Mataifa ya magharibi yamemtaka rais wa Syria Bashar al-Asad kuhakikisha anashiriki kwenye suluhu ya kupata amani nchini humo na kuonya kuwa iwapo atashindwa kuzungumza kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito basi wataendelea kuwafadhili waasi kwa silaha. Kauli ya viongozi wa mataifa hayo imetolewa kwenye mkutano unaofanyika kwenye mji wa Amman nchini Jordan, mkutano unaolenga kusaka suluhu ya machafuko ya Syria.
Nchi ya Urusi inaunga mkono kuundwa kwa serikali ya mpito ingawa inasisitiza kujumuishwa kwa rais Asad kwenye serikali hiyo jambo ambalo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry analipinga. Serikali ya Syria imesisitiza rais Asad kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao na kwamba maamuzi ya nani awe rais wa Syria yatatokana na wananchi wenyewe wa Syria.
Mapema jumatano Upinzani nchini Syria ulitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa na jukwaa la kushughulikia misaada ya kibinadamu kwa lengo la kusaidia mji wa Qusayr ambapo kumeshuhudia mapigano makali kati ya majeshi ya serikali ya Syria dhidi ya waasi. Urusi imeendelea kuonekana kuwa mshirika wa muhimu wa utawala wa raisi wa Syria Bashar Al Assad huku mataifa ya magharibi wakiitaka serikali ya Moscow kuitumia fursa yake kuisaidia kukomesha mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa takribani miaka miwili sasa baina ya serikali dhidi ya waasi.
Hayo yanajiri wakati taarifa kutoka kwa vyombo vya usalama zikiarifu katika jiji la Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon watu sita wameuawa na wengine arobaini kujeruhiwa usiku wakati wapinzani walipopambana na wanajeshi watiifu wa raisi Assad.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO