Jinamizi la maandamano na migomo linazidi kuusakama utawala wa Kizayuni wa Israel huku mwaka huu wa 2012 ukielekea ukingoni. Matukio ya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yanabainisha kwamba, Israel itaingia katika mwaka mpya wa 2013 huku ikiandamwa na wimbi la maandamano na malalamiko ya Wazayuni kutokana na kushadidi mgogoro wa kiuchumi na kile kinachoonekana kuwa, kutokuwa na ustahiki na uwezo viongozi wa Tel Aviv wa kutatua migogoro lukuki inayoukabili utawala huo haramu. Kupanuka wigo wa malalamiko, migomo na maandamano huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kunatokea katika hali ambayo, sekta mbalimbali za kiuchumi za Israel nazo zimo katika hali ya kufilisika huku wafanyakazi wengi wakikabiliwa na hatari ya kukosa ajira zao. Katika fremu hiyo mamia ya wafanyakazi wa shirika kubwa kabisa la simu la Israel la Pelephone wameandamana mjini Tel Aviv na kukusanyika mbele ya nyumba ya Gil Sharon, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo. Mgomo wa wafanyakazi wa shirika hilo la simu umeingia katika wiki yake ya nne. Hii ni katika hali ambayo, wafanyakazi wa Bezeq shirika jengine linalotoa huduma za simu, wamejiunga na wenzao wa Pelephone katika mgomo huo. Kujiunga wafanyakazi wa mashirika hayo ya simu na mgomo wa wafanyakazi wa mashirika mengine, kumeifanya migomo dhidi ya Israel iingie katika hatua na marhala mpya kabisa. Gazeti la Israel la Haaretz limeripoti juu ya kuenea mgomo na maandamano ya wafanyakazi wa kiwanda cha ufumaji cha utawala huo ghasibu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo waandamanaji hao wakiwa na mabango na maberamu wamechoma matairi na kufunga njia ya mlango mkuu wa kiwanda hicho kwa kuweka mkusanyiko mkubwa. Hii ni katika hali ambayo, wafanyakazi wa viwanja vya ndege vya Israel nao wametishia kuwa, endapo hawatoongezewa mishahara na kuboroshewa huduma na suhula za kazi watafanya mgomo katika kipindi hiki cha kukaribia mwaka mpya wa Miladia. Shirika la Umeme la Israel ambalo ndilo shirika pekee la umma linalotoa huduma ya ugavi wa umeme huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu limetangaza kuwa, linakaribia kukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha kutokana na mzigo mkubwa wa madeni; hivyo huenda likawafukuza kazi wafanyakazi wake 2000 waliojiriwa rasmi. Kwa hakika kushadidi mgogoro wa kiuchumi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kunabainisha kugonga ukuta hatua za viongozi wa Israel za mwaka huu wa 2012 za kumfukuza pepo mbaya wa mgogoro wa kiuchumi wa utawala huo ghasibu. Kwa mukatadha huo, mwaka huu wa 2012 unaweza kupewa jina la “mwaka wa kushadidi migogoro mbalimbali ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel” ikiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kama vile haitoshi, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, katika mwaka huu wa 2012 vitendo vya jinai na uhalifu vimeongezeka sana huko Israel. Fauka ya hayo, kushikana mashati, kunyoosheana vidole vya lawama na mivutano ya kisiasa nayo imeonekana kushika kasi baina ya viongozi wa utawala huo; jambo ambalo limeifikisha Israel katika hatua ya kufanyika uchaguzi wa Bunge wa kabla ya wakati ambao unatarajiwa kufanyika Januari 22 mwakani. Ala kulli haal, mwenendo wa kuongezeka migogoro ya kiuchumi, kisiasa na kijamii huko Israel ni jambo linalobainisha kwamba, kivitendo viongozi wa utawala huo hawana ubavu wa kudhibiti hali ya mambo na kwamba harakati ya utawala huo inaelekea upande wa kuangamia na kusambaratika. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, kukithiri malamamiko na maandanao ya raia wa Kizayuni ni ithbati tosha kuwa, Israel sio tu kwamba, haina uhalali kimataifa, bali haikubaliki hata na raia wake wenyewe; na kwa msingi huo hatima ya utawala kama huu si nyingine ghairi ya kuangamia na kusambaratika.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO