Rais Barack Obama wa Marekani amesisitiza katika duru yake ya pili
ya urais nchini humo juu ya udiplomasia wa "mashinikizo na vikwazo"
na amempa makamu wake Jo Biden jukumu la kufuatilia kadhia ya nyuklia ya Iran.
Biden ambaye ameelekea Munich, Ujerumani kwa ajili ya kushiriki katika kikao
cha usalama, ameeleza kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa
moja na Iran na kwamba Washington ina mpango ambao kwa mujibu wa madai yake
unaweza ukafungua njia ya kutatuliwa kidiplomasia kadhia ya nyuklia ya Iran.
Biden amesema pia kuwa Marekani haitairuhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia na
kwamba mlango wa mazungumzo ya amani na Tehran hautakuwa wazi milele.
Matamshi hayo ya Joe Biden
yamekaribishwa na kuungwa mkono na viongozi wa Umoja wa Ulaya akiwemo Catherine
Ashton, Mkuu wa Siasa za Nje wa umoja huo na Guido Westewelle, Waziri wa Mambo
ya Nje wa Ujerumani. Matamshi ya kiongozi huyo wa White House yanaonesha kwamba
Marekani inaendeleza siasa zake za propaganda chafu dhidi ya Iran na kwamba
Tehran kwa mujibu wa mtazamo wa Wamagharibi, ni mtuhumiwa mkubwa; kwa sababu
hiyo mazungumzo ya aina yoyote ile na Iran yanapaswa kufanyika kwa mujibu wa
madai hayo yasiyo na msingi. Kwa hakika hatua hiyo ya Marekani ina lengo la
kuidhihirisha serikali ya Washington kuwa ina nia njema ya kutaka kutatua
kadhia ya nyuklia ya Iran kwa njia za kidiplomasia.
Ukweli wa mambo ni kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel
zimepanga njama kabambe na harakati kubwa kwa ajili ya kikao cha Munich na
zinafanya juhudi ili kunufaika na fursa hiyo dhidi ya miradi ya kuzalisha
nishati ya nyuklia ya Iran. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika hotuba yake
kwenye mkutano wa Munich, Makamu wa Rais wa Marekani amefanya jitihada kubwa za
kuchafua sura ya Iran badala ya kuzungumzia haki za nyuklia za Jamhuri ya
Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Iran wamekosoa vikali
suala la kubadilishwa mahali na tarehe ya kufanyika mazungumzo kati ya Tehran
na kundi la 5+1 na hatua ya nchi za Magharibi ya kuchapisha habari za uwongo
kuhusiana na suala hilo. Tangu karibu miezi 8 iliyopita yaani tangu baada ya
kikao cha Moscow, Iran ilikuwa imejiandaa kufanya duru mpya ya mazungumzo,
lakini upande wa Magharibi umekataa kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu
ambazo Iran pia haizijui.
Suala kuu hapa si wakati wa kufanyika mazungumzo hayo wala mahala
gani yatafanyika, bali ni jambo jingine ambalo ni kuwa, baadhi ya wanachama wa
kundi la 5+1 hawako tayari kufanya mazungumzo hayo. Viongozi wa Marekani
wameelewa kuwa Russia na China hazichezi tena katika uwanja wa udiplomasia wa
Magharibi kama ilivyokuwa huko nyuma na migongano ya mitazamo ya Kremlin na
Peking na ile ya Marekani imepanuka na kugusa masuala mengi kuanzia mgogoro wa
Syria hadi kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa sababu hiyo maafisa wa serikali ya
Marekani wametoa fikra ya kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Iran. Hatua
hiyo imechukuliwa kwa sababu kadhaa. Kwanza ni kuwa Marekani na baadhi ya
waitifaki wake wa Ulaya walitarajia kuwa vikwazo vyao dhidi ya Iran vitazusha
uasi na machafuko ya kijamii. Hata hivyo badala ya kuwafanya wananchi wa Iran
waichukie serikali na mfumo wao, vikwazo hivyo vimewafanya wazichukie zaidi
nchi za Magharibi.
Sababu ya pili ni kuwa tofauti na makelele yake ya kipropaganda,
Marekani haijaweza kubuni stratijia ya maana kwa ajili ya kuanza mazungumzo na
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu tunapotazama mwenendo wa
Marekani kuhusu Iran tutatambua kuwa madai ya kutaka kufanya mazungumzo ya moja
kwa moja na Tehran hayana maana yoyote. Ukweli ni kuwa lengo la Marekani katika
harakati yake hiyo ni kutaka kubadili mlingano wa kimataifa kuhusu suala la
mazungumzo na Iran. Duru za kisiasa za nchi za Magharibi pia zinatumia
propaganda za vyombo vya habari kuonesha kuwa Iran haiko tayari kufanya
mazungumzo na kwa njia hiyo itambulike kuwa ni tishio kwa jamii ya
kimataifa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO