Wednesday, June 19, 2013

WAZAYUNI WAPINGA KUUNDWA NCHI YA PALESTINA

Utawala wa Kizayuni wa Israel umepinga vikali mpango wa kuundwa nchi huru ya Palestina na kupelekea hatua hiyo kukabiliwa na radiamali za Wapalestina na fikra za walio wengi duniani. Mamlaka ya Ndani ya Palestina siku ya Jumatatu uliutaka utawala huo ghasibu utoe ufafanuzi wa kina kuhusiana na matamshi ya kijuba yaliyotolewa na Naftali Bennett Waziri wa Uchumi wa utawala huo pale aliposema kwamba mpango wa kuundwa serikali ya Palestina haupo kabisa. Nabil Abu Rudaina Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, matamshi ya Waziri Bennett ni hatari, kwani yanaweza kukwamisha juhudi za kuhuisha mwenendo wa mazungumzo ya amani. Abu Rudaina ameitaka jamii ya kimataifa kulaani matamshi hatari ya waziri huyo wa Israel kwani yanakinzana na juhudi za kimataifa za kuleta amani na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Bennett alisema kuwa, wazo la kuundwa serikali ya Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu halipo tena. Naftali Bennett ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha 'Jewish Home' amesema kuwa, tatizo la msingi ni kwamba viongozi wa Israel hawasemi wazi kwamba eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ni la Wazayuni. Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema, mpango wa Marekani wa kutaka kutatua mgogoro wa Palestina hauna kheri  yoyote kwa Wapalestina, bali ni mbinu za kutaka kupora na kukanyaga kikamilifu haki za Wapalestina za kuunda taifa la Palestina. Harakati hizo mpya za upande mmoja za Marekani, zimekuwa zikiwashajiisha viongozi wa utawala huo ghasibu kutoa matamshi ya kukera na kijuba dhidi ya Wapalestina. Mikakati mipya ya Marekani na utawala wa Kizayuni ya kutaka kuhuisha mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati ina lengo la kuwahamisha kikamilifu Wapalestina na kuwapeleka kwenye nchi nyingine, ili kujenga mazingira ya kukwamisha mpango wa kuundwa nchi ya Palestina. Viongozi wa Washington na Tel Aviv  daima wamekuwa wakizikalia kwa mabavu  haki za kurejea wakimbizi wa Kipalestina kwenye makazi yao ya asili na badala yake kushinikiza wapatiwe eti  makazi ya kudumu kwenye nchi walizokimbilia. Viongozi hao pia wanapanga mikakati ya kuwafukuza Wapalestina wanaoishi kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ili kuandaa mazingira ya kuundwa taifa la Kiyahudi. Mikakati hiyo inafanyika katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jordan amesisitiza udharura wa kuundwa nchi ya Palestina katika ardhi za Palestina na si vinginevyo. Akizungumza kwenye kikao cha kamati ya mashauriano ya Wakala wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia wakimbizi wa Palestina UNRWA, Nasser al Judeh amesema, kuna udharura wa kukomeshwa mateso ya miaka 60  dhidi ya Wapalestina na kuundwa nchi yao kwenye ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Kuchukuliwa misimamo ya kijuba na viongozi wa utawala wa Israel kunaonyesha kuwa, lengo la utawala huo la kuwasilisha mipango kama vile ya kuwapatia Wapalestina makazi ya kudumu nje ya Palestina, ni kutaka kuifuta kabisa kadhia ya Palestina. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, utawala huo huanzisha migogoro na machafuko kati ya nchi za Mashariki ya Kati, ili kupotosha fikra za walio wengi kuhusiana na kadhia ya kimsingi, yaani kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO