Thursday, May 02, 2013

KUENDELEA KWA MASHAMBULIZI YA ISRAEL UKANDA WA GHAZA


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa, mashambulizi ya ndege za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza ni hatua ya hatari na isiyokubalika. Fauzi Barhum msemaji wa Hamas amesema, lengo la mashambulizi hayo ni kulikosesha amani eneo la Gaza ili kufunika uhalifu unaotekelezwa na utawala huo katika mji wa Quds katika operesheni za kuuyahudisha mji huo, ujenzi wa vitongoji na kushtadi bila kukoma kukamatwa ovyo wakaazi wa mji huo. Barhum ameongeza kuwa, adui Mzayuni ametambua madhara na matokeo ya jinai zake hizo, na kwamba kushambuliwa Gaza ni hatua ya hatari na ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji vita.  Hii ni katika hali ambayo, maeneo mengine ya Palestina pia yanashuhudia vitendo vya utumiaji mabavu vya Israel huku wakaazi wake wakiendelea kukandamizwa. Israel mara kadhaa imekiuka makubaliano ya usitishaji vita iliyofikia na Wapalestina kufuatia kushindwa kwake katika vita vya siku 8 dhidi ya Gaza, Novemba mwaka 2012. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Israel ilitakiwa kutofanya shambulizi lolote dhidi ya maeneo ya Palestina na kujiepusha na hatua za kuwachokoza Wapalestina. Lakini jinai dhidi ya Wapalestina zimeongezeka hasa baada ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel kuunda Baraza lake jipya la Mawaziri linalohesabiwa kuwa la kufurutu ada zaidi kuliko la huko nyuma. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Marekani katika kutekeleza sera zao za kila siku za kinafiki mkabala na Wapalestina, wanataka kuonyesha kuwa Israel inakusudia kufanya jitihada mpya za kuleta amani katika eneo. Kuhusu hilo John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na baadhi ya waitifaki wake wa nchi za Kiarabu katika kikao kilichofanyika mjini Washington wametaka kuanza tena kwa mwenendo eti wa kusaka amani kati ya Israel na Wapalestina. Kikao hicho kilihudhiriwa pia na Joe Baiden Makamu wa Rais wa Marekani, Nabil al Arabi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Hamad bin Jassim al Thani, Waziri Mkuu wa Qatar. Katika mazungumzo hayo Kerry alitangaza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa Marekani kazungumzia tena mpango wa amani uliopendekezwa na Saudi Arabia mwaka 2002 unaojulikana kama 'Mpango wa amani wa Kiarabu.'
Mpango huo unaeleza suala la kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na Israel sambamba na utawala huo kuondoka katika baadhi ya maeneo unayoyakalia kwa mabavu ya Palestina yaani ardhi zilizoghusubiwa mwaka 1967. Sisitizo la Marekani la kufuatilia Mpango wa Amani wa Kiarabu linatokana na kuwa, mpango huo licha ya kushinikiza Mamlaka ya Ndani ya Palestina iipe fursa zaidi Israel, unafumbia macho haki za wananchi wa Palestina ikiwemo haki ya kurejea wakimbizi wa Palestina katika nchi yao, kadhia ya mateka wa Palestina na Quds kuwa mji mkuu wa nchi huru ijayo ya Palestina. Mabadiliko yanayojiri sasa huko Palestina yanaonesha kuwa, Wapalestina wanakabiliwa na hatua zinazoshtadi za utumiaji mabavu za Israel na vilevile njama za Marekani na serikali za Kiarabu, ambazo zinafuatilia kuwa na maelewano na utawala huo haramu. Lakini tahadhari ya Wapalestina kwa utawala huo na waungaji mkono wake inaonyesha jinsi walivyokuwa macho na njama hizo. Pia inaonesha kuwa, Wapalestina kamwe hawatishwi na siasa za ukandamizaji za Israel na kama huko nyuma hawatodanganyika na madai ya upatanishi ya maadui wa taifa hilo, yaani Marekani na baadhi ya serikali za Kiarabu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO