Israel imethibitisha kuwa ilifanya shambulio la angani dhidi ya Syria ikilenga meli iliyokuwa imebeba shehena ya silaha zinazodaiwa kupelekwa kwa kundi la wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon usiku wa kuamkia jana.Serikali ya Marekani imesema inayumkinika kabisa kwamba Israel imefanya shambulio hilo. Shambulio hilo linashukiwa kulenga shehena ya silaha zinazodaiwa kupelekwa kwa kundi la wanamgambo wa Hezbollah, lenye makao yake katika nchi jirani ya Lebanon. Kituo cha Televisheni cha CNN kimesema taarifa hizo za kijasusi ni kwa mujibu wa mashirika ya kijasusi ya Marekani na mataifa ya magharibi. Afisa mwandamizi wa Marekani amekiambia kituo cha televisheni cha NBC kuwa mashambulio hayo huenda yanahusika na kuharibu kituo cha silaha za kemikali. Maafisa wa Ikulu ya Marekani na wizara ya ulinzi wamekataa kuzungumzia lolote kuhusu ripoti hiyo.Duru zinaarifu kuwa Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Alhamisi jioni alifanya kikao cha faragha na baraza lake la usalama mjini Jerusalem ambapo aliidhinisha shambulio hilo la angani.Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jafar amesema hana taarifa zozote kuhusu shambulio hilo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO