Chama cha kihafidhina cha Golden Dawn nchini Ugiriki kwa mara nyingine tena kimeupinga mpango wa serikali ya nchi hiyo wa kujenga Msikiti katika mji mkuu wa nchi hiyo Athens. Ilias Kasidiaris msemaji wa chama hicho cha kihafidhina amewaambia waandishi wa habari mjini Athens kwamba iwapo serikali ya nchi hiyo haitaachana na mpango wa kujenga Msikiti huo, chama hicho kitawakusanya wafuasi wake zaidi ya laki moja na kuzuia ujenzi wa msikiti huo. Taarifa kutoka Athens zinasema kuwa, wafuasi wa chama hicho wamewaonya Waislamu wafute wazo la kujengwa msikiti mjini humo, la sivyo watachinjwa kama kuku. Taarifa zinasema kuwa, Athens ndio mji mkuu pekee barani Ulaya ambao hadi sasa hakuna hata msikiti mmoja. Imeelezwa kuwa, idadi ya Waislamu nchini Ugiriki inafikia laki tatu, na serikali ya Ugiriki imekubali matakwa ya Waislamu ya kujengwa Msikiti katika eneo ambalo awali kulikuwa na kambi ya kijeshi ya nchi hiyo. Baadhi ya viongozi wa Kanisa la Orthodox na chama cha Golden Dawn wanadai kuwa, ujenzi wa msikiti huo utasababisha kupotea utambulisho wa Kikristo nchini humo. Amma serikali ya Ugiriki imesisitiza mpango wake wa kujenga msikiti katika mji mkuu wa nchi hiyo hata kama kuna upinzani wa mirengo ya wahafidhina nchini humo. Waislamu wengi wanaoishi nchini humo wanatoka nchi za kaskazini mwa Afrika, Mashariki ya Kati na kusini mwa Asia.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO