Tuesday, April 02, 2013

KOREA KUZINDUA MRADI MPYA WA NYKLIA


Korea Kaskazini imetangaza kuwa itazindua upya kituo chake kikuu cha nyuklia katika eneo la Yongbyon huku ngoma za vita zikiendelea kupigwa katika Peninsula ya Korea. Shirika rasmi la habari la nchi hiyo KCNA limesema kituo cha kurutubisha madini ya urani na tanuri nyuklia tano ambazo zilifungwa mwaka 2007 kama sehemu ya mkataba wa kuangamiza silaha, zitaanza kufanya kazi upya katika Taasisi ya Nyuklia ya Yongbyon.
Msemaji wa mirdai ya nishati ya nyuklia ya Korea Kaskazini amesema hatua hiyo ni katika fremu ya sera za kujiimarisha kwa zana za nyuklia na vile vile kutatua matatizo sugu ya ukosefu wa umeme. Jumatatu Korea Kaskazini ilitangaza kuwa sera zake kuu kitaifa ni kuwa na uchumi wenye nguvu na kuzalisha silaha za nyuklia. Siku hiyo hiyo Marekani ilitangaza kutuma meli zake za kivita katika Peninsula ya Korea kwa lengo la kukabiliana na makombora ya Korea Kaskazini. Aidha ndege za kivita za Marekani aina ya F-22 zenye uwezo wa kukwepa rada zimefanya mazoezi katika eneo hilo. Katika upande mwingine Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amesema nchi yake itajibu haraka hujuma kutoka nchi jirani ya Korea Kaskazini. Korea Kusini na Korea Kaskazini ziliwahi kupigana vita vikali kati ya mwaka 1950 – 1953 na kisha kusaini makubaliano ya usitishaji vita kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO