Friday, July 12, 2013

TANZANIA YAIONYA RWANDA JUU YA KUSHAMBULIANA

Serikali ya Tanzania, imeionya Rwanda isijaribu kuishambulia kijeshi nchi hiyo, vinginevyo itajibu uchokozi wowote ule kwa nguvu zake zote. Kauli hiyo nzito ilitolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania kufuatia matamshi makali yanayodaiwa kutolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na kutishia kuishambulia Tanzania. Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema ingawa Serikali ya Tanzania hadi sasa haijawahi kuwa na ugomvi wa aina yoyote ile na Rwanda, lakini amekiri kuwepo kile alichokiita kuwa ni 'kupishana lugha' baina ya Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame. Aidha Mkumbwa alisema kuwa Serikali ya Tanzania ina ushahidi wa maneno yanayodaiwa kutolewa na Rais Kagame katika moja ya hotuba zake alizozitoa tarehe 30 Juni, nchini Rwanda. Kwa mujibu wa maneno hayo, Kagame anadaiwa kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya Rais Kikwete kwamba anamsubiri katika wakati aujuao yeye ili amchape. Hii ni katika hali ambayo mbali na Kagame, viongozi kadhaa wa Rwanda wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya Rais Kikwete wa Tanzania. Hata hivyo Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania alisema, msimamo wa Tanzania uko pale pale kwa kuitaka serikali ya Kigali ikubali kukaa meza moja na wapinzani wake, ili kumaliza migogoro inayoendelea katika nchi hizo za maziwa makuu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO