Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudhriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
لَتَتَّبِعُنَّ سَنَنَ مَنْ قَبْلَكُمْ شِبْرًا بِشِبْرٍ وَذِرَاعًا بِذِرَاعٍ حَتَّى لَوْ سَلَكُوا جُحْرَ ضَبٍّ لَسَلَكْتُمُوهُ, قُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ, الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى؟ قَال: فَمَنْ
“Mtafuata nyendo za watu waliokuwa kabla yenu, kiganja kwa kiganja, mkono kwa mkono, hata wakiingia kwenye shimo la kenge mtawafuata)). Tukasema: Ee Mjumbe wa Allaah, ‘Je, Unamaanisha Mayahudi na Manaswara?’ Akasema: Kwani nani zaidi ya wao?” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Tunakaribia kuingia mwaka mpya wa Kikristo (wa kalenda ya Papa Gregory ijulikanayo kama ‘Gregorian Calendar’), na kuna Waislamu wengi wanaosherehekea mwaka huo mpya kama wanavyofanya makafiri, jambo ambalo halimo katika mafundisho ya Kiislamu.
Imekuwa ni kawaida Waislamu kujiunga na wafanyakazi wenzao au marafiki zao au majirani zao na kusherehekea sherehe hizi potofu, na kuwa na tabia isiyoendana na mwendo na mafundisho ya dini yetu tukufu. Swali ni kwamba, Vipi Muislamu ajitengee siku kama hizo na kusherehekea?
Jibu kutoka kwa Mwanachuoni wa Ummah, Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah kwamba:
"Sisi Waislamu tusifanye jambo lolote lilokuwa si la kawaida katika siku hizi. Iwe kama siku yoyote nyingine katika maisha yetu bila ya kuwa imekhusishwa na lolote kama mfano wao watu wa Vitabu walivyokuwa hawasherehekei wala kuzifanya siku zetu za ‘Iyd kuwa ni khaswa (maalum) kwao."
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuonyesha ubaya wa makafiri katika Aayah nyingi kama:
إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُواْ لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا
“Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.” [An-Nisaa: 101]
Vile vile Amewaita kuwa ni jamaa wa mashaytwaan na vikosi vyao.
Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah ametoa dalili za kuharamishwa kusherehekea Krismasi, sherehe za wafursi kama Neyrouz, Sherehe za Mayahudi na nyinginezo (kama hizi za mwaka mpya) kwa kusema kwamba zote zinakuja katika hukumu hiyo hiyo moja.
Muislamu anapaswa kukataa mwaliko huo wa kusherehekea mwaka mpya hata kama mwaliko huo umetoka kwa Muislamu mwenzake.
Makatazo yanaenea pia kwa kila jambo linalohusu sherehe hizo kama vile kusalimiana (kama kusema ‘Merry Christmas’ au ‘Happy New Year’ n.k.), kupeana zawadi, vyakula na kadhalika kwani haya ndiyo mambo yanayotendwa na kuwepo katika sherehe hizo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukamilishia dini yetu kabla ya kufa kwake na hakuna jambo lililokuwa jema ila ametujulisha na hakuna jambo baya ila ametukataza. Kwa hiyo katika mafundisho yake ya Sunnah hakuna hata mwaka mmoja uliothibitika kwamba Maswahaba walisherehekea mwaka mpya unapoingia hata wa Kiislam sembuse huo wa kikafiri!
Katika Sunnah, Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
‘‘Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja Madiynah na walikuwa wana siku mbili ambazo walikuwa wakipumzika na kustarehe na kucheza. Akasema: "Hizi ni siku gani?" Wakasema: Ni siku ambazo tulikuwa tukicheza na kustarehe katika Ujaahiliya". Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Allaah Amekupeni zilizo bora kuliko hizo; Yawmul-Adhwhaa (‘Iydul-Adhwhaa) na Yawmul-Fitwr (‘Iydul-Fitr) )) [Abu Daawuud]
Hii inaonyesha dhahiri kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha Ummah wake kusherehekea sherehe za makafiri na amefanya hima kuzifuta kwa kila njia.
Sababu mojawapo ya kuharamishwa sherehe zao kama za mwaka mpya ni kwa sababu ya maovu, uchafu na fitna zinazotokea humo. Na hata kama hakuna maovu yanayotendeka humo lakini kusherehekea kutasababisha uzushi huu kuendelea katika vizazi vyetu na kusababisha kuingiza mila za kikafiri ndani ya Uislamu.
Makafiri ni maadui wetu na maadui wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kwa hiyo inatupasa tujiepushe nao kadiri tuwezavyo ila tu kwa yale tuliyoruhusiwa katika sheria ya Kiislamu.
‘Umar Ibnul-Khatwtwaab amesema: "Jiepusheni na maadui wa Allaah katika sherehe zao"
Imeripotiwa katika mapokezi sahihi kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr akisema: “Yeyote anayeishi katika nchi isiyo ya Kiislam na akasherehekea sherehe yao ya mwaka mpya, na kuwaiga na akafa katika hali hiyo, basi atakusanywa pamoja nao siku ya Qiyaamah”.
WA ALLAAHU A’ALAM.