Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilipasisha vikwazo dhidi ya kundi la waasi wa M23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na waungaji mkono wao wa Rwanda. Kwa mujibu wa baraza hilo vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia fedha za viongozi wa kundi hilo au watu wenye uhusiano na kundi hilo pamoja na kuwapiga marufuku kufanya safari za nje. Ni kwa muda sasa ambapo waasi wa M23 wamelitumbukiza katika dimbwi la machafuko eneo la mashariki mwa Kongo ambapo mbali na kufanya vitendo vichafu kama vya ubakaji, mauaji na uporaji katika majengo ya serikali, limegeuka na kuwa tishio kwa usalama na uthabiti wa Kongo. Katika miezi ya hivi karibuni waasi hao wamesonga mbele na kufanikiwa kuudhibiti mji wa Goma makao makuu ya Kivu Kaskazini. Hata hivyo, kushtadi mashinikizo ya kieneo na kimataifa dhidi ya waasi hao, kumewalazimisha kuondoka katika mji huo. Viongozi wa Kiafrika wamewataka waasi hao waachane na matakwa yao ya kutaka kuiangusha serikali na wajiepushe kuitumbukiza tena Kongo katika vita. Kuondoka waasi wa M23 huko Goma kulifungua mlango wa mazungumzo baina yao na serikali na hivyo kukahuishwa matumaini ya kupatikana amani katika nchi hiyo. Vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vimepasishwa katika hali ambayo, mazungumzo baina ya waasi wa M23 na serikali ya Kinshasa yamepangwa kuendelea tena mwezi huu baada ya kumalizika sherehe za Krismasi na mwaka mpya. Mazungumzo hayo yaliyokuwa yameanza tarehe 21 Desemba mwaka jana huko Kampala Uganda, yalisitishwa kwa muda na pande mbili kuafikiana kuendelea tena na vikao vyao mwezi huu wa Januari. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, tuhuma zinazowakabili waasi wa M23 za kushambulia helikopta za Umoja wa Mataifa ni jambo ambalo limeifanya nafasi yao izidi kuwa tata. Hivi karibuni kamanda wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa huko mashariki mwa Kongo sanjari na kutahadharisha mashambulio ya mara kwa mara ya waasi dhidi ya helikopta za UN aliwataka waasi hao wasitishe mashambulio hayo. Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kusema kuwa, kushambuliwa vikosi vya UN ni katika jinai za kivita na ukaonya kuwa, endapo waasi wa M23 watakariri tena mashambulio hayo basi watashtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Hii ni katika hali ambayo waasi wa M23 wamekadhibisha tuhuma hizo. Waasi hao wanawatuhumu wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba, hawafahamu hasa kile kinachojiri mashariki mwa Kongo na kwamba, ripoti yao haina itibari. Baadhi ya wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushadidishwa vikwazo na mashinikizo dhidi ya waasi wa M23 kunabainisha ukweli huu kwamba, waasi hao hawafungamani na madola makubwa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO