Kupanuka wimbi la maandamano katika maeneo tofauti ya Saudi Arabia ukiwemo mji mkuu wa Riyadha, kumepelekea kuongezeka mashinikizo kwa utawala wa ukoo wa Aal Saud kwa ajili ya kufanyika marekebisho katika siasa za utawala huo. Katika siku za Jumatatu na Jumanne, umati mkubwa wa Wasaudia ulifanya maandamano katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu Riyadh, wakitangaza mfungamano wao na wafungwa wa kisiasa wanaoendelea kushikiliwa katika jela za utawala huo na kutaka kukomeshwa adhabu dhidi ya wafungwa hao. Waandamanaji pia walizitaka taasisi na asasi mbalimbali za haki za binaadamu nchini humo na zile za kimataifa, kufichua jinai zinazotendwa na utawala wa Aal Saud dhidi ya wafungwa wa kisiasa, sambamba na kuwashinikiza viongozi wa utawala huo wawaachie huru wafungwa hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishikiliwa katika jela bila ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na kupanuka kwa mwamko wa Kiislamu Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, wananchi wa Saudia pia walianzisha maandamano ya amani, wakitaka kufanyika marekebisho ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Mfalme mgonjwa wa Saudia ambaye alishuhudia mwisho mbaya wa madikteta wenzake huko Tunisia na Misri, alifanya njama ya kuwahonga wananchi wa nchi hiyo kwa kuwapa fedha ili waachane na maandamano dhidi ya utawala wake. Hata hivyo juhudi hizo hazikumsaidia mfalme Abdullah wa Saudia kwani maandamano katika maeneo ya mashariki yamezidi kupanuka na kufika katika maeneo na sekta nyingine vikiwemo vyuo vikuu. Aidha katika kulalamikia ukosefu wa usawa na kufumbiwa macho haki zao nchini humo wanawake nao wamemiminika mabarabarani na kuendesha magari kwa lengo la kudhihirisha uasi wao wa kiraia kwa utawala wa nchi hiyo. Utawala wa Saudi Arabia ambao umefananishwa na taasisi za haki za binaadamu kuwa sawa na ngome ya udikteta, unaendeleza vitendo vya ukandamizaji, kamatakamata, adhabu kali na kuwazuilia kwa muda mrefu katika jela zake wapinzani na wanaharakati wa kisiasa nchini. Ukandamizaji huo unaofanywa na utawala wa Riyadh, umesababisha kuongezeka kwa upinzani nchini humo na kufanya upinzani uliokuwa katika maeneo ya mpakani kuingia katika miji mingine ukiwemo mji mkuu Riyadh.
Kupanuka kwa wimbi la upinzani mjini Riyadh kunaashiria kwamba, wapinzani nchini Saudia, si tu kwamba wanalalamikia huduma za chakula na kiuchumi, bali pia wanapinga udikteta, ukatili na vitendo vinavyokinzana na haki za binaadamu nchini humo. Utawala wa Riyadh unafuata mfumo wa kifalme, ambao unaweka madaraka yote muhimu ya nchi mikononi mwa ukoo wa Aal Saud. Ubaguzi huo wa kisiasa umepelekea kuongezeka ufisadi wa kisiasa na kiuchumi katika muundo wa kisiasa wa Saudia. Utawala wa nchi hiyo umefikia kiwango cha kufumbia macho haki muhimu za raia wake, ukiwemo ushiriki wa kisiasa na haki za kijamii kama vile za uendeshaji magari na upigaji kura kwa wanawake. Mbali na hayo, mfumo wa mahakama wa nchi hiyo unawakandamiza moja kwa moja wapinzani. Karibu wafungwa wa kisiasa elfu 30 wanashikiwa kwa muda mrefu katika jela za Saudi Arabia bila kusomewa mashtaka mahakamani, na wala jamaa zao hawana habari yoyote kuhusiana na mustakbali wao. Na Sudi Jafar
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO