Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani. Padri Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO