Tuesday, July 09, 2013

UN YALAANI MAUAJI YA RAIA MISRI

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji yaliyofanywa na jeshi la Misri dhidi ya waandamanaji nchini humo na kusema kuwa, hali inayotawala nchini humo inatia wasi wasi. Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mauaji dhidi ya waandamanaji wa nchini Misri na kuyataka makundi yote ya kisiasa katika nchi hiyo kufanya kila yawezalo kuzuia kuzidi kuharibika hali ya mambo katika nchi hiyo.
Aidha Umoja wa Mataifa umetaka kufanyike uchunguzi huru na kushtakiwa wale wote waliohusika na mauaji hayo. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza wasi wasi wake pia kuhusiana na kutiwa mbaroni wanasiasa wengi nchini humo.
Ban Ki moon amewataka Wamisri kuandamana kwa amani na amelitaka jeshi la nchi hiyo liache kutumia mabavu dhidi ya waandamanaji hao. Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri imesema kuwa idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya jana ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya wafuasi wa Muhammad Mursi, imeongezeka na kufikia watu 53 wakiwemo watoto watano.
Ikhwanul Muslimin imesema kuwa, wafuasi wake wameuawa wakati jeshi la Misri lilipoushambulia umati wa watu hao waliokuwa wameketi chini nje ya kambi za wanajeshi hao kupinga kupinduliwa Rais Muhammad Mursi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO