Tuesday, March 05, 2013

JARIBIO LA MAPINDUZI YA KIJESHI LAZIMWA BENIN


Serikali ya Benin Machi 3 ilitangaza kuwa kumefanyika jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Boni Yayi wa nchi hiyo. Mwendesha Mashtaka wa serikali ya nchi hiyo, Justin Gbenameto amesema kuwa tayari watu kadhaa wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo. Gbenameto amesisitiza kuwa kanali mmoja wa jeshi aliyefahamika kwa jina la Pamphile Zomahoun pamoja na mfanyabiashara mashuhuri, Johannes Dagnon ni miongoni mwa watu waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na jaribio la mapinduzi la Februari 22 ambapo lengo lilikuwa kumuondoa madarakani Rais Yayi na kuanzisha serikali ya kijeshi. Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Benin amefichua pia kwamba tayari kamati ya uchunguzi imeundwa na imeanza kazi kubaini wahusika wengine. Imedaiwa kuwa wapanga mapinduzi walijaribu kumzuia Rais Boni Yayi kurejea nchini akitokea Equatorial Guinea alikokuwa amekwenda kuhudhuria mkutano uliowakutanisha pamoja viongozi kadhaa wa Afrika na wale wa Amerika ya Latini.
 Jaribio la mapinduzi si jambo geni nchini Benin kwani itakumbukwa kuwa, mwaka uliopita, mpambe wa karibu wa Rais Yayi alijaribu kubadilisha dawa za maradhi ya moyo za kiongozi huyo na sumu ya kuua panya lakini mbinu yake ikatibuka. Kuhusu tukio hilo, watu kadhaa walikamatwa akiwemo Waziri wa Biashara na bintiamu wa Rais Yayi pamoja na daktari wake. Nchi hiyo aidha imeshuhudia mapinduzi kadhaa ya kijeshi katika miaka 1963, 1965 na 1969.
Boni Yayi mwenye umri wa miaka 60, alichukua madarakani mwaka 2006 na kisha akachaguliwa kuongoza tena nchi hiyo mwaka 2011. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kiongozi huyo amejilimbikizia maadui chungu nzima kutokana na misimamo yake ya kupinga ufisadi. Mtego wa kiongozi huyo dhidi ya ufisadi umewanasa watu kadhaa wa ngazi za juu wakiwemo mawaziri ambao kwa sasa wanasotea jela; jambo linaloendelea kuwakosesha usingizi masogora na miamba ya ufisadi nchini humo. Hata hivyo kiongozi huyo ametuhumiwa na wapinzani kwamba anatumia mkono wa chuma kuwafunga midomo wakosoaji wake. Pia imedaiwa kwamba, waandishi habari wamekuwa wakiandamwa na vyombo vya dola kutokana na kuchapisha au kutangaza makala zinazokosoa uongozi wa Rais Yayi.
Kiongozi huyo ambaye mwanzoni mwa mwaka huu alimaliza kipindi chake cha uongozi kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), anasifiwa kwa juhudi zake za kutetea uhuru na kujitawala nchi za Kiafrika. Pia alikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika walioshinikiza kutumwa kikosi cha Jumuiya ya ECOWAS huko kaskazini mwa Mali kukabiliana na makundi ya waasi wenye misimamo mikali ambao walikuwa wameteka miji mingi katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO