Friday, May 24, 2013

KATIBU MKUU WA UN AENDELEA NA SAFARI ZAKE AFRIKA

Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea na safari yake ya kuzitembelea nchi za eneo la Maziwa Makubwa la katikati mwa Afrika iliyoanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Jana Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliwasili katika mji wenye mgogoro wa kivita wa Goma wa mashariki mwa Kongo DRC kwa lengo la kuizindua jamii ya kimataifa kuhusu nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya ndani kwa miaka mingi sasa huku mamilioni ya watu wakiendelea kuteseka kutokana na mgogoro huo. Ban Ki moon aliwasili mjini humo masaa machache baada ya waasi wa M23 kutangaza kusimamisha vita karibu na mji huo ili kuruhusu kufanyika kwa usalama safari ya Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. Safari fupi ya Ban katika mji huo wenye utajiri mkubwa wa madini imefanyika siku tatu tu tangu mapigano makali yazuke kwenye eneo hilo kati ya wanajeshi wa serikali na waasi. Watu wasiopungua 20 wameripotiwa kuuawa katika mapigano hayo mapya yaliyoanza siku ya Jumatatu huku makombora yakiripotiwa kuanguka karibu na mji huo. Mbali na Kongo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametembelea pia nchi jirani na Kongo yaani Rwanda na anatarajiwa kutembelea pia Uganda.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO