SHULE ya Sekondari Kibiti imeifungwa shule kwa madai ya mgogoro wa kidini hivyo
wanafunzi kupewa saa mbili kutoonekana shuleni hapo vinginevyo watachukuliwa
hatua za kisheria.
Kufungwa kwa shule hiyo kumefikiwa na Bodi
iliyokutana na kuamua kuifunga shule hiyo kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa
matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na hisia za kidini zinazozidi kukua kwa
kasi shuleni hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, amethibitisha
kufungwa kwa shule hiyo.
“Sipo Rufiji lakini nimejulishwa kuhusiana na
kufungwa kwa shule hiyo,”alisema kwa ufupi.
Chanzo cha kufungwa kwa shule
hiyo inadaiwa kuwa ni malalamiko ya pande zote mbili baina ya wanafunzi Waislam
na Wakikristo ambao wamekuwa wakilaumiana kila upande kudhalilisha dini ya
mwenzake hapo shuleni.
Mmoja wa wanafunzi hao wa dini ya kiislam ambaye
aliomba asitajwe jina na kudai kuwa waislam wanalalamika kuwa wakiwa wanafanya
ibada katika eneo hilo wenzao wa dini ya kikristo huwafanyia
fujo.
Alisema kuwa sababu nyingine ni kwamba wanafunzi wenzao siku moja
walikwenda kutafuta nyama ya nguruwe na kuja kuitumia katika vyombo
vinavyotumika shuleni hapo.
Kwa upande wa wanafunzi wa kikristo wao
wanasema kuwa wanafunzi wenzao walichana chana Biblia na kuchoma ofisi yao ya
kidini iliyopo hapo shuleni .
Alisema kuwa bodi ya shule imelazimika
kuifunga shule hiyo kwa muda usiojulikana ili kuepuka vurugu kutokea shuleni
hapo ili wapate muda wa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.
Mmoja wa
wanafunzi hao alisema kuwa wanafunzi hao walilalamikia suala hilo kwa muda mrefu
bila kupatiwa ufumbuzi na ndipo kukawa na mgomo wa hapa na pale wakiutuhumu
uongozi wa shule hiyo kwa kushindwa kuthibiti malalamiko
hayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Mkuu wa shule hiyo,
Leslaus Kihongosi alithibitisha kufungwa kwa shule hiyo lakini akasema kuwa
hawezi kuwa msemaji wa suala hilo kwa kuwa sio mmiliki wa shule
hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji anayedaiwa
kuwa mmiliki wa shule hiyo Nasoro Mwingira alipoulizwa kuhusiana na kufungwa
kwa shule hiyo alisema kuwa amepata taarifa za tukio hilo.
“Nasema kwa
sasa siwezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa naelekea kwenye tukio nipo
njiani,”alisema.
Diwani wa kata ya Mtawanya iliyopo shule hiyo ya
kitaifa, Rashidi Mkinga alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa
analisikia mitaani na hakushirikishwa katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo na
yeye hawezi kusema lolote.
Haijafahamika mgogoro wa kidini baina ya
wanafunzi wa dini mbili hizo umeanza lini kutokana na wahusika kukwepa
kulizungumzia suala hilo huku wakitupiana mpira.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO