Wednesday, February 13, 2013

KASHFA MTAWALIA WA KANISA KATOLIKI ZAMFIKISHA PABAYA PAPA

Papa Benedict XVI ametangaza kuwa, tarehe 28 mwezi huu atajiuzulu wadhifa wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani. Papa mwenye umri wa 85 ambaye kidhahiri inaonekana hawezi kutekeleza vizuri majukumu yake, yamkini ndiye Papa wa kwanza kujiuzulu katika kipindi cha miaka 700 iliyopita. Licha ya kuwa maradhi na udhaifu wa mwili uliotokana na umri mkubwa kinaonekana kuwa kisingizio kizuri cha kuhalalisha kujiuzulu Papa Benedick XVI, lakini weledi wa mambo wanaamini kuwa, changamoto na kashfa mtawalia zilizolikabili Kanisa Katoliki katika kipindi cha uongozi wake, ndio sababu kuu ya maji kumfika shingoni Papa huyo raia wa Ujerumani na kulazimika kuachia ngazi. 

Kashfa mbalimbali za kimaadili na kifedha zilizoikumba Vatican na Kanisa Katoliki katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikigonga vichwa vya habari na kuwa gumzo kubwa lisilokwisha. Ujio wa Papa Benedick XVI  kama kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki Duniani wadhifa ambao aliuchukua 2005 baada ya kufariki dunia Papa John Paul II, ulitazamwa na Wakatoliki kwa jicho la faraja huku akthari yao wakiaminmi kwamba, hatua hiyo ingeimarisha misingi na utambulisho wa ukatoliki ulimwenguni. Hata hivyo matukio yaliyoanza kulisakama kanisa hilo kama kashfa za ubakaji za makasisi na mlolongo mwingine wa kashfa chungu nzima zilizotokea katika kipindi cha Papa Benedict XVI, umelifanya Kanisa Katoliki kuporomoka zaidi katika historia yake baada ya harakati ya Martin Luther katika karne ya 16. Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi jambo ambalo kwa hakika limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki duniani na hata kuwafanya wafuasi wake kutilia alama ya swali uhalali wa kanisa hilo. Si hayo tu, kanisa Katoliki linakabiliwa na kashfa nyingine kama za ufisadi, uongozi mbaya na vita vya kuwania madaraka. Ukweli wa mambo ni kuwa, Vatican na Kanisa Katoliki limeshughulishwa na mambo mengi hususan masuala ya kimaadili, kifedha na vita vya kugombea madaraka. Suala la kutoruhusiwa kuoa makasisi katika madhehebu ya katoliki ni jambo ambalo limelifanya kanisa hilo kutumbukia katika utovu mkubwa zaidi wa maadili ambao ni kulawitiana na kunajisiwa watoto wadogo. Katika upande mwingine, jinamizi la ufisadi na ubadhirifu wa mali ni miongoni mwa matatizo ambayo yanahesabiwa kulitikisa kanisa Katoliki. Fauka ya hayo, matamshi na misimamo ya Papa Benedict XVI na Vatican katika masuala mengi kati ya tuliyoyataja yamelifanya kanisa hilo kupoteza itibari yake kimataifa. Makasisi ambao wanajulikana katika Ukristo kama baba wa kimaanawi, hii leo wamegeuka na kuwa tishio kubwa kwa watoto kutokana na kuripotiwa kesi nyingi za kuwanajisi watoto wadogo. Hapana shaka kuwa, hii haina maana kuwa hakuna makasisi wasafi kimaadili katika kanisa hilo, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, hilo ni pigo kubwa kwa itibari na uhalali wa kanisa hilo, pigo ambalo bila shaka halitafutika kwa urahisi. Kuongezeka takwimu za watu wanaojiua, vitendo vya ubakaji, kuzaliwa watoto nje ya ndoa na watu kuipa mgongo dini ni ishara za kusambaratika kimaadili jamii za Kimagharibi huku viongozi wa kanisa wakiwa na nafasi kubwa katika hayo.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO