Waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamedhibiti miji mingine miwili ya katikati mwa nchi hiyo na hivyo kuzidi kuwa tishio kwa serikali ya Rais Francois Bozize wa nchi hiyo. Habari kutoka Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zinasema kuwa, miji ya Alindao na Kouango ya katikati mwa nchi hiyo inadhibitiwa na wapiganaji wa muungano wa waasi wa SELEKA. Josue Binoua, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, licha ya serikali kutangaza utayarifu wake wa kufanya mazungumzo na waasi wa SELEKA, lakini waasi hao wanaendeleza mapigano na utumiaji mabavu.
Mazungumzo baina ya waasi hao na serikali ya Rais Bozize yamepangwa kufanyika tarehe 8 ya mwezi huu huko Libreville, Gabon. Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewataka waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuacha kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui na badala yake kukaa katika meza moja ya mazungumzo na serikali. Katika upande mwingine, Mfuko wa Watoto Duniani UNICEF umeitaka serikali ya Bangui na waasi wa SELEKA kuacha kuwatumia watoto kwenye mapigano ya nchini humo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO