Friday, July 05, 2013

RAIS MORALES APANGA KUUFUNGA UBALOZI WA MAREKANI NCHINI KWAO

Rais Evo Morales wa Bolivia ambaye ndege yake ilinyimwa kupaa katika anga ya Ulaya wiki hii kutokana na kushukiwa kuwa, huenda alikuwa ameandamana na Edward Snowden afisa wa zamani wa CIA ya Marekani anayesakwa na Washington amesema, nchi yake haihitaji ubalozi wa Marekani. Akizungumza huko Cochabamba Bolivia ambako viongozi wa Venezuela, Ecuador, Argentina na Uruguay wanakutana ili kuonyesha mshikamano na rais huyo, Morales ameilaumu Marekani kwa kuzishinikiza nchi za Ulaya zikatae kuruhusu ndege yake kupaa katika anga zao. Ameongeza kuwa hatua hiyo ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kwamba hatosita kuufunga ubalozi wa Marekani kwani nchi yao ina utu na uhuru, na bila Marekani wanaweza kuboreka zaidi kisiasa na kidemokrasia.
Jumanne nchi za Ufaransa, Ureno na Uhispania ziliinyima ruhusa ndege iliyokuwa imembeba Rais Morales, kutumia anga yao wakati rais huyo akirejea nyumbani baada ya kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa nishati huko nchini Russia na kulazimika kutua kwa dharura nchini Austria. Nchi hizo zilidai kuwa, hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na hitilafu za kiufundi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO