YAJUE MAKOSA MBALIMBALI YAFANYIKAYO KATIKA IBADA YA HIJJA
IHRAMU NA MAKOSA YAKE
Imethibiti katika Sahihul
Bukhari na Muslimu kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) amewapangia
waislamu wa sehemu na pembe mbalimbali za dunia sehemu zao za kuhirimia
wanapotaka kufanya ibada ya Hijja au Umrah. Sehemu hizo ni kama zifuatazo:
1. Dhul Hulayfah kwa watu wa Madiynah
2. Juh’fa kwa watu watokao Shamu
3. Qarnul Manaazil kwa watu wa Najd
4. Yalamlam kwa watu watokao Yemen
baadhi ya Mahujaji wanaokwenda moja kwa
moja Makkah badala ya kuhirimia katika sehemu hizo wakiwa katika ndege au
katika usafiri wowote walionao na si kusubiri hadi wateremke uwanja wa ndege wa
Jiddah ndipo wahirimie. Haya ni makosa na ni kukhaalifu amri ya Mtume (Swalla
Llaahu ‘Alayhi Wasallama).
MAKOSA YA
KIVITENDO YANAYOAMBATANA NA KUTUFU AU KUZUNGUKA AL-KA’ABAH
1.Kuanza kuzunguka Al-Ka’abah kabla ya kufika sehemu ya jiwe jeusi, na
kwa sasa kuna alama ya mstari maalumu inayoonyesha lilipo jiwe jeusi na kama ni
usiku kuna taa ya rangi maalumu taa ya kijani yenye kuonyesha lilipo jiwe jeusi.
2.
Kutufu
ndani ya eneo linaloitwa Hijr kutokana na msongamano mkubwa wa watu. Kimsingi
hili ni kosa kubwa kwa kuwa eneo la Hijr kishari’ah liko ndani ya Al-Ka’abah na
tawafu inatakiwa iwe nje ya Al-Ka’abah na sio ndani ya Al-Ka’abah. Kwa hiyo kwa
kupita ndani ya Hijr unapotufu unakuwa umetufu katika sehemu ya Al-Ka’abah na
si Al-Ka’abah yote ambayo ndiyo inayotakiwa.
3.
Kukimbia kimbia katika Tawafu zote saba.
4.
Kusongamana na kupigana vikumbo kwa
ajili ya kulifikia jiwe jeusi ili kulibusu, jambo ambalo mara nyingine
husababisha watu kurushiana matusi na hata kupigana na kwa kufanya hivyo wakawa
wanaivunjia heshima nyumba tukufu ya Allaah. Kutufu kwa namna hii kunapunguza
daraja ya kutufu bali mara nyingine hata kuipunguza tija ibada nzima ya Hijja
5.
Itikadi ya baadhi ya Mahujaji kuwa jiwe
jeusi linanufaisha au linadhuru kwa dhati yake hivyo utawakuta pindi
wanapoliamkua wanajipangusa katika viwiliwili vyao au wanawapangusa watoto wao
walionao katika ibada ya Hijja au ‘Umrah. Na
yote haya ni kutokana na ujinga na ni upotevu wa wazi.
6.
Baadhi ya Mahujaji kung’ang’ania nguzo zote
za Al-Ka’abah na mara nyingine wakawa wanazishika kuta zote za Al-Ka’abah na
hata mara nyingine kuing’ang’ania sana Al-Ka’abah kwa kila sehemu au wakawa
kila wakiigusa Al-Ka’abah wakawa wanajipangusia. Na huu ni ujinga na upotevu wa
wazi.
MAKOSA YA KUSIMAMA KATIKA VIWANJA VYA
‘ARAFAH
1. Kufika mapema katika sehemu viliko viwanja vya ‘Arafah lakini wakawa
nje ya Viwanja vya ‘Arafah hadi jua likazama. Kisha wakaondoka kwenda
Muzdalifah hali ya kuwa hawajasimama katika Viwanja vya ‘Arafah. Na hili ni
kosa kubwa ambalo linapotokea mtu anakuwa ameikosa Hijja kwani kusimama katika
viwanja vya ‘Arafah ndiyo nguzo kubwa ya Hijja ambayo Hijja ya mtu haiswihi
hadi mtu awe amesimama katika viwanja vya ‘Arafah. Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama) amesema kuwa: “Hijja ni ‘Arafah, atakayekuja usiku wa
baada ya Mahujaji kusimama ‘Arafah lakini kabla ya kuchomoza Alfajiri ya tarehe
10 atakuwa ameidiriki ‘Arafah na Hijja yake itakuwa sahihi”.
2. Kuondoka kwao katika viwanja vya ‘Arafah kabla ya kuzama jua. Na hii
kosa kubwa tena ni haramu kwa kuwa kufanya hivyo ni kukhalifu amri ya Mtume
(Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kwani yeye Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama) alikaa katika viwanja vya ‘Arafah hadi jua likazama na giza likaanza
kuingia ndipo akaondoka kuelekea Muzdalifah. Ama kuondoka kabla ya jua kuzama
hii ni katika vitendo vya kijahiliya alivyokataza Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama).
3. Baadhi ya Mahujaji kuelekea Jabal ‘Arafah wakati wa kuomba du’aa hata
kama kwa wao kufanya hivyo wanakipa Qiblah mgongo au kinakuwa upande wa kulia
au wa kushoto. Na hili ni kinyume na mwendo wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama), kwani Sunnah wakati wa kuomba du’aa hapo ni kuelekea Qiblah na si
Jabal ‘Arafah au kilima cha ‘Arafah.
KUTUPA MAWE
NA MAKOSA YAKE
1. Baadhi ya watu kuitakidi kuwa ni lazima wachukue vijiwe kutoka Muzdalifah
tu. Kwa itikadi yao hiyo wakawa wanajikalifisha na kuzichosha nafsi zao kwa
kufanya hivyo.
2. Itikadi yao kuwa wanapopiga minara ile ya Jamarati wanakuwa wanampiga Shetani.
Hivyo mara nyingine utawasikia wakisema kuwa tumempiga Shetani mkubwa au mdogo
au tumempiga baba wa Mashetani wakimaanisha ule mnara mkubwa yaani Jamaratul
‘Aqabah na mfano wa hivi. Na mingi ya mifano ambayo haifai katika sehemu hii
tukufu.
3. Kutupa mawe makubwa, viatu na hata miti. Hili ni kosa kubwa na
linalokhalifu mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) ya kauli na
vitendo.
4. Kuziendea sehemu za kupiga mawe kwa vurugu na papara bila hata kuwahurumia
waja wengine wa Allaah, jambo ambalo husababisha maudhi kwa Waislamu wengine na
hata mara nyingine kutukanana na kupigana au hata vifo. Hali hii hugeuza sehemu
hizi tukufu na kuwa kama sehemu za vurugu, kutukanana na mapambano.
5. Kuacha kwao kuomba baada ya kutupa mawe mnara wa kwanza na wa pili katika
yale masiku yanayoitwa Ayyaamu Ttashriyq au masiku matatu ya kutanda nyama.
Ilivyothibiti ni kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) alikuwa pindi
akimaliza kupiga mawe minara miwili ya kwanza alikuwa akisimama baada ya kupiga
kila mmoja ya minara hii miwili ya mwanzo akielekea Qiblah na kunyanyua mikono
yake na kuomba du’aa ndefu.
6. Kutupa mawe yote kwa mkupuo mmoja. Na hili ni kosa kubwa sana. Wanachuoni
wanasema kuwa ikiwa mtu atatupa mawe yote kwa mkupuo mmoja basi hiyo
itahesabiwa kuwa ametupa jiwe moja.
7. Kuzidisha kwao du’aa wakati wa kutupa mawe, yaani du’aa ambazo
hazikuthibiti wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) kama kusema
kwao; “Ee Mwenyezi Mungu yajaalie mawe hayo kuwa ni radhi kwako na ni ghadhabu
kwa Shetani”. Mara nyingine wao huacha Takbira iliyothibiti kutoka kwa Mtume
(Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama). Na haya ni makosa kishari’ah.
8. Watu wengine kutaka kutupiwa mawe hata kama hawana udhuru wa kishari’ah.
Hii inaweza kuwa ni kwa sababu ya kukwepa zahma na misongamano. Na hili
linakuwa ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama) na
alivyoagiza.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO