Saturday, December 29, 2012

IRAQ YAKABILIWA NA WIMBI LA NJAMA MPYA

Matukio ya siku chache zilizopita nchini Iraq yamefichua njama mpya zinazopangwa na pande kadhaa dhidi ya nchi hiyo.
Ijumaa ya jana tarehe 28 Disemba miji ya al Anbar, Salahuddin na Mosul ilikumbwa na maandamano ya wapinzani wa serikali ya sasa ya Baghdad. Waandamanaji hao waliojumuisha wafuasi wa chama tawala zamani cha Baath walibeba bendera ya utawala wa zamani wa Iraq na ya makundi ya wapinzani wa serikali ya Syria huku wakipiga nara dhidi ya serikali ya Iraq. Wakati huo huo na sambamba na maandamano hayo, habari zinasema kuwa chama cha dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein cha Baath kimezindua televisheni iliyopewa jina la Falluja kwa msaada wa kifedha wa Qatar. Vilevile kuna habari kwamba kumeanzishwa kundi la wanamgambo lililopewa jina la Jeshi la Ukombozi wa Iraq chini ya uongozi wa Izzat Ibrahim Al Douri, aliyekuwa makamu wa dikteta aliyenyongwa wa Iraq kwa ajili ya kuratibu tena harakati za wafuasi wachama cha Baath nchini humo. Matukio haya yote hayatokei kwa sadfa na yanafichua kwamba kuna sinario na njama inayotekelezwa kwa mpangilio maalumu dhidi ya Iraq.
Baadhi ya weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, matukio ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati hususan hali tata iliyojitokeza huko Syria na vilevile hitilafu zilizoibuka kati ya Wakurdi na serikali ya Baghdad vimetayarisha mazingira kwa makundi ya kichochezi ya ndani na nchi za kigeni kuingilia masuala ya Iraq na kuanza kusambaza sumu na fitina dhidi ya serikali ya Baghdad. Hasa ikitiliwa maanani kwamba shakhsia mkubwa kama Jalal Talabani, Rais wa Iraq ambaye anaaminiwa na karibu makundi yote nchini humo na daima amekuwa mstari wa mbele katika kutatua hitilafu za ndani, amelazwa hospitani akiwa taabani.
Katika hali kama hiyo inaonekana kuwa Magharibi na nchi za Kiarabu zinazofuata sera za Marekani kama Saudi Arabia, Qatar na Uturuki zimezidisha fitina na mchezo mchafu wa kueneza hitilafu ndani ya Iraq. Hii ni pamoja na kuwa, Marekani bado inafanyia kazi mpango wa kuzigawa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati hususan Iraq.
Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu wanatumia mbinu ya kuzusha machafuko ya kimadhehebu na kikaumu katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kama Lebanon, Syria na Iraq. Baada ya kuzusha mapigano ya kikaumu na kimadhehebu huko kaskazini mwa Lebanon na vita vya ndani huko Syria inaonekama kuwa sasa imewadia zamu ya Iraq.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, moto wa hitilafu zilizotokea kati ya viongozi wa eneo la Kurdistan na serikali ya Baghdad na kuyalazimisha majeshi ya pande hizo mbili kuelekezeana mitutu ya bunduki, na maandamano yaliyofanyika kwa lengo la kuchochea hitilafu za kimadhehebu kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni katika maeneo ya Wasuni wengi umewashwa na nchi za kigeni na ni ishara kuwa Iraq inakabiliwa na njama na tishio kubwa.
Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Waziri Mkuu wa Iraq Nuri Al Maliki akasema waziwazi kuwa, sera za kuzusha hitilafu za kimadhehebu na kikaumu hazitaifikisha popote Iraq na ameyaasa makundi yote ya upinzani kuketi kwenye meza ya mazungumzo.      

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO