Tuesday, March 26, 2013

NAFASI YA CIA KATIKA KUYAPA SILAHA WAASI WA SYRIA

Gazeti la New York Times la nchini Marekani limeandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki kwa kusaidiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA mwaka jana ziliyapelekea tani 3500 za silaha makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji nchini Syria. Gazeti hilo limetegemea taarifa za minara ya kuongozea ndege, mahojiano na viongozi wa nchi mbalimbali na matamshi ya makamanda wa makundi ya waasi nchini Syria na kuandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki katika miezi ya hivi karibuni pia zimeongeza misaada yao ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi nchini Syria. Taarifa za kijasusi zinasema kuwa, jambo hilo lilianza mwanzoni mwa mwaka 2012 kwa kutumwa shehena ndogo nadogo na likaendelea mtawalia hadi mwishoni mwa msimu uliopita wa mapukutiko na kuongezeka mno katika miezi ya mwishoni mwa mwaka jana. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya New York Times, shehena hizo za silaha zinajumuisha zaidi ya shehena 160 za kijeshi zilizotoka kwa serikali za Jordan, Saudi Arabia na Qatar na kupelekwa katika viwanja vya ndege kadhaa vya Urutuki na baadaye kutumiwa magenge ya kigaidi nchini Syria. Gazeti hilo la Marekani limekiri pia kuwa, kutumwa shehena hizo za silaha kulileta mabadiliko katika vita vya ndani vya Syria. Limeandika kuwa, katika hali ambayo Rais Barack Obama wa Marekani alikuwa anadai kwamba anapinga kutumwa msaada wowote ule kwa waasi wa Syria isipokuwa wa kiraia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilitoa mchango mkubwa wa kutumwa silaha kwa magenge ya waasi ya Syria jambo ambalo linaonesha kuwa Marekani ina hamu ya kuona machafuko nchini Syria yanaendelea kupitia kuwaunga mkono waitifaki wake wa Kiarabu. Maafisa waandamizi wa Marekani ambao hawakutaka majina yao yatajwe nao wamesema kuwa, maajenti wa CIA wamezisaidia nchi za Kiarabu kununua silaha hizo na kuzituma kwa makundi ya kigaidi huko Syria. Serikali ya Uturuki nayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika jambo hilo. Wachambuzi wa masuala ya kudhibiti silaha za magendo wanasema kuwa, tani 3500 za silaha ni shehena kubwa sana na hili linaonesha ni kiasi gani taifa la Syria lilivyoshikamana na serikali yao pamoja na uimara wa utawala wa Rais Bashar al Assad kiasi kwamba umeweza kukabiliana vilivyo na ugaidi huo unaoiandama Syria kutoka kila mahala. Baada ya kuchaguliwa tena Obama kuwa Rais wa Marekani, viongozi wa Washington wamejitokeza na mikakati mipya ya kuzidi kushirikiana na Ufaransa, Uingereza, Uturuki, Saudia na Qatar kuyasheheneza silaha hatari hata za kemikali, makundi ya kigaidi huko Syria. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ni kichekesho kuzisikia Marekani na waitifaki wake hasa Uingereza, Ufaransa, Uturuki, Saudia na Qatar zikidai kuwa zinataka kuutatua mgogoro wa Syria wakati ndizo zinazochochea mauaji na ukatili wa makundi ya waasi yasiyo na chembe ya ubinaadamu huko Syria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO