Thursday, July 11, 2013

MISRI YAISHUTUMU IRAN KWA KUINGILIA MASUALA YAKE

Misri imeishutumu Iran hii leo kwa kuingilia masuala yake ya ndani baada ya nchi hiyo kulikosoa jeshi kwa kumuondoa rais aliyechaguliwa kihalali Mohammed Mursi. Mapema wiki hii Iran ilisema kwamba kuondolewa kwa Rais Mohammed Mursi baada ya maandamano dhidi yake kufanyika ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa makini na kusema mkono wa nchi za Kigeni unaingilia maswala ya nchi za kiarabu. Baada ya tamko hilo Misri nayo ikasema taifa hilo la kiislamu la Iran, halina elimu ya maendeleo ya kidemokrasia inayopitia Misri.
Hivi sasa wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Misri imesema jambo la kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake kamwe halitakubalika. Nchi hiyo pia imetoa tamko kama hilo kwa Uturuki, baada ya kuikosoa serikali ya Misri kwa kumuondoa Mohammed Mursi. Mpaka sasa mataifa ya Magharibi yamekuwa makini sana kulikosoa jeshi kwa kumpindua rais Mursi.
Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu Hazem al-Beblawi, amesema hatazuia chama cha udugu wa kiiislamu kupata nyadhifa katika baraza lake la mawaziri bora tu wawe na ujuzi wa kushikilia nyadhifa hizo.
Hata hivyo taarifa hii inakuja wakati bado polisi nchini humo wakiendelea na oparesheni ya kuwakamata viongozi wa chama hicho. Akizungumza na chombo cha habari cha AFP Belawi amesema bado mpaka sasa yuko katika harakati ya kuunda serikali yake ya mpito.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO