Thursday, December 27, 2012

MTAZAMO WA MAREKANI JUU YA DEMOKRASIA


Uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Misri kwa rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo umeiweka njia panda Marekani ya kuyakubali au kuyakataa matakwa ya kidemokrasia ya Wamisri waliowengi.  Katika radiamali yake ya kwanza kwa asilimia 64 ya kura za wananchi wa Misri walioipigia kura ya ‘ndiyo’ rasimu ya katiba mpya, Washington imetangaza kuwa demokrasia ni zaidi ya matakwa ya kura za waliowengi. Kwa maneno mengine ni kwamba ikiwa katika nchi yoyote ile wananchi waliowengi watalipigia kura za ‘ndiyo’ suala lisiloiridhisha Marekani demokrasia haitokuwa imefikiwa.
Bila ya shaka kuyapuuza matokeo ya kura zinazoakisi matakwa ya wananchi si kitu kigeni na cha ajabu kwa Marekani, na tukio la kura ya maoni ya katiba mpya ya Misri si la kwanza na wala halitokuwa la mwisho. Miaka sio mingi iliyopita wakati wananchi wa Palestina walipoichagua harakati ya Hamas katika uchaguzi wa kwanza huru, Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Marekani Condoleeza Rice alitamka kwamba demokrasia, haina maana tu ya kulipa uhalali wa kisheria kila kundi linalochaguliwa kwa masanduku ya kura. Ni kwa mantiki hiyo Marekani na Israel zilizidisha mashinikizo kwa wananchi wa Palestina ya kuwakomoa na kuwadhibu kwa sababu tu ya kushiriki katika uchaguzi huru na wa kidemokrasia. Mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Gaza na baadaye vita vya siku 22 dhidi ya watu wa eneo hilo zilikuwa miongoni mwa radiamali za Washington na Tel Aviv kwa uamuzi uliochukuliwa na wananchi wa Palestina katika uchaguzi wao wa bunge.
Hivi sasa Marekani inakabiliwa tena na mazingira yanayofanana na yale. Itakumbukwa kuwa kwa miongo kadhaa sasa Washington imekuwa ikijigamba kuwa ndio kiranja na kinara wa uhuru na demokrasia duniani. Lakini licha ya majigambo hayo kuna vielelezo na mifano hai kadha wa kadha inayosuta madai hayo ya Washington. Kwa mfano hakuna asiyejua kuwa katika kipindi chote hiki cha nusu karne iliyopita kumekuwepo na tawala kadhaa za kidikteta na kandamizi zaidi duniani ambazo zilikuwa ni waitifaki wakubwa wa Marekani. Katika baadhi ya nchi Marekani imehusika waziwazi katika mapinduzi ya kijeshi ya kuziangusha serikali halali na zilizochaguliwa na wananchi au kuwasha moto wa vita vya ndani au vya kieneo dhidi ya serikali zisizokubali kuburuzwa na nchi hiyo. Mifano ya aina hii ni mingi mno hususan katika eneo hili la Mashariki ya Kati. Si siri kwamba vuguvugu la mapambano ya wananchi wa eneo hili ambalo vyombo vya habari vya Magharibi vimelipa jina la ‘Msimu wa Machipuo ya Kiarabu’ yalikuwa ni mapambano dhidi ya tawala vikaragosi na vibaraka wa Marekani. Kwani watawala waliong’olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi katika nchi za Tunisia na Misri, kwa miongo kadhaa walikuwa wakipata himaya na uungaji mkono wa kiuchumi na kisiasa wa Marekani na nchi za Ulaya licha ya kufanya ukandamizi na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia wao. Lakini kwa vile walikuwa wakikidhi na kudhamini maslahi ya Washington waliendelea kupata himaya ya madola ya Magharibi. Kwa kuzingatia rekodi hiyo haitokuwa ajabu ikiwa serikali ya Marekani itatia ulimi puani na kuyakataa matokeo ya kura ya maoni ya katiba ya Misri na kuielezea demokrasia kuwa ni kitu zaidi ya kura na matakwa ya waliowengi. Japokuwa wakati wa harakati za kumng’oa madarakani dikteta Hosni Mubarak na katika matukio yaliyojiri baadaye nchini Misri Washington haikujionyesha waziwazi kuwa iko dhidi ya wananchi wa nchi hiyo lakini kuongezeka harakati za Kiislamu, hisia za kutaka kujitawala na chuki dhidi ya Israel ndani ya Misri kumeitia hofu na wasiwasi mkubwa Marekani. Kwa hivyo tusije tukashangaa kuona serikali iliyochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi waliowengi wa Misri na maamuzi yatakayochukuliwa na serikali hiyo, mwishowe yanagongana na kukinzana na maslahi ya Marekani. Endapo hilo litajiri Washington inaweza kuchukua hatua sawa na zile za mwaka 1953 nchini Iran za kuiangusha kupitia mapinduzi ya kijeshi serikali halali ya Waziri Mkuu Dakta Muhammad Musaddiq, mwaka 1973 nchini Chile za kuiangusha kwa mbinu hiyo hiyo serikali halali ya Salvador Allende au za mwaka 2006 za kuiwekea vikwazo ya serikali halali ya Palestina. Kwa maneno mengine ni kuwa Washington ima itaandaa mazingira ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Misri au itaiwekea mbinyo na mashinikizo serikali ili kuwakomoa na kuwatia adabu wananchi wa nchi hiyo. Na sababu ya yote hayo ni kwamba kwa mtazamo wa Marekani demokrasia hukubalika na kutambuliwa rasmi pale tu matokeo yake yanapokidhi na kudhamini maslahi ya nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO