Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu
OIC imelaani na kulalamikia uamuzi wa karibuni hivi wa utawala wa
Kizayuni wa kutaka kujenga nyumba mpya 3000 huko katika Ukingo wa Magharibi wa
Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu. Ikmaluddin Ehsanoghlo Katibu Mkuu wa
jumuiya ya OIC amelaani vikali hatua hiyo ya Israel ya kutaka kujenga nyumba
mpya nyingine za walowezi wa Kizayuni na kuitaja kuwa ni changamoto
inayoikabili jamii ya kimataifa. Ikijibu kupandishwa hadhi Palestina na kuwa
nchi mtazamaji isiyo mwanachama wa Umoja wa Mataifa serikali ya utawala wa
Kizayuni imetangaza kuwa itajenga nyumba mpya elfu tatu huko mashariki mwa Quds
inayokaliwa kwa mabavu na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Gazeti la
Kizayuni la Jerusalem Post pia limemnukuu Ehud Olmert waziri mkuu wa zamani wa
Israel na kuandika kuwa kupasishwa ujenzi wa nyumba za walowezi elfu tatu huko
Baitul Muqaddas na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni dharau kubwa kwa
Obama. Hii ni kwa sababu mara hii lobi ya Marekani imeshindwa kuzuia
kutambuliwa nchi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa.
Baada ya nchi nyingi
wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kuunga mkono
kupandishwa hadhi ya Palestina na kuwa nchi mtazamaji isiyo mwanachama katika
Umoja wa Mataifa, hivi sasa Wapalestina wanaweza rasmi kuwasilisha mashtaka na
malalamiko yao kwa taasisi za Umoja wa Mataifa dhidi ya Israel. Viongozi wa
Palestina wanasema kuwa kuendelea ujenzi na upanuzi wa vitongoji vya Israel
katika ardhi za Palestina ni sababu tosha inayokubalika ili kuweza kuwasilisha
faili hilo kwa Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na baada ya
hapo taasisi za kimataifa zitekeleze wadhifa na nafasi yake mkabala na
mashambulizi na ukiukaji wa haki za raia wa Palestina unaofanywa na Israel
katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Hadi kufikia sasa makumi ya maazimio na hati zimepasishwa katika
Umoja wa Mataifa zikilaani siasa za mabavu na za kupenda vita za utawala wa
Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa. Mradi wa kujenga vitongoji
vya walowezi ulianza tangu mwaka 1967 baada ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu
Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds ya Mashariki na Ukanda wa Ghaza na
ujenzi huo umekuwa ukiendelea hadi sasa. Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
awali vilijengwa kandokando ya ardhi za Palestina na taratibu ujenzi huo
umekuwa ukizidi kupanuliwa na sasa umefikia ndani kabisa ya ardhi za Palestina.
Utawala wa Kizayuni unajenga na kupanua zaidi vitongoji hivyo kwa malengo
mbalimbali ambapo moja kati ya hayo ni kutaka kuitenganisha miji na maeneo ya
Wapalestina na vile vile kuizingira miji hiyo.
Nyumba za walowezi wa Kizayuni
zinajengwa katika ardhi za Wapalestina ili kukwamisha kuasisiwa nchi huru ya
Palestina. Israel imejenga vitongoji vingi vya walowezi wa Kizayuni huko Quds
na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika miongo minne ya hivi
karibuni lengo likiwa ni kubadili muundo wa kijamii na kijiografia wa maeneo
hayo. Katika mazingira hayo Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu sambamba
na taasisi nyingine za kimataifa zinalaani siasa hizo za Israel zilizo dhidi ya
binadamu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO