Tuesday, March 26, 2013

KOREA KASKAZINI YAELEKEZA MIZINGA YAKE KWA VITUO VYA MAREKANI


Korea ya Kaskazini imeamuru mizinga yake iwekwe katika hali ya kivita, ikivilenga vituo vya  Marekani. Hayo yametangazwa na vyombo vya habari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Pyongyang. Vikosi vya maroketi na mizinga ya masafa marefu vimetakiwa kuwa katika hali ya tahadhari, vikilenga Marekani na visiwa vyake vya Hawaii na Guam, ambako kuna kambi za jeshi la nchi hiyo. Shirika la habari la Korea KCNA limeripoti kuwa kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un jana aliwatembelea wanajeshi walioko msitari wa mbele.
Korea ya Kaskazini imejenga zana za nyuklia, lakini haiaminiwi kuwa na uwezo wa kufyatua makombora ya masafa marefu. Utawala wa nchi hiyo ambao umetengwa na nchi nyingi duniani, siku za hivi karibuni umekuwa ukitoa vitisho kwa Korea Kusini na mshirika wake Marekani, baada ya nchi hizo kuanzisha mazoezi ya kijeshi pamoja katika eneo linalozunguka rasi ya Korea.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO