Friday, April 05, 2013

MISRI YAKATA MELI YA ISRAEL YENYE SHEHENA YA SILAHA

Vyombo vya usalama vya Misri vimeikamata meli yenye shehena kubwa ya silaha baada ya kuingia katika maji ya nchi hiyo ikitokea bandari ya Ilat huko Israel. Wafanyakazi wote waliokuwa katika meli hiyo pia wametiwa nguvuni.
Vyombo vya usalama vya Misri vimeripoti kuwa meli hiyo yenye silaha ina masanduku 105 yenye aina mbalimbali za silaha kwa ajili ya kampuni moja ya masuala ya usalama ya Kiafrika.
Maafisa usalama wa Misri wamesema kuwa meli hiyo itaendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama hadi uchunguzi kamili utakapokamilika na kuhakikisha kwamba haikuwa katika mikakati ya kutorosha silaha kwa ajili ya makundi ya kigaidi.
Viongozi wa utawala haramu wa Israer wamekataa kusema lolote kuhusu meli hiyo ya silaha iliyokamatwa na jeshi la majini la Misri.

MADAKTARI WASEMA KIFO CHA MFUNGWA WA KIPALESTINA NI UZEMBE WA ISRAEL

Jumuiya ya Madaktari Watetezi wa Haki za Binadamu imetangaza kuwa kifo cha mateka wa Kipalestina aliyekuwa akishikiliwa katika korokoro za kutisha za Israel Maisara Abu Hamdiyeh kimesababishwa na uzembe na kupuuzwa na maafisa wa jela ya Ishel ya Israel.
Jumuiya hiyo imesema kuwa kifo cha Mpalestina huyo katika jela ya Israel kinazidisha wasiwasi juu ya hali mbaya na matatizo ya maelfu ya wafungwa wa Kipalestina walioko katika jela za Israel.
Maisara Abu Hamdiyeh ambaye amekuwa katika jela ya Israel tangu mwaka 2002 alifariki dunia Jumanne iliyopita katika jela ya Ishel baada ya kuzidiwa na maradhi kwa kupuuzwa na maafisa wa jela hiyo. Waziri anayeshughulikia masuala ya mahabusi wa Kipalestina katika jela za Israel Issa Qaraqe amekitaja kifo hicho kuwa ni aina fulani ya hukumu ya kifo iliyotekelezwa kwa njia ya kimyakimya.

MAREKANI KURUDISHA MAENEO YA JAPAN ILIYOYATEKA

Japan na Marekani zimekubaliana mpango wa kuirudishia Japan sehemu ya ardhi inayokaliwa na jeshi la Marekani, katika jaribio la kuondoa hali ya mkwamo katika mvutano wa muda mrefu. Shirika la habari la Kyodo limesema, Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, na Balozi wa Marekani, John Roos, wanatarajiwa kusaini makubaliano hayo baadaye leo, yanayohusiana na maeneo matano ya jeshi la Marekani na sehemu nyengine katika kisiwa kikuu cha Okinawa.
Japan na Marekani pia zimekubaliana kwamba ardhi inayotumiwa hivi sasa na kituo cha jeshi la anga la Marekani cha Futenma itarejeshewa Japan mwaka 2022 au baadaye. Hatua hizo mbili zimekuja baada ya upinzani mkali wa wakaazi.

LEBANON YATAFUTA WAZIRI MKUU MPYA

Upinzani nchini Lebanon unaoungwa mkono na Saudi Arabia na nchi za magharibi, umejiimarisha katika kinyang'ayiro cha kumpata Waziri mkuu, baada ya mwanasiasa maarufu Walid Jumblatt kumuunga mkono mgombea aliyeteuliwa kuwania wadhifa huo na kuchukua nafasi liyoachwa na mtangulizi wake aliyekuwa akiungwa mkono na chama cha Hezbollah .
Upinzani unaojulikana kama "Muungano wa Machi 14," umemteuwa Tammam Salam kuwa mgombea wake kuchukua nafasi ya waziri mkuu  Najib Mikati aliyejiuzulu mwezi mmoja uliopita. Kuungwa mkono kwa Salam na chama cha Jumblatt cha Progressive Socialist cha jamii ya  Wadruze, kinampa mgombea huyo uungaji mkono wa wabunge 67 kati ya 128. Salam, mwenye umri wa miaka 67, anaonekana kuwa ni mtu mwenye msimamo wa wastani.

BAN KI MOON AILAUMU KOREA KWA MAANDALIZI YAKE

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-moon, amesema kwamba Korea kaskazini imekwenda mbali mno katika vita vyake vya maneno dhidi ya Marekani. Akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Madrid, Uhispania, Ban Ki-moon alisema mgogoro wowote usiohitajika kuhusu rasi ya Korea, utakuwa na athari kubwa.
Jana (Alhamisi) Korea Kaskazini ilitishia vita vya nyuklia dhidi ya Marekani ikisema jeshi lake limeandaa shambulio. Marekani imejibu kwa kuimarisha usalama wa majeshi yake katika eneo la bahari ya Pasifik. Waziri wa ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amesema watafanya kila linalowezekana kujilinda.
Wakati huo huo, Korea Kaskazini imewazuwia wafanyakazi wa Korea kusini kuingia katika eneo la kiwanda cha Kaesong, ikiwa ni siku ya pili mfululizo. Kiwanda hicho kiko maili tatu, ndani ya ardhi ya Korea Kaskazini. Wafanyakazi wanasema hali ni tete.

KAMISHNA POLISI ZANZIBAR ASEMA HAWAKUSHIRIKIANA NA FBI KATIKA UPELELEZI ZANZIBAR

Baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DDP) kulitaka Jeshi la Polisi kumwachia mtuhumiwa Mussa Omar Makame kutokana na ushahidi kutojitosheleza, jeshi hilo sasa limeingia kwenye mkorogano. Wiki iliyopita jeshi hilo lilitangaza kumkamata Makame pamoja na watuhumiwa wengine na kudai kuwa ndiye aliyemuua Paroko wa Parokia ya Mpendae, Padri Evarist Mushi, kwa risasi huku wenzake wakitajwa kuhusika kuwajeruhi viongozi wengine wa dini. Tukio hilo pia liligusiwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Machi, akisema limehusisha vyombo vya nje vikishirikiana na jeshi la polisi nchini. Hata hivyo, jeshi hilo jana lilikana kushirikiana na vyombo vya nje katika uchunguzi huo uliomtia hatiani Makame baada ya ushahidi wao kukataliwa na Mkurugenzi wa Mashataka, Ibrahimu Mzee Ibrahimu.
Katika mahojiano na gazeti hili, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa, alikanusha jeshi la polisi kushirikiana na kikosi cha upelelezi cha Marekani (FBI) ili kumkamata Makame. Kauli yake inakinzana na ile aliyoitoa Machi 23, mwaka huu aliposema uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na makachero wa polisi kwa kushirikiana na wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo. Hatua hiyo ilikuwa ni baada ya jeshi hilo kulaumiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polikarp Kardinali Pengo, kuwa limekuwa kimya kuhusu matukio hayo na kusingizia kwamba yanafanywa na vikundi vya wahuni........................

endelea

Thursday, April 04, 2013

MGOGORO WA MAREKANI NA RUSSIA WAONGEZEKA

Wanadiplomasia wakubwa wa Marekani na Russia wameonyesha kusikitishwa kwao kutokana na kupanuka migogoro kati ya nchi mbili. Hayo yamesemwa na mabalozi wa zamani wa Marekani na Russia ambao wamekutana mjini Moscow kwa ajili ya kikao cha 80 cha kufufua mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi mbili. Wamesema kuwa, Washington na Moscow lazima ziweke pembeni tofauti zao na kukabiliana na changamoto kali za kiuchumi na usalama zinazoyakabili mataifa hayo. Rai iliyokuwa na lengo la kufufua kiwango cha uhusiano kati ya nchi mbili iliyotolewa na Rais Barack Obama wa Marekani, ilikabiliwa na upinzani kutoka kwa serikali ya Russia inayoituhumu Washingtona kuwa inaingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. James Collinsbalozi wa Marekani nchini Russia kuanzia mwaka 1997-2001, na Vladimir Lukin, balozi wa Russia nchini Marekani katika muongo wa 1990, wameeleza kusikitishwa na mivutano inayozidi kupanuka kati ya nchi hizo huku balozi huyo wa zamani ya Russia akiituhumu Washingtona kwa kile alichosema kuwa ni kuzingatia maslahi yake binafsi hasa kuhusiana na kadhia ya Syria.

MAFURIKO YASABABISHA MAAFA MAKUBWA ARGENTINA

Serikali ya Argentina imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya watu 52 kufariki dunia kufuatia mafuriko yaliyotokea siku mbili zilizopita katika mji wa La Plata, mashariki mwa nchi hiyo. Watu wengine 6 wameripotiwa kufariki dunia katika viunga vya mji mkuu, Buenos Aires hapo jana Jumatano. Rais Cristina Kirchner ametembelea eneo lililokumbwa na mafuriko na kusema kuwa, serikali itatuma misaada inayotakiwa na vilevile itatuma maafisa zaidi wa polisi kulinda mali za watu pindi watakapokuwa wakihamishwa. Gavana wa La Plata amesema wengi wa wahanga wa janga hilo la kimaumbile walifikwa na mauti baada ya magari yao kufunikwa ghafla na maji. Amesema pia baadhi ya watu walifariki dunia baada ya kuangukiwa na nyaya za umeme zilizoshika maji. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 2000 wameachwa bila makazi kufuatia mkasa kuo.

RAIS WA SYRIA AIKOSOA JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU

Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameikosoa jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa uamuzi wake wa kuupatia upinzani wa Syria, kiti katika jumuiya hiyo, akisema kuwa chombo hicho kimekosa uhalali. Hayo yamechapishwa katika ukurasa wa Rais Assad kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, baada ya kuhojiwa na vyombo vya habari vya Uturuki. Mwezi uliopita, jumuiya hiyo iliupatia kiti muungano wa upinzani nchini Syria, mwanzoni mwa mkutano wake nchini Qatar, uliohudhuriwa na kiongozi wa zamani wa muungano huo, Ahmed Moaz al-Khatib. Rais Assad amesema uhalali halisi hautolewi na mashirika au maafisa wa kigeni au nchi, bali ni jambo linalotolewa na wananchi.

KAMANDA WA JESHI LA ISRAEL ASEMA IRON DOME HAINA UWEZO KUZUIA MAKOMBORA YA HIZBULLAH


Kufuatia kubadilika mlingano wa kiusalama na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kwa faida ya Hizbullah ya Lebanon na muqawama wa Palestina katika vita na utawala wa Kizayuni, kamanda mmoja wa jeshi la Israel amekiri kuwa ngano ya makombora ya utawala huo haramu ijulikanayo kama "Kuba la Chuma" haina uwezo wa kuzuia mashambulio ya makombora ya Hizbullah. Brigedia Jenerali Kobi Barak, kamanda wa kitengo cha teknolojia na lojistiki katika jeshi la utawala wa Kizayuni amesema makabiliano yoyote yale na Hizbullah ya Lebanon yatapelekea kuenea vita hadi ndani ya Israel. 
Ngao ya Israel iliyotumika kuzuia mshambulizi ya Palestina
Jenerali Barak amesisitiza kwamba vita vyovyote vitakavyotokea siku za usoni na Hizbullah vitaifanya Israel ikabiliwe na mashambulio ya makombora yasiyopungua 1,200 kwa siku ambapo mwanzoni mwa vita hivyo mashambulio ya makombora hayo ya Hizbullah yatakuwa makali mno na yatalenga kwa umakini mkubwa vituo nyeti vya jeshi na hasa kwenye mikusanyiko ya vikosi vya wanajeshi, vituo vya askari wa dhiba na vile vya lojistiki.
Nao makamanda wa kitengo hicho cha teknolojia na lojistiki cha jeshi la utawala wa Kizayuni wameeleza bayana kwamba endapo vitatokea vita, Hizbullah ya Lebanon itavilenga vituo vyote muhimu vya Israel vilivyoko katika ramani na kusababisha askari wengi wa Israel kuuawa. Wakati huohuo Jenerali Eyal Eizenberg, mkuu wa Kamandi ya Ndani ya jeshi la utawala wa Kizayuni ametahadharisha kuwa ngao ya makombora inayojulikana kama "Kuba la Chuma" haina uwezo wa kuyakinga maeneo ya makazi na ya raia na nguvu za makombora ya Hizbullah. Eizenberg amesema Hizbullah inao uwezo wa kufyatua kila siku zaidi ya makombora elfu moja kuelekea Israel. Katika upande mwengine Chuo cha Wanafikra wa Kizayuni cha Begin – Saadat kimekiri kwamba ngao ya makombora ya "Kuba la Chuma" ina kasoro na mushkili mkubwa na wala haina uwezo wa kukabiliana na makombora ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina. Haya yanajiri katika hali ambayo wataalamu wa masuala ya kijeshi wamefichua hivi karibuni kuwa mafanikio ya ngao hiyo wakati wa vita vya Siku nane vya kati ya Novemba 14 hadi 21 mwaka uliopita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya ukanda wa Gaza yalikuwa katika kiwango cha sifuri. Gazeti la New York Times limeandika kuwa kinyume na madai ya Israel kwamba ngao ya "Kuba la Chuma" ilifanikiwa kutungua na kuteketeza kwa kiwango cha asilimia 90 ya makombora ya Palestina wakati wa mashambulio makubwa ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza iliyozingirwa, utafiti uliofanywa na wataalamu wa masuala ya kijeshi nchini Marekani na huko Israel umeonyesha kuwa ngao hiyo iliweza kutungua asilimia 40 tu au chini ya hapo ya kiwango hicho cha makombora ya Hamas. Naye Jeffrey White, mtaalamu wa kituo cha utafiti wa masuala ya Mashariki ya Karibu kilichoko Washington, Marekani amesema ngao ya makombora ya "Kuba la Chuma" haitoweza kamwe kuidhaminia Israel uwezo na nguvu za juu zaidi kistratijia kiasi kwamba endapo mashambulio ya makombora ya Hizbullah ya Lebanon yatakuwa makubwa na ya mtawalia hakuna ngao yoyote ya makombora itakayoweza kuyazuia, stratijia ambayo harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon imetamka bayana kuwa ndiyo itakayoitumia katika vita vijavyo…

DPP NA POLISI WAKOROGANA MAUAJI YA PADRI MUSHI


Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani. Padri Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.

RUSSIA YASISITIZA IRAN KUWA NA NISHATI YA NYUKLIA


Russia imesema kutambuliwa bila masharti haki ya Iran kunufaika na nishati ya nyuklia ndio ufunguo wa kutatuliwa hitilafu kati ya nchi za Magharibi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Igor Morgulov ambaye ameongeza kuwa, nchi yake inashirikiana kwa karibu na China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Ujerumani kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Nchi hizo sita ndio wanachama wa kundi la 5+1 linalofanya mazungumzo na Iran. Ameelezea matumaini yake kuwa mazungumzo yajayo kati ya Iran na 5+1 yatazaa matunda. Morgulov amesisitiza kuwa Russia ina mtazamo sawa na China katika kupinga vikwazo vya upande mmoja na mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Duru ya pili ya mazungumzo ya Iran na 5+1 inatarajiwa kufanyika Almaty Kazakhstan kuanzia Aprili 5 hadi 6.

MAREKANI NAYO YAJIANDAA KWA AJILI YA KOREA

Jeshi la marekani likijiandaa kwa ajili ya Korea

Marekani imepeleka mitambo ya kukinga makombora katika kisiwa cha Guam katika bahari ya Pacific huku Korea Kaskazini ikitishia kurusha makombora ya nuklia nchini humo. Idara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema kuwa mitambo hiyo itakuwa tayari katika kipindi cha wiki kadhaa , na kuongeza kwa zana za kivita ambazo zilipelekwa katika eneo hilo.  Korea Kaskazini ilitaja kisiwa cha Guam kuwa miongoni mwa maeneo yanayolengwa kwa mashambulizi ikiwemo Hawaii na Marekani.
Korea Kaskazini haidhaniwi kuwa na teknolojia ya kutosha kushambulia Marekani kwa zana za nuklia au makombora ya masafa marefu. Korea Kaskazini inasema kwamba imewaweka wanajeshi wake, tayari kwa shambulio dhidi ya Marekani ikiwemo kutumia zana za nyukilia. Taarifa hii imejiri wakati Marekani imeimarisha mitambo yake ya kukinga makombora katika kisiwa cha Guam kilichoko bahari ya Pacific. Idara ya ulinzi ya Korea Kaskazini imesema inatoa taarifa kwa Marekani kwamba jeshi lipo tayari kushambulia bila huruma, kile imetaja kama vitisho vya Marekani dhidi yake.
Utawala wa Pyongyang ulionekana kukerwa na hatua ya Marekani ya hivi maajuzi ambapo wanajeshi wake walifanya mafunzo ya pamoja na ambayo yalihusisha utumizi wa zana za kivita. Hata hivyo wachanganuzi wamesema Korea Kaskazini haina silaha ambazo zinaweza kushambulia ardhi ya Marekani, japo katika siku za karibuni imefanya majaribio ya makombora ua masafa marefu. Hapo jana Jumatano, Korea Kaskazini iliwazuia wafanyikazi wa Korea Kusini kuvuka mpaka kuelekea katika viwanda vya pamoja vinavyomilikiwa na nchi mbili, na hivyo kukatiza uhusiano uliobaki kati yake na Kusini. Baadhi wanaona malumbano ya sasa kama hatua ya Korea Kaskazini kushinikiza Marekani kuanzisha mazungumzo ya pamoja ambayo yataafikia mkataba wa amani.

APPLE APP STORE ALERT


Important Warning!


As-Salamu 'Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatu

A new version of the Quran has been released on the Apple APP STORE by the kafir ahmadiyyah/qadiani community. The name of the app is "The Holy Quran, Arabic text and English translation". "Translated by Maulvi Sher Ali, Ahmadiyya Muslim Community" has been clearly mentioned in the app information in iPhone App Store.

Please make Muslims aware not to buy/download this app!

Boycott this product as the contents of this application are incorrect/misleading & contradict the teachings of the Holy Quran and Hadith.

URUSI YAWAPELEKEA MSAADA WAKIMBIZI WA LEBANON

Ndege ya Urusi iliyobeba tani 36 ya misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Syria walioko Lebanon ilitua leo mjini Beirut ikiwa ndiyo msaada wa kwanza kutoka Urusi ambayo imekuwa ikimuunga mkono Rais Bashar al-Assad katika vita vya Syria vya miaka miwili. Balozi wa Urusi nchini Lebanon, Alexander Zasypkin, amesema ndege hiyo ilibeba mablanketi, vyakula, mitambo ya Jenereta kuwapa wakimbizi nchini humo ambako Umoja wa Mataifa unasema kuna wakimbizi karibu laki nne kutoka Syria. Urusi imekuwa ikimuunga mkono Assad kwa kupinga vikwazo dhidi ya utawala wake na kuwekewa vikwazo vya silaha kwa kupiga kura ya turufu katika mikutano ya Umoja wa Mataifa. Idadi ya wakimbizi kutoka Syria nchini Lebanon imekuwa kubwa na kuzua wasiwasi katika taifa lililo na raia milioni nne ambalo waziri mkuu wake alijiuzulu mwezi uliopita kutokana na mizozo katika baraza la mawaziri iliyochochewa na vita vya Syria.