Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF umeitambua rasmi serikali ya Somalia, na kufungua pazia la kuboreshwa uhusiano wa pande mbili, baada ya IMF kusitisha uhusiano wake na nchi hiyo yapata miaka 22 iliyopita. Taarifa ya IMF imeeleza kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kutokana na uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na taasisi nyingine za kimataifa kwa serikali inayoongozwa na Rais Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, hivi sasa nchi hiyo ina madeni ya dola milioni 352 hivyo haina sifa ya kupokea misaada mipya ya kifedha kutoka mfuko huo. Tokea mwaka 1991, baada ya kuangushwa utawala wa Muhammad Siad Barre, Somalia ilikuwa haina serikali kuu na hali hiyo ilisababisha nchi hiyo kukumbwa na machafuko. Serikali ya Rais Hassan Sheikh Mahmoud iliingia madarakani mwezi Septemba mwaka 2012 na mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisimamisha kwa muda wa mwaka mmoja vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO