Friday, June 21, 2013

BALOZI COOVADIA AILAUMU ISRAEL KWA UBAGUZI

Balozi wa zamani wa Afrika Kusini huko Tel Aviv amesema Israel ni utawala wa kibaguzi.
Ismail Coovadia Balozi wa Zamani wa Afrika Kusini mjini Tel Aviv katika barua aliyoawaandikia wanaharakati wa Palestina amesema,  utawala wa Israel ni sawa na utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwa madarakani Afrika Kusini. Amesema kuwa mwaka 2012 alipomaliza shughuli zake Tel Aviv, wizara ya mambo ya nje ya Israel ilimtaka apande mti katika bustani ya wanadiplomasia lakini alikataa ombi hilo. Ameongeza kuwa hangeruhusu mti upandwe kwa jina lake au jina la Afrika kusini katika ardhi ya Wapalestina iliyoporwa na Israel. Mwanadiplomasia huyo amesema sera za Israel za kuwabagua Wapalestina ni sawa na yale yaliyoshuhudiwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.  
Uhusiano wa Israel na Afrika Kusini umezorota katika miaka ya hivi karibuni na kufika kiwango cha chini kabisa mwaka 2012 wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ebrahim Ismail Ebrahim alipowataka watu wa Afrika Kusini kutotembelea Israel. Alisema Israel inawadhulumu Wapalestina sambamba na kukalia ardhi zao kwa mabavu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO