Msemaji wa Serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina inayoongozwa na Hamas amesema kuwa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas ni muungaji mkono mkubwa wa mzingiro kidhulma unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Twahir an Nunu Msemaji wa serikali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina amesema kuwa, utendaji wa Mahmoud Abbas unaonyesha wazi kwamba anafanya njama za kudumishwa mzingiro uliowekwa na Israel dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Gaza. An Nunu ameongeza kuwa, 'Abu Mazin' aliitaka serikali ya Marekani imshinikize Raccep Tayep Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki afute safari yake huko Gaza mwezi ujao.
Wakati huohuo Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema kuwa, takwa la John Kerry Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani kwa Erdogan linaonyesha kuwepo makubaliano kati ya Kerry na Mahmoud Abbas. Katika mazungumzo ya viongozi hao wawili siku kadhaa zilizopita, Kerry alimtaka Erdogan afute safari yake katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, utawala wa Israel ulishadidisha mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza mwaka 2007, baada ya Hamas kujipatia ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa bunge la Palestina.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO