Wednesday, December 19, 2012

IRAN YATAHADHARISHA NCHI ZA KIARABU KUZIDI KUNUNUA SILAHA TOKA NCHI ZA MAGHARIBI

Njama za madola ya Magharibi za kujaribu kuionyesha Iran kuwa ni tishio, zimekuwa kisingizio kizuri cha madola hayo cha kutiliana saini mikataba ya silaha ya mabilioni ya dola na nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati. Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, madola hayo yamekuwa yakitia kibindoni mabilioni ya dola yanayozipata kutokana na kuziuzia silaha nchi za Kiarabu baada ya kuzionyesha kuwa Iran ni tishio kwa usalama wa eneo hili. Katika toleo lake la hivi karibuni gazeti la Washington Post sanjari na kuelezea sehemu kubwa ya mikataba hiyo ya silaha liliandika kuwa, hatua ya Marekani ya kuwapatia silaha washirika wake katika Ghuba ya Uajemi imechukua sura hatari na tata sana. Katika ripoti hiyo imedaiwa kwamba, vita pekee tarajiwa vya Saudi Arabia, Imarati na washirika wengine wa Marekani katika Mashariki ya Kati vitakuwa na Iran; kwani yamkini nchi za Ghuba ya Uajemi zikashiriki katika mashambulio ya Marekani dhidi ya taasisi za nyuklia za Tehran. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, fikra inayotawala katika senario hii ni kwamba, Iran ikiwa na lengo la kujibu aina yoyote ile ya hujuma dhidi ya usalama wake itashambulia vituo vya kijeshi vitakavyotumiwa na Marekani katika Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kuishambulia Tehran; jambo ambalo bila ya shaka litazitumbukiza nchi hizo katika sokomoko na machafuko na yamkini nchi hizo zikanasa katika kinamasi hicho. Marekani na madola ya Magharibi awali huwa yanazusha mgogoro na kulionyesha eneo la Mashariki ya Kati kwamba linakabiliwa na tishio la ukosefu wa amani na baadaye hutumia kisingizio hicho kuziuzia silaha za kisasa nchi za Kiarabu za eneo hili. Nukta muhimu na ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, nchi nne za Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambazo zimekuwa mstari wa mbele kupiga upatu kwamba, Iran ni tishio kwa usalama wa Mashariki ya Kati ndizo zinazoshikilia rekodi ya kuuza silaha kwa wingi kwa nchi za Kiarabu. Licha ya kuwa mashindano ya kumiliki silaha katika Mashariki ya Kati yamekuwa ya kupanda na kushuka, lakini baada ya tukio la Septemba 11 mwenendo huo ulishika kasi zaidi; ambapo ununuzi wa zana za kijeshi kwa baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu ulichukua mkondo wa ajabu sana. Baada ya China, India na Korea Kusini, nchi ya Imarati ni ya nne kwa kununua silaha kutoka nje. Asilimia 60 ya silaha za Imarati zinanunuliwa kutoka Marekani. Katika hali ambayo, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hususan Uingereza zinakabiliwa na hali mbaya ya kuporomoka uchumi wake, zimekimbilia soko la kuziuzia silaha nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, na kwa muktadha huo zimepelekea kutokea ushindani mkubwa katika soko kubwa la uuzaji silaha katika nchi za Kiarabu za eneo hili. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, madola ya Magharibi yanayoisingizia Iran kuwa tishio kwa usalama wa Mashariki ya Kati, kimsingi yenyewe ndio chanzo cha ukosefu wa amani katika eneo hili.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO