Russia na China zimeitahadharisha Marekani kutozidisha chokochoko za kijeshi katika Peninsula ya Korea na kwamba hali hiyo huenda ikalitumbukiza eneo hilo kwenye ukosefu wa amani. Taarifa iliyotolewa leo na Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia imeeleza kuwa, hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini huenda zikaleta maafa makubwa. Wizara ya Mambo ya Nje ya China pia imezitaka pande mbili kufanya juhudi za kupunguza hali ya wasiwasi na kuimarisha amani na uthabiti katika Peninsula ya Korea. Hayo yamejiri baada ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kutangaza kuwa nchi yake imeweka makombora yake tayari kushambulia Marekani, vituo vya kijeshi vya Pasifiki, vikiwemo vya Hawai na Guam pamoja na vya Korea Kusini. Pyongyang imetangaza hayo baada ya Marekani kupeleka jana huko Korea Kusini ndege mbili zenye kubebea vichwa vya nyuklia aina ya B2 kwa madai ya kufanya maneva ya kijeshi katika Peninsula ya Korea. Vilevile Washington na Seoul jana zilisaini makubaliano ya kijeshi, yanayoziruhusu nchi hizo mbili kujibu hata vitisho vya kiwango cha chini vya Korea Kaskazini.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO