Sunday, May 05, 2013

IRAN YALAANI KUHUJUMIWA KWA KABURI LA HUJR BIN ADI, SYRIA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewaandikia barua wakuu wa taasisi kadhaa za kimataifa akilaani vikali kuvunjiwa heshima na kufukuliwa kaburi la sahaba wa Mtume SAW na Imam Ali (as), Hujr bin Adi, huko Syria. Katika barua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi mbali na kulaani kitendo cha watu wenye kufurutu mipaka ambao wamelihujumu kaburi hilo, ametaka hatua za dharura zichukuliwe kwa lengo la kuwaadhibu waliohusika na kitendo hicho kichafu. Salehi ametuma barua tatu tafauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO. Katika barua hiyo Salehi amelaani kitendo hicho kilicho dhidi ya ubinaadamu na kinachokiuka akhlaqi na kusema taasisi hizo za kimataifa zinapaswa kuchukua hatua kali na za kivitendo ili kurejesha heshima ya sahaba huyo wa Mtume SAW. Salehi amesema kuna haja ya kulinda maeneo matakatifu ya dini mbali mbali na kuonya kuwa kitendo kama hicho cha kuvunja kaburi la sahaba ni jambo linaloweza kuchochea mapigano ya kidini na kimadhehebu. Wakati huo huo wanazuoni wa ngazi za juu wa kidini kote Iran wamelaani vikali kitendo hicho kiovu cha kuhujumu kaburu la sahaba mkubwa wa Mtume SAW. Hali kadhalika wanafunzi wa vyuo vya kidini katika mji mtakatifu wa Qum na Tehran jana walifanya maandamano makubwa kulaani kitendo hicho cha kinyama. Siku ya Alkhamisi Mawahabi wenye misimamo ya kufurutu ada katika kundi la kigaidi Syria linalojiita ‘Jabhat An-Nusra’ walivamia na kufukua kaburi la Hujr bin Adi sahaba mkubwa wa Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW na Imam Ali (as) huko Damascus mji mkuu wa Syria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO