Friday, June 21, 2013

WANANACHI BRAZIL WAKATAA KOMBE LA DUNIA KUFANYIKA KWAO

Watu zaidi ya milioni moja wameandamana kote Brazil kulalamikia viwango duni vya huduma za umma na mfumuko wa bei uliosababishwa na maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazonfayika nchini humo mwakani. Polisi nchini Brazil wanasema tayari mtu mmoja amepoteza maisha katika maandaamano hayo baada ya kugongwa na gari. Rais Dilma Roussef wa Brazil yuko chini ya mashinikizo makubwa kufuatia maandamano hayo ambayo yameripotiwa kuwa makubwa zaidi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Bi. Roussef amelazimika kubatilisha safari yake aliyokuwa amepanga kuenda Japan wiki ijayo.
Maandamano makubwa pia yameripotiwa katika mji mkuu Brasilia na miji ya Rio de Janeiro na Sao Paolo. Katika mji wa Salvador polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za plasiki kuwatawanya waandamanaji waliojaribu kuvuruga mechi ya jana ya Kombe la Confederations baina ya Nigeria na Uruguay. Maandamano yameanza wiki mbili baada ya serikali kuongeza nauli. Waandamanaji sasa wamezidisha matakwa yao na kutaka kupunguzwa kodi na bei za bidhaa muhimu. Aidha Wabrazil wamekasirishwa na huduma duni za umma katika hali ambayo serikali inatumia dola bilioni 26 fedha za umma kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia mwakani na Michezo ya Olimpiki mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO