Marekani imekosoa uamuzi wa Israel kujenga nyumba 3,000 za
walowezi mashariki mwa Jerusalem na katika ukingo wa magharibi, ambapo waziri
Hillary Clinton amesema hatua hiyo kuwa inarudidha nyuma jitihada za amani.
Mapema, Ikulu ya Marekani iliita hatua hiyo ambayo imekuja siku
moja baada ya Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kihistoria na kuipandisha
Palestina hadhi ya nchi muangalizi siku ya Alhamisi kwa kuzingatia mipaka ya
mwaka 1967, kama isiyo na manufaa yoyote. "Kwa kuzingatia tangazo la leo
(30.11.2012), naomba nirejee kwamba utawala huu, kama tawala zilizotangulia,
umeweka bayana kwa Israel kuwa shughuli hizo zinarudisha nyuma jitihada za
majadiliano ya amani," alisema Clinton.
Clinton aliyasema hayo wakati akizungumza katika jukwaa
lilioandaliwa na kituo cha sera za mashriki ya kati cha Saba mjini Washington,
mbele ya hadhira iliyowajumuisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Israel Avigdor
Lieberman na wa Ulinzi Ehud Barak. Clinton alisema kuwa suluhisho la kudumu la
mgogoro wa Gaza lingekuwa mpango mpana wa amani kati ya Israel na Wapalestina
wote, wakiongozwa na wawakilishi wao halali, mamlaka ya Palestina.
Aelezea sababu za kuipinga Palestina Umoja wa Mataifa
Utawala wa rais Barack Obama ulijaribu kuzuia shinikizo la
Palestina la kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, ukisema kuwa hatua hiyo ingekuwa
kizingiti katika njia ya amani na kwamba taifa la Palestina lingetokana tu na
mazungumzo na Israel. "Wote tunapaswa kuweka kituo baada ya kura ya wiki
hii. Pande zote zinapaswa kutafakari kwa kina njia iliyoko mbele yetu,"
Clinton alisema. Aliongeza kuwa pande zote zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja
ili kutafuta njia ya kusonga mbele katika mazungumzo ambayo ndiyo yataleta
suluhisho la mataifa mawili, ambayo inabaki kuwa shabaha yao.
Alisema pande mbili zitakapokuwa tayari kushiriki tena
mazungumzo, rais Obama atakuwa tayari kushirikiana nao kikamilifu. Mapema,
msemaji wa bazara la taifa la usalama, Tommy Vietor alisema kuwa Marekani
inarejea upinzani wake wa muda mrefu dhidi ya makaazi ya walowezi, ujenzi
mashariki mwa Jerusalem na matangazo ya Israel. "Tunaamini vitendo hivi
havileti manufaa yoyote zaidi ya kuhujumu jitihada za kurudi kwenye meza ya
mazungumzo;" alisema Vietor.
PLO yalaani tangazo la Israel
Taarifa za vyombo vya habari zimesema baadhi ya ujenzi wa Israel
utafanyika katika eneo linalogombaniwa katika ukingo wa magharibi maarufu kama
E1, ambalo linapita kati ya upande wa mwisho wa mashariki ya eneo lililotekwa
la Jerusalem mashariki, na makaazi ya Maaleh Adumim. Chama cha Ukombozi wa
Palestina, PLO, kimelaani hatua hiyo na kusema ni uvamizi dhidi ya taifa hilo.
Wapalestina wanapinga kwa nguvu zote, mradi wa E1 kwa sababu unaligawanya eneo
la ukingo wa magharibi katika vipande viwili - kaskazini na kusini, hatua
ambayo inafanya uundwaji wa taifa la Palestina kuwa mgumu.
Wapalestina wanaitaka Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa lao na
wanapinga mipango ya upanuzi wa Maaleh Adumim, eneo lililoko kilomita 5 kutoka
ukingo wa mashariki wa mji wa Jerusalem. Kitendo cha Marekani kulaani ujenzi wa
makaazi ya walowezi na Israel huko nyuma kimekuwa kikisababisha malumbano kati
ya Obama na waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Viongozi hao wawili wana uhusiano
wa mashaka hivi sasa, licha ya hoja za utawala wa rais Obama kuwa serikali hiyo
imefanya kazi ya ziada kuhakikisha inalinda usalama wa Israel kuliko utawala
uliyopita.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO