Wanawe rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela, wameamua
kuchukua hatua za kuwaondoa wasaidizi wake watatu kutoka katika makampuni
anayoyamiliki. Hii ni kwa mujibu wa vyombo ya habari nchini humo. Makaziwe na Zenani Mandela wanadai kuwa watatu hao hawana haki ya kuwa kwenye
bodi mbili za kampuni hiyo ambazo ni za thamani ya dola milioni 1.1. Mmoja wa wasaidizi hao, ambaye pia ni wakili wa Mandela, George Bizos,amekana
madai hayo.
Kesi hiyo inakuja wakati kuna wasiwasi mkubwa kuhusu afya ya Mandela mwenye
umri wa miaka 94. Mandela aliondoka hospitalini baada ya kutibiwa ugonjwa wa mapafu pamoja na
homa ya mapafu. Mandela alilazwa hospitalini mara ya nne katika kipindi cha miaka miwili. Duru zinasema kuwa kumekuwa na mzozo wa kichinichini tangu mwaka 2005 wa
kudhibiti pesa zinazotokana na mauzo kwenye jina la Mandela hususan picha
alizokuwa anachora akiwa jela.
Makaziwe na Zenani Mandela waliwasilisha kesi mahakamani wakidai kuwa bwana
Bizo, waziri wa nyumba, bwana Tokyo Sexwale na wakili wa zamani wa Mandela,
Bally Chuene, hawakuwahi kuteuliwa kama wamiliki au wakurugenzi wa kampuni ya
Harmonieux Investment Holdings na Magnifique Investment Holdings, kulingana na
gazeti la Star. Pesa zinazotokana na makampuni hayo zinapaswa kuwafaidi wanawe Mandela na
yeye mwenyewe. "Bizos, Chuene na Sexwale hawakuwahi kuteuliwa rasmi kama washika dau katika
kampuni hiyo.'' Bwana Bizos, wakili anayeheshimika sana na ambaye pia ni rafiki wa karibu
sana wa bwana Mandela, alisema kuwa watajitetea vikali katika kesi hiyo. Aliongeza kuwa wanawe Mandela walikuwa wanataka kuuza vitu ambavyo havipaswi
kuuzwa .
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO