MKUU WA KJIASUSI ISRAEL INAENDELEA KUMOMONYOKA
Mkuu wa zamani wa Taasisi ya Kijasusi na Usalama wa Ndani ya utawala wa Kizayuni (SHABAK) amesisitiza kwamba, Israel inaendelea kumomonyoka ndani kwa ndani. Yuval Diskin amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la United Press na kuchapishwa jana na gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot na kumlaumu vikali Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akisema kuwa Benjamin Netanyahu ameshindwa kuchukua maamuzi muhimu kuhusu Palestina na Iran kama ambavyo pia hawezi kutekeleza vizuri majukumu yake na hivyo anahatarisha kusambaratika Israel. Vile vile amepinga vikali jaribio lolote la kuishambulia Iran na kusema kuwa hata kama kwa mfano Wairani watamiliki bomu la nyuklia, bado suala hilo halitakuwa na umuhimu wa kwanza kwa utawala wa Kizayuni kwani kuna hatari kubwa zaidi inayoikabili Israel nayo ni kusambaratika ndani kwa ndani. Diskin ambaye alikuwa mkuu wa Taasisi ya Ujasusi na Usalama wa Ndani ya utawala wa Kizayuni baina ya mwaka 2005 hadi 2011, pia amesema kuwa, Benjamin Netanyahu na Ehud Barak, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni muda wote wanajali maslahi yao binafsi na kila wanachosema kinalenga tu kulinda vyeo vyao hata kama itakuwa ni kwa madhara ya Israel. Amesema kuhusu siasa za utawala wa Kizayuni kuhusu Wapalestina kwamba hivi sasa mazungumzo kati ya Israel na Mamlaka ya Ndani ya Palestina yamekwama lakini wakati huo huo viongozi wa Israel wanaendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vinavyolalamikiwa dunia nzima. Mkuu huyo wa zamani wa taasisi ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni vile vile amekiri kuwa nguvu za wanamapambano wa Palestina zimeongezeka sana na kusema kwamba miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuwa wanamapambano wa Palestina wamezidi kupata nguvu ni kulazimika Israel kuwaachia huru mateka wa Palestina, kushindwa utawala wa Kizayuni kufanikisha malengo yake katika vita vya Ghaza na kupata nguvu Khalid Mash'al, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS kutembelea Ghaza na kutothubutu Israel kumfanya chochote. Aidha amesema kuwa, malalamiko makubwa hasa ya vijana katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ni hatari nyingine inayoukabili utawala wa Kizayuni. Ameashiria pia jinsi asilimia 37 ya wakazi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu walivyo na nia ya kuhama ardhi hizo na kusema kuwa suala hilo ni hatari zaidi kwa Israel na ni mithili ya bomu ambalo linaripuka pole pole na mwishowe litaingamiza kabisa Israel. Vile vile amewalaumu viongozi wapenda vita wa utawala wa Kizayuni akiwemo Shaul Mofaz mkuu wa chama cha Kadima na kusema kuwa, siasa za kupenda vita na kueneza chuki dhidi ya Wapalestina na Iran zimewafanya walimwengu waichukie Israel. Mkuu huyo wa zamani wa Taasisi ya Kijasusi na Usalama wa Ndani ya utawala wa Kizayuni Shabak amekosoa pia kushindwa viongozi wa Israel kuwatatulia watu matatizo yao makubwa ya kiuchumi. Matamshi hayo ni sehemu ndogo tu ya malubambano makubwa yanayoripotiwa kila leo kati ya viongozi wa utawala wa Kizayuni na bila ya shaka mambo hayo ndiyo yatakayoharakisha kusambaratika kikamilifu utawala dhalimu wa Kizayuni.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO