Wednesday, March 27, 2013

IRAQ YAPINGA WAASI WA SYRIA KUPEWA UANACHAMA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Hoshyar Zebari amelaani hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ya kuwapa uanachama magaidi wa Syria kwenye jumuiya hiyo. Zebari amesema hatua hiyo inakiuka sheria na katiba ya Arab League. Akifafanua zaidi nukta hiyo, Hoshyar Zebari amesema wanachama wa jumuiya hiyo ni serikali za nchi za Kiarabu zilizochaguliwa kidemokrasia na wananchi na wala sio makundi yanayobeba silaha. Amesisitiza kwamba, magaidi wa Syria wanaungwa mkono zaidi na nchi za kigeni na hilo linakiuka vipengee muhimu vya mkataba wa kuundwa Jumuiya hiyo. Iraq ambayo kwa sasa ndiyo mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekuwa ikisisitiza kuwa njia pekee ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria ni kupitia mazungumzo kati ya serikali na waasi. Radiamali ya Iraq inakuja siku moja baada ya Arab League kuchukua nafasi ya Syria katika jumuiya hiyo na kuwapa magaidi wanaopigana na serikali ya Rais Bashar Asad.  

JESHI LA ISRAEL LAWAKAMATA VIONGOZI WA HAMAS

Jeshi la utawala haramu wa kizayuni wa Israel limewatia nguvuni viongozi 3 waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS baada ya kushambulia makaazi yao katika mji wa Khalil. Habari zinasema kuwa, wanajeshi wa Kizayuni wamemtia nguvuni Mohammad Jamal mwenye umri wa miaka 55 baada ya kumvurugia nyumba yake na kuchukua vitu vyake vya kibinafsi zikiwemo kompyuta na simu ya mkononi. Wazayuni hao maghasibu pia wamewakamata Amjad Hamouri na Abdul-Khaliq Natshe na kuwapeleka katika eneo lisilojulikana. HAMAS imelaani hujuma hiyo na kusema inakiuka makubaliano ya usitishaji vita yaliyomaliza mapigano ya siku 8 kati ya pande mbili hizo mwaka uliopita. Utawala haramu wa Israel umeendelea kukiuka haki za wapalestina sambamba na kukanyaga sheria za kimataifa huku Jamii ya kimataifa ikiendelea kuwa kimya. Uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani ndio sababu ya kuendelea kuvimba kichwa  utawala huo haramu wa Kizayuni.

KOREA YASEMA VITA YA NYUKLIA INAKARIBIA

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa ikisema vita vya nyuklia vinanukia katika Peninsula ya Korea. Taarifa ya Pyongyang kwa Umoja huo inasema kuwa, Marekani na Korea Kusini zinaendelea na chokochoko katika eneo hilo; jambo linalotishia kuanza kwa vita vya silaha za nyuklia. Taarifa hiyo pia imesisitiza kuwa, Korea Kaskazini itatumia kila njia kulinda ardhi na uhuru wake hata kama italazimika kutumia makombora ya nyuklia. Vitisho hivyo vimetajwa kuwa hatari zaidi kuwahi kutolewa na Pyongyang na kutokana na hali hiyo, Marekani imetangaza kuwa imeimarisha ngao zake dhidi ya makombora ili kukabiliana na vitisho hivyo. Majuma mawili yaliyopita, Korea Kaskazini ilitishia kuzishambulia Marekani na Korea Kusini kutokana na nchi mbili hizo kufanya maneva ya pamoja ya kijeshi katika Peninsula ya Korea. Pyongyang ilisema maneva hayo ni tangazo la moja kwa moja la vita dhidi yake. Tayari Korea Kaskazini imejiondoa kwenye mkataba wa usitishaji vita wa mwaka 1953 uliohitimisha vita kati yake na nchi jirani ya Korea Kusini.

RAIS WA SUDAN ATAKA WAASI KUSHIRIKI KATIBA MPYA

Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan, Ali Osman Taha ametoa wito kwa makundi ya waasi kushiriki mchakato wa kuunda katiba mpya ya nchi hiyo. Katika hali isiyo ya kawaida, Taha amewakaribisha Malik Agar na Abdul-Aziz al-Hilu; viongozi wa kundi la waasi la SPLM-North na kusema kwamba, kushiriki kwao kwenye mchakatu wa kuandika katiba mpya utahitimisha fujo na tandabelua katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kusini. Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan aidha amesema katiba mpya itafungua milango ya kuelekea kwenye demokrasia halisi pamoja na kuleta amani na utulivu ndani na nje ya Sudan. Vita na rangaito katika mikoa ya Kordofan Kusini na Blue Nile vilianza punde baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan mwezi Julai mwaka 2011 na nchi mbili hizo zimekuwa zikinyoosheana kidole cha lawama kuhusu uungaji mkono wa waasi katika majimbo hayo yaliyoko kwenye mpaka wao wa pamoja.

RUSSIA YAITAKA LEBANON KUTATUA MATATIZO YAKE WENYEWE

Serikali ya Russia imewataka Walebanon kuzuia uingiliaji wa aina yoyote ile wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Alexander Lukashevich ameyasema hayo leo na kusisitiza kuwa, nchi yake inaamini kwamba, Walebanon lazima watatue matatizo ya taifa lao wao wenyewe kwa njia za mazungumzo, likiwamo suala la uundwaji wa serikali mpya na kufanyika uchaguzi wa bunge na wasitoe mwanya kwa wageni kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Aidha ripoti hiyo imesisitiza kuwa, suala la usalama na utulivu nchini Lebanon ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na kwamba, taifa hilo la Kiarabu lazima lichukue hatua za lazima zitakazoiletea maslahi nchi hiyo na kusaidia demokrasia ya kweli na kuhakikisha usalama na ustawi unapatikana nchini humo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia piaamesema kuwa, nchi yake inaunga mkono haki ya kujitawala, uhuru wa nchi na juhudi zote zinazofanywa na makundi ya kisiasa na kidini ya Lebanon katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi hiyo hivi sasa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Lebanon, Mohammad Najib Mikati, alitangaza kujiuzulu na Rais Michel Suleiman wa nchi hiyo akakubali kujiuzulu kwake.

WAFUNGWA WA GUANTANAMO WAUNGWA MKONO

Wanaharakati wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia wameendelea kuunga mkono mgomo wa chakula wa wafungwa wa jela ya Guantanamo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa na televisheni ya PRESS TV, mgomo wa wanaharakati hao wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia unafanyika kama ishara ya kuungana na wafungwa hao wanaoendelea kuzuiliwa katika jela ya kutisha ya Guantanamo. Mgomo huo ulianza tarehe 24 Machi na unatarajia kuendelea hadi tarehe 30 ya mwezi huu. Mbali na mgomo huo, wanaharakati hao wamepanga kufanya mikusanyiko kadhaa katika nchi kadhaa katika kuwaunga mkono wafungwa hao. Tarehe 14 mwezi huu mawakili 45 wanaowatetea baadhi ya wafungwa wanaoshikiliwa katika jela hiyo ya Guantanamo walimtumia barua ya wazi Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel wakimtaarifu kuhusu suala hilo na kumtaka achukue hatua za haraka ili kumaliza mgomo huo. Wafungwa hao walianza mgomo huo tangu Februari 6 mwaka huu baada ya wafanyakazi wa jela hiyo ya Guantanamo kupora vitu vya wafungwa hao zikiwemo barua, picha na kuzivunjia heshima nakala za kitabu kitukufu cha Qu'rani wakati walipozikagua seli zao.

SHAMBULIO LA BOMU LAUA MMOJA RWANDA


Mripuko wa guruneti uliotokea mjini Kigali Rwanda umeua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wanane. Msemaji wa polisi ya Rwanda ameeleza kuwa guruneti hilo liliripuka jana jioni katika sehemu iliyoko baina ya kituo cha basi na soko moja kwenye eneo la Kimironko katika mji mkuu Kigali. Baadae polisi ilisema kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba watu wawili wametiwa mbaroni kwa kushukiwa kutekeleza shambulio hilo. Itakumbukwa kuwa milipuko mingine mitatu ya maguruneti ilitokea nchini Rwanda katika kipindi kama hiki mwaka jana yaani katika mwezi Machi. Mlipuko mmoja wa guruneti uliua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine watano huko kaskazini mwa Rwanda na milipuko mingine miwili  iliwajeruhi watu sita huko Kigali. Rwanda imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya guruneti tangu mwaka 2010 huku serikali ikiwanyooshea kidole cha tuhuma maafisa wawili wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo waliokimbilia uhamishoni.

MISIKITI NA NYUMBA KADHAA ZA WAISLAM ZACHOMWA MOTO MYANMAR


Misikti miwili na nyumba kadhaa za Waislamu zimeteketezwa kwa moto katika mashambulizi mapya dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Afisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa mashambulizi hayo yametokea katika vijiji vya eneo la Bago kaskazini mwa mji wa Yangon siku ya Jumatatu.
Amesema hakuna habari zozote kuhusu mauaji katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Waislamu walio wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Mnamo Machi 20 Mabuddha wenye misimamo mikali waliteketeza kwa moto nyumba za Waislamu na misikiti katika mji wa Meiktila nchini Myanmar ambapo watu 40 waliuawa na wengine 12,000 kuachwa bila makao. Wakati huo huo mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Vijay Nambiar, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuwaadhibu wanaofanya mashambulizi dhidi ya Waislamu.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, serikali ya Myanmar inawabagua, inawatesa na kuwakandamiza Waislamu wa Rohingya ambao idadi yao inafikia laki nane kwa madai kwamba, Waislamu hao ni wakimbizi waliokimbilia nchini humo wakitokea nchini Bangladesh.

Tuesday, March 26, 2013

KOREA KASKAZINI YAELEKEZA MIZINGA YAKE KWA VITUO VYA MAREKANI


Korea ya Kaskazini imeamuru mizinga yake iwekwe katika hali ya kivita, ikivilenga vituo vya  Marekani. Hayo yametangazwa na vyombo vya habari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Pyongyang. Vikosi vya maroketi na mizinga ya masafa marefu vimetakiwa kuwa katika hali ya tahadhari, vikilenga Marekani na visiwa vyake vya Hawaii na Guam, ambako kuna kambi za jeshi la nchi hiyo. Shirika la habari la Korea KCNA limeripoti kuwa kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un jana aliwatembelea wanajeshi walioko msitari wa mbele.
Korea ya Kaskazini imejenga zana za nyuklia, lakini haiaminiwi kuwa na uwezo wa kufyatua makombora ya masafa marefu. Utawala wa nchi hiyo ambao umetengwa na nchi nyingi duniani, siku za hivi karibuni umekuwa ukitoa vitisho kwa Korea Kusini na mshirika wake Marekani, baada ya nchi hizo kuanzisha mazoezi ya kijeshi pamoja katika eneo linalozunguka rasi ya Korea.

ISRAEL YAACHIA FEDHA ZA KODI KWA PALESTINA


Israel imesema itaanza tena kuipa mamlaka ya wapalestina fedha zinazotokana na kodi ambazo Israel huzikusanya kwa niaba ya mamlaka ya utawala wa Palestina. Fedha hizo zilisimamishwa baada ya Palestina kuomba na kupata hadhi ya mwanachama wa Umoja wa Mataifa asiye taifa huru.
Tangazo kuhusu kuachiwa kwa fedha hizo ambalo limetolewa na ofisi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu halikutoa maelezo zaidi kwa nini hatua imechukuliwa. Marekani na Israel zilipinga ombi la wapalestina kupandishwa hadhi na Umoja wa Mataifa na kuwa mwanachama asiye taifa.

IRAN YAITAKA UN IZUIE MATUMIZI YA KEMIKALI SYRIA

Dk Ali Akbar Salehi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa tena utumiaji wa silaha za kemikali uliofanywa na makudi ya kigaidi nchini Syria. Salehi amemuandikia barua Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo sanjari na kulaani kitendo cha magaidi wa Syria cha kutumia silaha za kemikali ameutaka umoja huo ufanye uchunguzi kuhusiana na jinai hizo za waasi na kuchukua hatua za lazima za kuzuia kukaririwa tena kitendo kama hicho. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza katika barua yake kwa Ban Ki-Moon kwamba, kuna haja kwa Umoja wa Mataifa kutuma timu ya wachunguzi huko Syria ili kufanya uchunguzi kuhusiana na jinai zilizofanywa na waasi hao wanaofanya mauaji kila leo dhidi ya raia katika nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha Ali Akbar Salehi amesisitiza kwamba, hatua ya waasi wa Syria ya kutumia silaha za kemikali katika mji wa Halab ni tishio la wazi kabisa dhidi ya amani na usalama na kwamba, hatua hiyo inakiuka wazi sheria za kimataifa na mikataba ya kimataifa hususan mkataba wa silaha za kemikali.

NAFASI YA CIA KATIKA KUYAPA SILAHA WAASI WA SYRIA

Gazeti la New York Times la nchini Marekani limeandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki kwa kusaidiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA mwaka jana ziliyapelekea tani 3500 za silaha makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji nchini Syria. Gazeti hilo limetegemea taarifa za minara ya kuongozea ndege, mahojiano na viongozi wa nchi mbalimbali na matamshi ya makamanda wa makundi ya waasi nchini Syria na kuandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki katika miezi ya hivi karibuni pia zimeongeza misaada yao ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi nchini Syria. Taarifa za kijasusi zinasema kuwa, jambo hilo lilianza mwanzoni mwa mwaka 2012 kwa kutumwa shehena ndogo nadogo na likaendelea mtawalia hadi mwishoni mwa msimu uliopita wa mapukutiko na kuongezeka mno katika miezi ya mwishoni mwa mwaka jana. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya New York Times, shehena hizo za silaha zinajumuisha zaidi ya shehena 160 za kijeshi zilizotoka kwa serikali za Jordan, Saudi Arabia na Qatar na kupelekwa katika viwanja vya ndege kadhaa vya Urutuki na baadaye kutumiwa magenge ya kigaidi nchini Syria. Gazeti hilo la Marekani limekiri pia kuwa, kutumwa shehena hizo za silaha kulileta mabadiliko katika vita vya ndani vya Syria. Limeandika kuwa, katika hali ambayo Rais Barack Obama wa Marekani alikuwa anadai kwamba anapinga kutumwa msaada wowote ule kwa waasi wa Syria isipokuwa wa kiraia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilitoa mchango mkubwa wa kutumwa silaha kwa magenge ya waasi ya Syria jambo ambalo linaonesha kuwa Marekani ina hamu ya kuona machafuko nchini Syria yanaendelea kupitia kuwaunga mkono waitifaki wake wa Kiarabu. Maafisa waandamizi wa Marekani ambao hawakutaka majina yao yatajwe nao wamesema kuwa, maajenti wa CIA wamezisaidia nchi za Kiarabu kununua silaha hizo na kuzituma kwa makundi ya kigaidi huko Syria. Serikali ya Uturuki nayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika jambo hilo. Wachambuzi wa masuala ya kudhibiti silaha za magendo wanasema kuwa, tani 3500 za silaha ni shehena kubwa sana na hili linaonesha ni kiasi gani taifa la Syria lilivyoshikamana na serikali yao pamoja na uimara wa utawala wa Rais Bashar al Assad kiasi kwamba umeweza kukabiliana vilivyo na ugaidi huo unaoiandama Syria kutoka kila mahala. Baada ya kuchaguliwa tena Obama kuwa Rais wa Marekani, viongozi wa Washington wamejitokeza na mikakati mipya ya kuzidi kushirikiana na Ufaransa, Uingereza, Uturuki, Saudia na Qatar kuyasheheneza silaha hatari hata za kemikali, makundi ya kigaidi huko Syria. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ni kichekesho kuzisikia Marekani na waitifaki wake hasa Uingereza, Ufaransa, Uturuki, Saudia na Qatar zikidai kuwa zinataka kuutatua mgogoro wa Syria wakati ndizo zinazochochea mauaji na ukatili wa makundi ya waasi yasiyo na chembe ya ubinaadamu huko Syria.

12 WAUAWA SHAMBULIO LA TALIBAN

Kwa akali watu 12 wameripotiwa kuuawa nchini Afghanistan kufuatia shambulio la wanamgambo wa Taliban mashariki mwa nchi hiyo. Duru za usalama zinaripoti kwamba, wanamgambo wa Taliban wamefanya shambulio katika kituo kimoja cha polisi mashariki mwa nchi hiyo na kupelekea watu 12 kuuawa wakiwemo polisi watano. Taarifa zaidi zinasema kuwa, kituo kimoja cha polisi katika mji wa Jalal-Abad kimeshambuliwa kwa mabomu yasiyopungua saba. Kundi la wanamgambo wa Taliban limetangaza kuhusika na shambulio hilo ambalo limepelekea pia makumi ya watu kujeruhiwa. Nchi ya Afghanistan inaendelea kushuhudia hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani, licha ya kuweko vikosi vya kigeni vinavyoongozwa na Marekani ambavyo vinadai viko katika nchi hiyo kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu.

CHRISTIAN RONALDO AKATAA KUBADILISHANA JEZI NA MUISRAEL


Christiano Ronaldo nahodha na mshambuliaji machachari wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Real Madrid ya Uhispania amekataa kubadilishana jezi na mchezaji mwenzake wa utawala wa Kizayuni wa Israel, mara baada ya kumalizika mechi kati ya timu hizo mbili za kuwania tiketi ya kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil iliyochezwa hivi karibuni huko Tel Aviv, Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Takwa la mchezaji wa Israel la kubadilishana jezi na Ronaldo lilikataliwa katika hali ambayo, wachezaji wote waliobakia wa Ureno walikubali kubadilishana jezi na wale wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kitendo cha kubadilishana jezi ni cha kawaida, na hasa kinaonyesha upendo na kinabaki kuwa kumbukumbu kwa wachezaji hao.
Aidha pambano hilo la kundi F, lilimalizika kwa timu hizo mbili kutoshana kwa  sare ya kufungana mabao 3-3. Ureno ilitangulia kupachika bao katika dakika ya 2 lililofungwa na Bruno Alves, na baada ya hapo Israel ilichachamaa na kusawazisha katika dakika ya 40, na kupachika mabao mengine mawili katika dakika za 40 na 70 yaliyofungwa na Ben Basat na Gershon. Ureno nusura iumbuke ugenini, lakini Fabio Coentrao anayechezea Real Madrid ya Uhispania alisawazisha katika dakika za majeruhi 90+3. Ronaldo aliulizwa swali la kichokozi  na lenye mtazamo wa kisiasa na mwandishi mmoja wa habari juu ya suala la nchi ya Israel na kujibu; anachojua yeye ni kwamba amecheza mechi hiyo nchini Palestina, na wala siyo Israel.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mara baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia eneo la Ukanda wa Gaza mwishoni mwa mwaka 2012, Ronaldo alitoa msaada wa kiasi cha euro milioni moja na nusu kwa ajili ya ukarabati wa shule ilizobomolewa kwa makombora ya ndege za utawala wa Israel. Aidha mwaka 2011 aliwahi kutoa viatu vyake na kupigwa mnada na fedha zilizopatikana alizikabidhi kwa Wapalestina kwa minajili ya kujenga na kukarabati shule za eneo la Ukanda wa Gaza.

WAISLAM WA UFARANSA WASHIKAMANA ZAIDI NA UISLAM


Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Sociovision nchini Ufaransa unaonesha kuwa, Waislamu nchini humo wanafungamana zaidi na misingi na thamani za kidini kuliko wafuasi wa dini nyingine za mbinguni.
Uchunguzi huo uliotolewa na taasisi hiyo hivi karibuni unaonesha kuwa, asilimia 68 ya Waislamu wa Ufaransa wanashikamana zaidi na thamani na misingi ya dini tukufu ya Kiislamu kuliko wafuasi wa dini nyinginezo. Uchunguzi uliofanywa mwezi Februari baina ya Waislamu, Wakristo na Mayahudi nchini humo unaonesha kuwa, asilimia 40 ya Mayahudi wanafungamana na thamani za kidini na asilimia 60 wanafungamana na thamani za kitaifa. Uchunguzi huo umeonesha kuwa, asilimia 63 ya Wakristo wanafungamana na thamani za kiutaifa na asilimia 37 tu ndiyo inashikamana na misingi na thamani za kidini. Kwa upande mwingine ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na gazeti la New York Time la nchini Marekani inaonyesha kuwa, kasi ya kuongezeka wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini Ufaransa imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.