Friday, November 30, 2012

NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR' AN. Part. 1

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

 
كيف تحفظ القرآن في عشر خطوات – حسن أحمد بن أحمد همام

 
Haifichiki kwa kila Muislam ubora wa kuhifadhi Qur-aan Tukufu na fadhla za aliyeihifadhi.
 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
 
“Wale tuliowapa kitabu (Taurati, injili, Zaburi…) wakakisoma kama ipasavyo kukisoma (bila ya kupotoa tafsiri yake wala kutoa hili na kutia lile), hao huiamini hii (Qur-aan wakasilimu). Na wanaokikanusha (hicho kitabu chao wakapinduapindua tafsiri yake na wakaongeza na wakapunguza), basi hao ndio wenye hasara.” Al-Baqarah: 121.
 


“Kisha Tumewarithisha, (tumewapa) kitabu (hiki cha Qur-aan) wale Tuliowachagua miongoni mwao wanaodhulumu nafsi zao (kwa kuwa na maasia mengi kuliko mema). Na wako wa kati na kati, (wana mema kuliko mema). Na wako wanaokwenda mbele kabisa katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.” Faatwir: 32.

 
“Kwa yakini wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Swalah, na katika yale Tuliyowapa wakatoa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai (faida ya) biashara isiyododa (isiyobaga).” Faatwir: 29.

 
Katika hizi Aayah ni dalili ya ubora ya watu wa Qur-aan na kufaulu biashara yao na Allaah.
Ama Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) ni nyingi tunachukua zifuatazo:


 
kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):


 
“Hakuna hasadi ila katika vitu viwili; mtu ambaye Allaah Amempa hekima (elimu) anaisimamia usiku na mchana, na mtu ambaye Allaah Amempa mali naye anatoa sadaka usiku na mchana.” Muslim
 


Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Afaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema, anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
 
“Mbora wenu ni aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” Al-Bukhaariy
 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
 

“Ataambiwa Swaahib al-Qur-aan soma kama ulivyokuwa ukisoma duniani hakika daraja yako peponi ni mwisho wa Aayah utakayosoma.” At-Tirmidhiy
 

Kutoka kwa Sahl bin Mu’adh kutoka kwa baba yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
 

“Mwenye kusoma Qur-aan na akaifanyia kazi yaliyomo atavalishwa mzazi wake taji siku ya kiyama mng’aro wake ni bora kuliko mwangaza wa jua katika nyumba za dunia lau ingekuwa kwenu mnadhani vipi kwa aliyeifanyia kazi.” Abu Daawuud
 

Imepokewa katika Al-Bukhaariy kwamba walikuwa wanatangulizwa watu wa Qur-aan (Ahlul Qur-aan) kuliko wengine katika Swallah na katika kuwazika mashahidi. Pia kuna mtu alimuoa mwanamke kwa Qur-aan aliyokuwa nayo kama mahari.
 

KUHIFADHI QUR-AAN NI KHASWA KWA UMMAH HUU

Allaah Amejaalia Ummah huu kuwa bora kuliko Ummah zingine na Akajaalia wepesi kuhifadhi  Kitabu hiki kimaandishi na kifuani.
 
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
 
“Bali hizi ni Aayah waziwazi (zinazokubaliwa) katika vifua vya wale waliopewa ilimu, na hawazikatai Aayah Zetu isipokuwa madhalimu (wa nafsi zao).” Al-‘Ankabuut: 49
 
Na imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy;
 
“Na imeteremshwa kwako Kitabu kisichooshwa na maji unasoma ukiwa umelala na ukiwa macho.” Muslim
 
Itaendelea Ijumaa ijayo inshaa -Allah........................

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO