Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa akishauriana na wawakilishi wa waandamanaji jijini Ankara usiku kucha kuwashawishi kuachana na maandamano ambayo yanaendelea kwa juma la pili sasa. Kikao hicho kilifanyika baada ya Waziri Mkuu Erdogan kusema kuwa, ametoa onyo la mwisho kwa waandamanaji hao kuachana na maandamano hayo au watakiona cha mtema kuni tishio ambalo wamepuuzilia mbali na kusalia katika viwanja vya Taksim mjini Istanbul. Mmoja wa kiongozi wa makundi hayo ya waandamanaji Tayfun Kahraman amesema kuwa mazungumzo kati yao na Waziri Mkuu yalionekana kuzaa matunda na huenda wakawaomba waandamanaji hao kuondoka katika viwanja hivyo siku ya Ijumaa.
Waandamanaji hao wamesema kuwa hawataondoka katika viwanja hivyo hadi pale serikali itakapositisha mpango wake wa kujenga kambi za kijeshi na maduka katika viwanja hivyo wanavyosema ni vya kihistoria. Awali, Erdogan alisema kuwa huenda akalazimika kutangaza kufanyika kwa kura ya maoni nchini humo kuamua hatima ya maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali jijini Instabul na miji mingine nchini humo. Licha ya hali ya utulivu kushuhudiwa kwa saa kadhaa siku ya Jumatano, waandamanaji walijitokeza tena katika ukumbi wa Taksim na kuanza kukimbiza na polisi waliotumia mabomu ya kutoa machozi kuwasambaratisha. Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiweno lile la Kimataifa la Amnesty International limemshtumu nguvu inayotumiwa na polisi dhidi ya maandamano hayo na badala yake inataka serikali kuzungumza na waandamanaji hao.
Waandamanaji hao wanasema wamechoswa na serikali ya Erdogan na pia wanaongeza kuwa kiongozi huyo ameanza kuweka sheria za Kislamu nchini humo kinyume na sheria. Juma lililopita Erdogan aliwaambia wafuasi wake kuwa wamekuwa wavumilivu mno na mwishoni mwa wiki hii nao wataanza mikutano yao ya hadhara ya kuiunga mkono serikali ikiwa maandamnao ya wapinzani yataendelea. Maandamano nchini Uturuki yalianza mwisho mwa mwezi uliopita jijini Instabul na kusambaa kote nchini kupinga uongozi wa Erdogan ambao waandamanaji hao wanasema ni wa Kidikteta. Waandamanaji zaidi ya 5,000 wamejeruhiwa kutokana na maandamano hayo wengi wao vijana.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO