Taarifa kutoka Ikulu ya Afrika Kusini zinasema kuwa hali ya kiafya ya rais mstaafu Nelson Mandela sio nzuri na kuwa imezorota katika saa 48 zilizopita. Baada ya kumtembelea hospitalini, mwanawe mkubwa wa kike Makaziwa, alisema hali inaonekana kuwa mbaya lakini akaongeza kuwa Mandela anaweza kuwasikia jamaa zake wanapomuita huku akijaribu kufungua macho yake. Makaziwe amesema “Nimekasirishwa sana. Kwa sababu Mandela ni kiongozi mashuhuri duniani, haimaanishi utu wake udhalilishwe pamoja na kuvuka mipaka kuingilia mambo yake binafsi Hapa naona kuna ubaguzi wa rangi, huku vyombo vingi vya kimataifa vikivuka mipaka, ni kama ndega aina ya Tai au Vulture wanaosubiri Simba kumla mnyama aliomuwinda kisha wakimbilie mzoga.
Wamevuka mipaka ya maadili. Wakati hayati Margaret Thatcher alipokuwa mgonjwa mbona sikuona, ukaribu wa vyombo vya habari kiasi ninachokiona kwa banangu? Ni kwa sababu hii ni nchi ya kiafrika. wanahisi kuwa hapa wanaweza kuvuka mipaka wanavyotaka, '' alisema Makaziwe Mapema leo, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alifutilia mbali ziara yake ya kwenda Musumbiji baada ya kumtembelea hospitalini aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Rais Zuma amesema kuwa Bwana Mandela yuko katika hali mbali ya afya. Msemaji wa Zuma Mac Maharaj alisema kuwa hali yake imedorora zaidi
Mandela ambaye, ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, amelazwa hospitalini tangu tarehe 8 mwezi Juni akiugua maradhi ya mapafu. Madaktari wanasemekana kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Mandela anapona. Vikundi vya watu wenye huzuni mkubwa kuhusu hali ya afya ya Mandela, walikusanyika nje ya hospitali alikolazwa, wakiwa na ujumbe wa ugua pole kwa Mandela.Wadadisi wanasema kuwa wananchi wa Afrika Kusini wanaonekana kuwa tayari kwa habari zozote sasa kuhusu hali ya Mandela.
"tutasikitika sana ikiwa tutapata habari za kifo chake, lakini pia tutakuwa tunasherehekea maisha yake. Amefanya mambo mengi zaidi kwa nchi yetu,'' alisema kijana John Ndlovu, mwenye umri wa miaka 25.
Zuma alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa marais nchini Msumbiji, hii leo lakini akaamua kuakhirisha safari yake. Taarifa kutoka kwa ofisi yake ilisema kuwa anaendelea kuwapongeza wananchi wa Afrika Kusini wanaoendelea kuiombea familia ya Madiba. Uamuzi wa Rais Zuma kufutilia mbali ziara yake ambako alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa kikanda kuhusu uekezaji anaonyesha wazi kuwa hali ya Mandela inaendelea kuzorota zaidi kulingana na mwandishi wa BBC mjini Johannesburg Mike Wooldridge.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO