Thursday, December 27, 2012

WASYRIA WALIOUWAWA WAFIKIA 45,000


Idadi ya waliouawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ni zaidi ya watu 45,000, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza. Idadi hiyo imetangazwa huku mpatanishi wa kimataifa kuhusu mzozo huo, Lakhdar Brahimi, akielekeza matumaini yake kwa Urusi, kusaidia kutafuta suluhu la amani.
Mkuu wa shirika hilo la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria, Rami Abdel Rahman, amesema kuwa watu zaidi ya 1,000 wameuawa mnamo wiki moja iliyopita. Tangazo hilo limezidisha hofu iliyoelezwa na Umoja wa Mataifa kwamba hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya nchini Syria. Mjumbe maalumu wa umoja huo kuhusu Syria Paulo Pinheiro amesema ripoti za hivi karibuni zimedhihirisha ghasia zenye misingi ya kikabila.
Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uturuki imesema kwamba Wasyria zaidi ya 1,000 walikimbilia nchini humo katika muda ma saa 24 zilizopita. Wakati huo huo, Marekani imekaribisha kwa tahadhari, taarifa kwamba mkuu wa polisi jeshini General Abdel Aziz Jassem al-Shallal amejitenga na serikali ya Rais Bashar al-Assad na kujiunga na upinzani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO