Thursday, May 09, 2013

MAREKANI NA KOREA KUSINI ZAAPA KUIADHIBU VIKALI KOREA KASKAZINI PINDI ZIKISHAMBULIWA


Viongozi wa Marekani na Korea Kusini wametangaza kutokuwa na huruma yoyote dhidi ya Serikali ya Korea Kaskazini iliyo mstari wa mbele kwa kutoa vitisho vya kuyashambulia mataifa hayo mawili rafiki. Viongozi wa Marekani na Korea Kusini waliongia kwenye mgogoro na almanusura waingie vitani dhidi ya Korea Kaskazini wameahidi kuendelea kuimarisha ulinzi katika nchi zao kukabiliana na vitisho kutoka Pyongyang. Rais wa Marekani Barack Obama na Kiongozi wa Korea Kusini Park Guen-Hye ndiyo wametangaza msimamo wa nchi zao kuhusiana na mgogoro uliokuwa unaendelea baina yao na Korea Kaskazini.
Viongozi hao wamesema wataendelea kushirikiana kijeshi licha ya Korea Kaskazini kupinga vikali kile wanachokifanya na badala yake wanapaswa kusitisha mpango wao wa kutengeneza silaha za nyuklia. Rais wa Korea Kusini Park kwenye mazungumzo yake na Obama ametoa wito kwa Korea Kaskazini kuacha kutengeneza silaha za nyuklia ndipo watakapopata uungaji mkono kutoka Jumuiya ya Kimataifa na si kinyume na hapo.
Kiranja wa Dunia Rais Obama amesema wakati wa Korea Kaskazini kuendelea kuleta ubabe wao na kuanzisha migogoro umekwisha na hivyo hawatokuwa tayari kukaa kimya pindi vitisho vitakavyotolewa. Rais Obama amesema yeye na Park wamekubaliana kutokaa kimya kutokana na vitisho vinavyoendelea kutolewa na Korea Kaskazini na hivyo wanaendelea kuandaa mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanakuwa na usalama wa kutosha. Serikali ya Korea Kaskazini inayoongozwa na Kim Jong-Un imekuwa katika mvutano mkubwa na Marekani na Korea Kusini kutokana na nchi hizo kuendesha mazoezi ya pamoja ya kijeshi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO