Rais Barack Obama wa Marekani hapo jana alitaka kumuondoshea wasiwasi Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuhusu upelelezi ulioripotiwa wa Marekani kwa washirika wake na wamekubaliana kuwa na mkutano wa ngazi ya juu kuhusu suala hilo hivi karibuni. Umoja wa Ulaya ulikuwa umedai Marekani iitolee ufafanuzi taarifa zilizotolewa na jarida la Ujerumani kwamba serikali ya Marekani imekuwa ikiwapeleleza washirika wake wa Ulaya na kusema litakuwa ni jambo la kufadhaisha iwapo taarifa hizo ni za kweli. Ripoti hizo zinakuja huku kukiwa na sakata la mfanyakazi wa zamani wa shirika la usalama la taifa la Marekani, Edward Snowden, kwa kuvujisha taarifa za ujasusi za serikali ya Marekani.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani imesema Obama na Merkel hapo jana walizungumza kwa njia ya simu ikiwa ni wiki mbili baada ya kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana mjini Berlin. Viongozi hao wamekubaliana kuwa na mkutano wa maafisa wa usalama wa Marekani na Ujerumani kulizungumzia suala hilo kwa kina hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO