ya serikali ya kuingilia mambo yao. Kwa siku kadhaa sasa mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa umekuwa ukishuhudia maandamano makubwa ya Waislamu wakilalamikia kitendo cha kuuawa Sheikh Nuru Yimam Muhammad aliyepigwa risasi wakati akitoka msikitini katika jimbo la Amhara, nchini humo. Sheikh Nuru Yimam alikuwa mmoja wa wanaharakati wakubwa wa Kiislamu nchini Ethiopia.

PALESTINA YAIOMBA MISRI KUFUNGUA KIVUKO CHA RAFAH

Ismail Hania, Waziri Mkuu wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina amewaomba viongozi wa serikali ya Misri wakifungue tena kivuko cha Rafah kilichoko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Ukanda wa Gaza wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Hania alitoa wito huo katika hotuba za Sala ya Idil Fitri iliyosaliwa jana huko Gaza na kuwataka viongozi wa Misri wakifungue tena kivuko hicho kwa ajili ya Wapalestina ili wananchi hao madhulumu waweze kuingia na kutoka kirahisi na pia kuwepesisha uingizaji wa bidhaa zinazohitajika huko Gaza. Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali halali ya Palestina yenye makao yake huko Ukanda wa Gaza ilitahadharisha juu ya kutokea maafa ya kibinadamu katika eneo hilo kutokana na mzingiro uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwaka 2007. Naye Muhammad al Katri, afisa mwanadamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Wapalestina wa Gaza hususan wagonjwa wanashindwa kufuatilia matibabu yao nje ya Palestina kutokana na kufungwa mara kwa mara kivuko cha Rafah na kwamba wagonjwa wanaohitaji kupelekwa ng'ambo kwa matibabu wanakabiliwa na hatari ya kifo. Ameongeza kuwa vizuizi katika kivuko cha Rafah vimeshadidishwa na serikali ya Misri tangu rais wa nchi hiyo Muhammad Morsi alipong'olewa madarakani.
Wakati huohuo jumuiya na taasisi za masuala ya sheria huko Ukanda wa Gaza zimetoa taarifa zikitahadharisha kwamba kufungwa kivuko cha Rafah katika mpaka wa pamoja wa Misri na Ukanda wa Gaza kumesababisha matatizo mengi kwa eneo hilo. Jumuiya hizo zimesema kuendelea mzingiro dhidi ya Gaza na kufungwa vivuko vya kuingilia na kutokea katika eneo hilo kunakiuka sheria za kimataifa, na zimezitaka jumuiya za kimataifa zifanye juhudi kuhakikisha mzingiro uliowekwa dhidi ya Gaza unaondolewa. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kwa upande wake imeikosoa serikali ya Misri kutokana na vizuizi vikali inavyowawekea Wapalestina. Katika ripoti yake, OIC imesema matukio ya hivi karibuni nchini Misri yamekuwa na taathira mbaya mno kwa maisha ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza na kuwataka viongozi wa Cairo wachukue hatua za lazima kuhusiana na kivuko cha mpakani cha Rafah ili kupunguza mateso na machungu wanayopata Wapalestina.
 Kwa sasa kuna wasafiri wapatao 250 wanaopita kwenye kivuko cha Rafah kwa siku ambapo kabla ya matukio ya hivi karibuni nchini Misri, idadi hiyo ilikuwa ikifikia watu elfu moja. Hadi sasa zaidi ya Waplestina 460 wameshafariki dunia kutokana na uhaba wa dawa na vifaa vya tiba uliosababishwa na mzingiro wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza, na hivi sasa maisha ya mamia ya wagonjwa wengine wa Kipalestina yako hatarini kutokana na hali hiyo. Kutokana na kuvurugika hali ya mambo nchini Misri baada ya kung'olewa madarakani rais wa nchi hiyo Muhammad Morsi, kivuko cha Rafah ambayo ndiyo njia pekee ya kuingilia na kutokea Wapalestina wa Gaza imefungwa rasmi na huwa inafunguliwa kwa muda tu katika siku makhsusi

JANGA LA KIBINADAMU LAINYEMELEA GAZA

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS Fawzi Barhoum amesema kuwa, eneo la Ukanda wa Gaza ambalo linakabiliwa na mzingiro, linanyemelewa na janga la kibinaadamu. Afisa huyo mwandamizi wa Chama cha Hamas ametahadharisha kwamba, hali ya kibinaadamu huko Gaza ni mbaya mno na kuna uwezekano wa eneo hilo kukumbwa na maafa ya kibinaadamu.  Amesema kuwa, kushadidi mzingiro huo unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kufungwa vivuko vya kuelekea katika eneo hilo, kikiwemo kivuko cha Rafah kinachopakana na Misri kumelifanya eneo hilo kukabiliwa na hali mbaya mno huku wakazi wa eneo hilo wakishindwa kujidhaminia baadhi ya mahitaji yao muhimu kama chakula. Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametahadharisha kwamba, endapo hakutachukuliwa hatua za haraka za kuhitimisha mzingiro huo, basi yamkini eneo la Ukanda wa Gaza likakabiliwa na maafa ya kibinaadamu.

WITO WATOLEWA KWA MISRI

Marekani na Muungano wa Ulaya wamezitaka pande zote katika mgogoro wa kisiasa wa Misri, kumaliza mzozo wao unaosemekana kuwa hatari kwa taifa hilo. Hii ni baada ya serikali ya mpito kusema kuwa juhudi za mapatano zimekosa kufua dafu.Katika taarifa yao ya pamoja, walisema kuwa serikali ya Misri ndio ina jukumu kubwa kuanzisha mazungumzo na kuhakikisha kuwa mchakato huo unafanikiwa. Serikali ya mpito inayoungwa mkono na Jeshi, imesema kuwa jeshi litalazimika kuvunja mkusanyiko wa wafuasi wa Morsi ambao wamepiga kambi mjini Cairo wakitaka aachiliwe.
Mamia ya watu wamefariki tangu kuanza kwa vurugu zilizofuata kuondolewa mamlakani kwa Morsi tarehe 3 mwezi Julai. Tangu hapo, wanadiplomasia kutoka Marekani, Muungano wa Ulaya na Milki za kiarabu, wote wamejaribu kusuluhisha mgogoro huo. Lakini siku ya Jumatano rais wa mpito Adly Mansour alitangaza kuwa juhudi za kidiplomasia zimekosa kufaulu na hivyo kusema kuwa mazungumzo yaliisha hiyo jana.
''Juhudi hizi hazijaweza kuafikia lolote,'' ilisema taarifa ya rais. Rais alisema kuwa analilaumu vuguvugu la Muslim Brotherhood ambalo linamuunga mkono Morsi kwa kuwa sababu ya kukosa kufaulu kwa mazungumzo.

ALSHABAB YAWAACHILIA WAKENYA

Siku mbili baada ya kuachiliwa huru na wapiganaji wa kiislamu wa Al Shabab, Yese Mule na Fredrick Wainana, hatimaye wamekutana na familia zao.Wawili hao wamekuwa chini ya ulinzi wa maafisa wa usalama wa Kenya. Maafisa hao wawili wa serikali, walitekwa nyara zaidi ya mwaka mmoja na nusu uliopita wakati waasi walishambulia kituo cha polisi katika eneo la Wajir, Kaskazini mwa Kenya.Mule aliambia BBC kuwa walihamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine mara 19 huku wakiwa wamefungwa kwa minyororo na kufumbw macho wakiwa nchini Somalia wakati wote walipokuwa wametekwa nyara. Serikali ya Kenya imekanusha madai kuwa ililipa kikombozi kwa wawili hao kuachiliwa.
Al-Shabab limewateka nyara raia wa kigeni ikiwemo aliyekuwa jasusi wa Ufaransa Denis Allex aliyeuawa mwezi Januari baada ya njama ya kumuokoa kutibuka mwezi mapema mwaka huu. Bwana Mule na mwenzake Wainana, walitekwa nyara miezi mitatu baada ya jeshi la Kenya kuingia nchini Somalia kusaidia nchi hiyo kupambana na kundi la Al Shabaab. Wanajeshi wake ni sehemu ya kikosi cha muungano wa Afrika kinachosaidia serikali ya Somalia inayoungwa mkono na umoja wa mataifa dhidi ya Al shabaab.
Bwana Mule alikuwa afisaa wa wilaya ya Garisa wakati bwana Wainana akiwa karani wa serikali walipotekwa nyara na karibu wapiganaji 100 wa al-Shabab katika kambi ya polisi eneo la Gerille, mji unaopakana na Somalia. Wakenya wanane waliuawa wakati wa utekaji nayara huo.

NDEGE YA KIJESHI YALIPUKA MOGADISHU

Ndege ya kijeshi imelipuka na kuteketea nchini Somalia baada ya kutua kwa dharura katika uwanja wa kimataifa wa ndege mjini Mogadishu. Kikosi cha muungano wa Afrika nchini Somalia ambacho kina kambi yake katika uwanja huo wa ndege kimesema kuwa wanajeshi wake kadhaa wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa.Inasemekana kuwa ndege hiyo ilikuwa ya jeshi la Ethiopia. Kuna ripoti kuwa ndege ilikuwa imebeba zana za kivita.
Wafanyakazi katika uwanja huo wa ndege walielezea kusikia milipuko kadhaa huku moto ukienea kwa ndege hiyo. Ndege za kijeshi hutua katika uwanja huo wa ndege unaotumiwa na wanajeshi wa muungano wa Afrika wanaopambana dhidi ya wapiganaji wa Al shabaab wanaosemekana kuwa na uhusiano na al Qaeda.
Wakati huohuo, kwenye mtandao wao wa Twitter kundi la Al Shabaab limeeleza kufurahia kwa kulipuka kwa ndege hiyo hasa kwa kuwa ililipuka yenyewe.
Kwenye ujumbe mwingine , kundi hilo lilisema kuwa ndege hiyo iliyokuwa imebeba silaha iliteketea katika uwanja wa Mogadishu na kuharibu kila kilichokuwa kwenye ndege yenyewe. Kundi hilo lililaumu ilichokiita watu waliolaaniwa kwa kupanga mauaji ya waumini na kufanya uharibifu lakini kila wanachokifanya, juhudi zao zinagonga mwamba.

WAFUASI WA MURSI WAAPA KUTOTAWANYIKA MAENEO WALIYOPO

Wafuasi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Misri, Mohamed Morsi wamesherekea sikukuu ya Eid al-Fitr wakiwa kwenye maeneo wanayoyakalia huku wakiapa kutoondoka licha ya tangazo la Serikali. Usiku wa kuamkia leo maelfu ya wafuasi wa Muslim Brotherhood walionekana kusherekea kwenye viwanja vya mjini Cairo jirani na chuo kikuu cha Cairo wakiimba nyimbo za kukashifu utawala wa kijeshi. Hapo jana mara baada ya sala, wafuasi wa Morsi waliokuwa kwenye uwanja wa Rabaa al-Adawiya walisikika wakiapa kuendelea kusalia kwenye viwanja hivyo licha ya tangazo la Serikali linalowataka kuondoka kwenye maeneo hayo.
Hofu ya kiusalama imeendelea kutanda nchini Misri huku mataifa ya magharibi yakieleza hofu yao kuhusu kuendelea kwa mvutano wa kisiasa kati ya wafuasi wa Morsi na wale wanaounga mkono Serikali ya mpito. Nchi ya Iran imeeleza hofu ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa maandamano kati ya wafuasi wanaomuunga mkono rais Morsi na wale wanaiunga mkono Serikali.

DOLA ELFU 6 KWA ATAYESAIDIA KUKAMATWA WALIOWAMWAGIA TINDIKALI WATALII

Polisi visiwani Zanzibar nchini Tanzania wametangaza donge nono la dola elfu 6170 sawa na paundi za Uingereza elfu 3971 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kuwamwagia tindi kali raia wawili wa Uingereza. Hapo jana jeshi la Polisi lilitangaza kuanza msako mkali visiwani humo kuwasaka watuhumiwa tukio hilo ambapo tangazo la donge nono linakuja wakati ambapo rais wa Jamuhuru Jakaya Kikwete akitaka waliohusika kusakwa popote walipo. Hapo jana rais Jakaya Kikwete aliwatembelea rais hao, Kirstie Trup na Katie Gee ambao walikuwa wamelazwa kwenye hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam ambako walisafirishwa kutokea Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kuwaona wasichana hao, rais Kikwete alisema tukio hilo limechafua sifa ya nchi ya Tanzania na kuliita ni laaibu kwakuwa ni nadra sana kwa wananchi wa Tanzania kutekeleza vitendo kama hivi. Kwa mujibu wa taarofa iliyotolewa na familia ya wasichana hao, imesema kuwa inalaani shambulio hilo baya kutekelezwa dhidi ya watoto wao ambao hawakuwa na hatia na kuwashukuru wanahabari na Serikali kwa ushirikiano waliouonesha. Wote wawili wamesafirishwa kwenda nchini Uingereza usiku wa jana kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Polisi, imesema kuwa wasichana hao wanaodaiwa kuwa na umri wa miaka 18 walimwagiwa tindi kali na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki kwenye mji Mkongwe wa Zanzibar na kisha watu hao kutokomea kusikojulikana. Polisi wanasema mpaka sasa hawajabaini sababu za watu hao kutekeleza shambulio hili dhidi ya raia wa kigeni na kwamba uchunguzi unaendelea na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kusaidia kuwakamata watu hao.

Wednesday, August 07, 2013

MAMBO MATATU YANAYOFUATA BAADA YA RAMADHAN

Tunakaribia kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan na mambo matatu yafuatayo ya muhimu yanayotukabili yanapasa kuzingatiwa ili tukamilishe Swawm zetu ipasavyo na tupate fadhila zake.

1- ZAKAATUL-FITWR  
Inaitwa Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana na kumalizika Swawm ya Ramadhaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika mwezi wa Ramadhaan.

 Hikmah Yake
Ni kutwaharisha Swawm ya Muislamu kutokana na maneno machafu, ya upuuzi wakati alipokuwa amefunga kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya ‘Iyd. Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود  بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .
Kutoka Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni twahaara ya mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalah basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalah basi hiyo ni miongoni mwa sadaka” [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].

WAFANYAKAZI WA BALOZI ZA MAREKANI NA UONGEREZA WAONDOLEWA YEMEN

Marekani na Uingereza zimewaondoa wafanyikazi wake wa balozi zao kutoka mjini Sana'a nchini Yemen kufuatia hofu ya kufanywa kwa shambulizi la kigaidi.Hatari hiyo kubwa ya shambulizi linaloaminika kupangwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda pia imesababisha kufungwa kwa muda kwa balozi 19 mashariki ya kati na nchi kadhaa za Afrika.Hii inakuja baada ya Marekani wiki iliyopita kutoa tahadhari kote ulimwenguni kuhusu tisho la kigaidi.Ubalozi wa Ujerumani nchini Yemen pia umefungwa kwa muda kutokana na sababu hizo za kiusalama.Yemen imeimarisha usalama wake katika mitaa ya mji mkuu Sana'a.Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imesema wanamgambo walikuwa wamepanga kushambulia ofisi na mashirika ya kigeni.Shambulio lililofanywa na ndege za Marekani zisizoendeshwa na marubani nchini Yemen hapo jana ziliwaua watu wanne wanaodaiwa kuwa wanachama wa Al Qaeda.Rais Obama amesema tisho hilo ni kubwa mno kiasi ya kuifanya Marekani kuchukua kila tahadhari.

JUHUDI ZA KIDIPLOMASIA ZAKWAMA MISRI

Juhudi za wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi na Uarabuni kumaliza msuguano wa kisiasa kati ya serikali ya mpito nchini Misri na wafuasi wa chama cha kiislam cha Muslim Brotherhood zimeshindwa, ofisi ya raisi imesema leo Jumatano. Taarifa hiyo inaona kuwa kwa sasa serikali inaweza kuanzisha harakati dhidi ya wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi, hatua ambayo jumuiya ya kimataifa inahofu kuwa inaweza kusababisha umwagaji damu zaidi.
Maseneta wa Marekani John McCain na Lindsey Graham ambao wamekuwa nchini Misri kujaribu kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo wamesema umwagaji damu huenda ukashuhudiwa nchini humo ikiwa suluhu la kudumu halitapatikana nchini humo na viongiozi wa Muslim Brotherhood wanaozuiliwa kuachiliwa huru. Duru zinasema kuwa wasuluhishi hao walishindwa kuafikiana na serikali ya mpito chini ya rais Adly Mansour ambaye amesema hatakubali mataifa ya kigeni kuingilia masuala yao.
Serikali ya mpito inaendelea kushikilia msimamo kuwa chama cha Muslim Brotherhood kinawajibika kwa kushindikana kwa juhudi hizi, na kwa ajili ya matukio yanayohusiana na ukiukwaji wa sheria na kuhatarisha usalama wa umma.

MAWASILIANO YA VIONGOZI WA ALQAEDA NA MAREKANI KUFUNGWA


Imebanika kuwa mawasiliano kati ya viongozi wakuu wa Al Qeada akiwemo Ayman al-Zawahiri kiongozi wa kundi hilo yalisababisha Marekani kuamua kufunga balozi zake Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kuanzia siku ya Jumapili iliyopita. Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa shirika la Ujasusi nchini humo lilifanikiwa kunasa mawasiliano hayo kabla ya hatua kuchukuliwa.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jayne Carney amesema kuwa walichukuwa hatua hiyo kuwalimda raia wake dhgidi ya magaidi hao ambao wameendelea kuwasaka. Mbali na Mashariki na ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Balozi za Marekani nchini Mauritiuys, Madagascar, Bunjumbura Burundi na Kigali Rwanda pia zimefungwa.

MAWAZIRI WA MAMBO YA KIGENI NA USALAMA WA URUSI NA MAREKANI KUKUTANA

Mawaziri wa mambo ya kigeni na masuala ya ulinzi kutoka mataifa ya Marekani na Urusi wanatarajia kukutana Ijumaa hii huko Washington Marekani kufuatia mvutano unaozidi baada ya serikali ya Moscow kumpatia hifadhi mfanyakazi wa zamani wa shirika la kijasusi nchini Marekani, Edward Snowden. Maafisa nchini marekani wamearifu kuwa mkutano huo utawakutanisha waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na wa masuala ya usalama Chuck Hagel, na wale wa Urusi Sergei Lavrov na Sergei Shoigu.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani imesema kufuatia hoja ya Snowden Marekani inatathimini upya manufaa ya mkutano uliopangwa kuwakutanisha Rais wa marekani Barack Obama na wa Urusi Vladimir Putin mapema mwezi Septemba. Ikulu ya Marekani imebainisha pia miongoni mwa agenda zitakazojadiliwa katika mkutano wa viongozi hao kuwa ni hali ya mambo nchini Syria mpango wa kukomesha silaha za nyuklia,vilevile Afghanstan na Iran.


MAELFU WAANDAMANA KUPINGA SERIKALI YA TUNISIA

Maelfu ya waandamanaji wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Tunisia,Tunis, kutaka serikali inayoongozwa na wanasiasa wa kiisilamu kujiuzulu. Ni maandamano makubwa zaidi kutokea tangu mgogoro wa hivi karibuni wa kisiasa kuanza wiki mbili zilizopita kufuatia mauaji ya mwanasiasa mashuhuri Mapema baraza la kikatiba lilihirisha kazi yake hadi serikali na upinzani zitakapoanza mazungumzo. Baraza hilo linaandika katiba mpya ya nchi.
Maandamano hayo yaliitishwa na upinzani unaotaka baraza la kikatiba kuvunjiliwa mbali pamoja na serikali kujizulu na kuadhimisha miezi sita ya mauaji ya kiongozi mashuhuri wa upinzani Chokri Belaid. Chama cha kitaifa chenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia ndicho kiliitisha maandamano ya wanachama wake laki sita kikiwataka kujiunga na maandamano ya wananchi. "watu wanataka utawala huu kuondolewa,'' walisema waandamanaji. Msemaji wa baraza la kikatiba, Mustapha Ben Jaafar, alisema kuwa kazi itaendelea kuhakikisha kuwa katiba mpya inaundwa pindi mazungumzo yatakapofanyika. Bwana Ben Jaafar, ambaye chama chake ni sehemu ya baraza la mawaziri, alikosoa wanasiasa kwa kukosa kuelewana ili kutatua mgogoro unaokumba taifa hilo.
Kumekuwa na maandamano karibu kila siku wananchi wakitoa wito wa kufutiliwa mbali kwa baraza la katiba tangu mwanasiasa huyo mashuhuri kuuawa. Mohamed Brahmi aliuawa tarehe 25 mwezi Julai , takriban miezi sita baada ya kuuawa kwa bwana Belaid, ambaye alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa kushoto. Zaidi ya wanachama 70 wa baraza hilo walijiuzulu kwa upinzani kufuatia mauaji ya wanasiasa hao na kupanga maandamano ya kukesha nje ya makao makuu ya baraza hilo mjini Tunis.Punde baada ya katiba kuandikwa , uchaguzi mpya utafanyika mwezi Disemba. Mgogoro huu wa kisiasa ndio mbaya zaidi kushuhudiwa Tunisia tangu kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa rais Zine al-Abidine Ben Ali kufuatia mapinduzi ya kiraia Januari 2011.

MAREKANI YAFUNGA BALOZI NYINGINE 4 AFRIKA

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani imeendelea kuchukua hatua za tahadhari kwa kufunga balozi zake nyingine 4 za Kiafrika. Hatua hiyo ya Marekani imechukuliwa kabla ya kumbukumbu ya kutimia miaka 15 tangu baada ya milipuko ya mabomu katika balozi zake huko Nairobi na Dar es Salaam tarehe 7 Agosti, 1998.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani imeeleza kuwa, balozi za Marekani katika nchi za Tanzania na Kenya zitaendelea kuwa wazi, isipokuwa imezifunga balozi zilizoko Rwanda, Burundi, Madagascar na Mauritius. Kabla ya hapo, Marekani ilikuwa tayari imeshatangaza kuzifunga balozi za nchi hiyo huko Misri, Jordan, Yemen, Saudi Arabia na Kuwait hadi kufikia tarehe 10 Agosti.
Duru za habari zinasema kuwa, Marekani imeamua kufunga balozi zake kutokana na wasiwasi wa kutokea mashambulio ya kigaidi ya kundi la al Qaeda katika eneo la Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika na maeneo mengine duniani.

LIBYA YAONYA JUU YA USHAMBULIAJI WA VITUO VYA AFYA

Wizara ya Afya nchini Libya imeonya juu ya kile ilichokiita kuwa ni kukaririwa mashambulizi dhidi ya hospitali na vituo vya afya nchini humo. Wizara hiyo imetoa taarifa hiyo mapema leo sambamba na kuonya kuhusiana na mashambulizi dhidi ya hospitali na vituo vya afya vya nchi hiyo, hususan mjini Benghazi na kusisitiza kuwa, mashambulizi hayo yanayofanywa na watu wanaojichukulia sheria mkononi, yana lengo la kudhoofisha huduma za sekta hiyo muhimu. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, kushambuliwa vituo vya afya kunahatarisha zaidi sekta hiyo na kuzitaka taasisi zote na sekta tofauti za serikali na kijamii nchini humo hasa jeshi na asasi za usalama na mabaraza yote ya mikoa kufanya juhudi kubwa ili kumaliza kadhia hiyo.
Wizara hiyo ya afya ya Libya pia imeonya juu ya mwendelezo wa vitendo hivyo na kusisitiza kuwa, kuendelea hali hiyo kunaathiri vibaya sekta ya afya, suala ambalo pia linawalazimisha madaktari na wauguzi wa Libya kukimbia maeneo yao ya kazi.

UWANJA WA NDEGE WA KENNYATTA WAWAKA MOTO

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta katika mji mkuu wa Kenya Nairobi umeharibiwa kufuatia moto uliozuka alfajiri ya leo. Taarifa za awali zinasema kuwa, moto uliozuka leo katika uwanja huo umeharibu vibaya sehemu kubwa ya sehemu ya kufikia abiria uwanjani hapo. Kufuatia tukio hilo, serikali ya Kenya imetangaza kufuta kwa muda safari zote za ndege za ndani na za kimataifa na kuzuia kutua uwanjani hapo ndege, hata kwa dharura. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya David Kimaiyo amesema kuwa, hakuna majeruhi yeyote aliyeripotiwa kufuatia ajali hiyo ya moto. Taarifa za awali zinasema kuwa, moto huo ulianzia katika kitengo cha uhamiaji sehemu wanapogongewa muhuri abiria katika pasi zao za kusafiria kwa ajili ya kuingia ndani na kisha baadaye kusambaa katika sehemu ya abiria ya kuchukulia mabegi. Taarifa zaidi zinasema, moto huo ulianza saa kumi na moja alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki na kuendelea kwa muda wa masaa matatu. Shirika la Ndege la Kenya, "Kenya Airways" limetuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter likiwataka abiria wake kutoelekea katika uwanja wa ndege. Rais Uhuru Kenyatta ametembelea eneo la tukio hilo majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki. Tukio hilo linatarajiwa kukwamisha safari nyingi za ndege zinazotumia uwanja huo.

GAZETI ANNUUR AUG 2, 2013

ANNUUR 1082 by MZALENDO.NET

GAZETI LA ANNUUR JULY 26, 2013

ANNUUR 1081 by MZALENDO.NET