Tuesday, April 02, 2013

VIONGOZI WA UAMSHO WAFUTIWA KESI


MAHAKAMA ya Mwanakwerekwe, Zanzibar imefuta kesi iliyokuwa ikiwakabili viongozi kumi wa Jumuiya ya Uamsho, visiwani Zanzibar. Mahakama hiyo, imefikia uwamuzi huo leo, wakati viongozi hao walipofikishwa Mahakamani hapo. Hii ni kwa mujibu wa taarifa fupi niliyoibandua kutoka ukurasa wa ‘facebook’ iliyowekwa na Hamed Mazrui. Haikufafanua kwanini mahakama imefikia uamuzi huo. Kwa hivyo: Kutokana na hatua hio, viongozi hao sasa watakuwa wanakabiliwa na kesi inayoendelea katika mahakama kuu ya Vuga, mjini Zanzibar. Mara ya mwisho viongozi hao wa Dini, walipofikishwa mahakama kuu, chini ya Jaji Fatma Hamid, kesi yao ilipangwa kusikilizwa tena Aprili 11, mwaka huu.
Jaji Fatma, aliuagiza upande wa mashtaka kupeleka mahakamani kwa maandishi, ombi la kuzuia kutolewa kwa dhamana kwa washtakiwa hao. Jaji huyo aliongeza: Licha ya kwamba upande wa mashtaka umekata rufaa kuzuia kusikilizwa kwa ombi la dhamana, mahakama itaendelea kusikiliza kesi ya msingi pamoja na dhamana inayohusu viongozi hao. Upande wa Mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa Ramadhan Nassibu na Raya Msellem, huku upande wa utetezi unaongozwa na wakili, Salim Towfiq na wenzake.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO